Mama wa mtoto huyo, Hadija Magalu
Mwanafunzi Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya
Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni akimuonesha mwandishi fomu ya
kuitwa shuleni
Mwenjuma M. Magalu (kulia) akiwa na Bibi yake nyumbani kwao Kijiji cha Msasa, wilayani Handeni
Na Joachim Mushi, Handeni
LICHA ya Serikali kuliarifu Bunge la Tanzania kuwa wanafunzi
wote waliofaulu darasa la saba mwaka 2011 kutoka mikoa 12 tayari wamejiunga na
kidato cha kwanza, imebainika bado kuna wanafunzi wameshindwa kujiunga na shule
kutokana na kipato duni cha familia zao.
Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya
Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni ni miongoni mwa wanafunzi walioshindwa
kujiunga na sekondari kutokana na mama yake kushindwa kumgharamia mahitaji ya
shule.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni
kijijini Msasa, wilayani Handeni, katika utafiti uliofanyika kwa ushirikiano na
Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), mama wa mtoto huyo Hadija Magalu
aliyetelekezwa na mumewe kwa muda mrefu alisema ameshindwa kumsomesha mwanaye
kutokana na kipato duni alichonacho.
Magalu alisema alipata taarifa za kufaulu kwa mwanae tangu
Desemba 12, 2011 na kuanza kujikusanya taratibu lakini hadi muda wa kwenda shule
ulipofika (Januari 9, 2012) alikuwa hajakamilisha baadhi ya vifaa vinavyohitajika
shuleni vikiwemo fedha ya ada na michango mingine.
“Naweza kukuonesha hata baadhi ya vitu ambayo nilikuwa
tayari nimenunua kama sare, kwanja na mahitaji
mengine madogo madogo…aliyenikwamisha na kunivunja moyo ni babayake (baba wa
mtoto), ambaye awali niliwasiliana naye kupitia kwa ndugu zake na kuahidi
angenisaidia ada lakini hakufanya hivyo hadi muda wa kwenda shule ulipofika,”
alisema Magalu.
Mume wa Magalu (jina tunalo) ametelekeza familia yake
(watoto wanne) pamoja na mkewe kwa zaidi ya miaka minne sasa kwa kisingizio
kwamba amekwenda nje ya Wilaya ya Handeni kutafuta maisha, huku mkewe akibaki
akiangaikia familia hiyo.
“Tumekuwa tukisikia tu kwamba ameonekana kijiji fulani
lakini ukifuatilia humpati, na mara nyingi anapowasiliana na ndugu zake ndio
wanatupa taarifa zake…nami niliwasiliana naye mara ya mwisho nikimpata taarifa
za mtoto kufaulu lakini hakutekeleza ahadi yoyote juu ya kunisaidia ada ya
mtoto.
Michango iliyomkwamisha mwanafunzi Mwenjuma Magalu kujiunga
na kidato cha kwanza ni ada ya sh. 20,000, fedha ya taaluma sh. 10,000, fedha
ya madawati 15,000, fedha ya sweta sh.10,000, kitambulisho sh. 5,000, ulinzi
sh. 5,000, tahadhari 5,000 pamoja na fedha kwa ajili ya nembo ya shule sh.
2,000.
Akihutubia Mkutano wa Saba wa Bunge la Tanzania
lililomalizika hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa kutoka mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa,
Mara, Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma na
Tanga, wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na
Kidato cha Kwanza.
Hata hivyo mwanafunzi Magalu kwa sasa anafanya vibarua kwa
moja ya kampuni za Kichina zinazofanya ujenzi wa barabara inayopita Kijiji cha
Msasa, kwa madai anatafuta fedha za ada na endapo akikamilisha atahakikisha
anaendelea na elimu ya sekondari hapo baadae.
Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, Hassan Mwachibuzi alisema ofisi yake
haina taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na shule, hivyo kumshauri mwandishi
amueleze mtoto huyo kufika ofisi za halmashauri ili aweze kujieleza na
ikiwezekana kusaidiwa.
“Kama huyo mtoto yupo
mwelekeze aje pale ofisini kuna wataalamu wa utambuzi watamuhoji na kuangalia
namna ya kumsaidia…sisi hatuna taarifa hizo na huenda wahusika wanatuficha,”
alisema kiongozi huyo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)