Baadhi ya wakazi wa eneo
la Kisarawe Mjini wakiwa wamepanga foleni ndefu za vyombo vya kutekea
maji kwenye moja ya mabomba ya umma eneo hilo hivi karibuni. Kumekuwa na
shida kubwa ya upatikanaji wa huduma za maji kwa matumizi ya nyumbani
na shughuli nyingine za wananchi eneo la Kisarawe hasa Kata ya
Maneromango iliyopo nje kidogo ya mji huo. (Picha na Joachim Mushi wa
Thehabari.com)
Na Joachim Mushi, Kisarawe
MGOGORO wa ukosefu wa maji ya matumizi ya nyumbani na
shughuli nyingine bado ni kero kubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani
Pwani hasa katika Kata ya Maneromango iliyopo nje ya Mji wa Kisarawe.
Uchunguzi uliofanywa na Thehabari.com hivi karibuni maeneo
ya Kata ya Maneromango imebaini bado kuna shida kubwa ya maji kwa wakazi wa
eneo hilo licha
ya uwepo wa baadhi ya visima vya umma na watu binafsi vilivyochimbwa hivi
karibuni.
Shida ya maji imepungua katika baadhi ya shule za msingi na
sekondari pamoja na vituo vya afya pekee baada ya kujitokeza wafadhili kujenga
mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua katika shule hizo na kituo cha afya.
Shule ambazo awali zilikuwa na shida kubwa ya maji na sasa
zimenufaika na msaada wa kujengewa mfumo wa uvunaji maji ya mvua eneo la
Maneromango ni pamoja na shule za msingi, Mengwa na Maneromango, Shule ya
Sekondari Maneromango pamoja na kituo cha Afya cha Maneromango.
Akizungumza na mtandao huu Said Mzara mkazi wa Kijiji cha
Boga amesema unafuu wa kupatikana kwa maji hutokea mvua zinaponyesha tu ambapo
wananchi wengi hupata maji lakini baada ya kipindi hicho shida ya maji hurejea kama kawaida.
“Wanaonufaika kwa kiasi kikubwa na huduma za maji ni shule
za msingi na sekondari pamoja na kituo chetu cha afya ambao wamejengewa mfumo
wa kuvuna maji ya mvua, ukweli ni kwamba bado wananchi tunaitaji msaada wa
kuboreshewa huduma za maji hasa visima vya umma,” alisema Mzara.
Muhamed Omar mkazi wa Kitongoji cha Msegamo anasema ushauri
wa kuvuna maji ya mvua unaotolewa na wataalam na baadhi ya viongozi ni mgumu
kwa wananchi wengi kutokana na kumiliki nyumba za nyasi ambazo ni hafifu kwa
uvunaji maji ya mvua.
“Wanashauri tuvune maji ya mvua suala hili ni gumu kwa
asilimia kubwa ya wakazi kwani bado tunamiliki nyumba za nyasi, isipokuwa kwa
wakazi wa mjini sasa kwa hali hii utavunaje maji ya mvua?,” alihoji Omar ambaye
ni mkulima na mfanyabiashara ndogo ndogo.
Mwandishi wa habari hizi ametembelea pia maeneo ya katikati
ya Mji wa Wilaya ya Kisarawe ambapo amebaini bado kuna shida kubwa ya maji
kutokana na kubaini foleni kubwa za maji katika maeneo ya mabomba ya maji.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)