Dr. Helen Kijo-Bisimba
----
Ndugu wanahabari na wananchi kwa ujumla,
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu tumefuatilia kwa makini sana mchakato wa
Katiba mpya kuanzia ulipoanza mpaka hapa ulipofikia.
Sote
tunafahamu kwamba hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuteuliwa na kuapishwa
kwa wajumbe wa tume ya kukusanya maoni juu ya mchakato mzima wa Katiba
mpya na namna ambavyo wananchi wangependa iwe.
Tunependa
kupompongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kupitia wizara ya Katiba
na Sheria kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa kwenye mchakato mzima.
Tunatoa
pongezi kwa uteuzi wajumbe wengi waliobobea katika fani mbalimbali za
Sheria, Siasa na Masuala ya kijamii. Tumefurahi kuona kuwa Mheshimiwa
Rais amemteua kuwa mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba ambae
tulishaona kazi yake nzuri hususan pale alipoongoza vizuri tume ya Rais
iliyohusu masuala ya Rushwa. Tuna imani kuwa ataongoza tume hii kufanya
kazi nzuri.
Wajumbe wa Tume hii ni 32 (akiwemo mwenyekiti na makamu) waliapishwa tarehe 13/04/2012.
Wajumbe hao ni kama ifuatavyo;
Mwenyekiti
wa Tume ambaye ni Jaji Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu
Mstaafu Agustino Ramadhani.Wajumbe wa tume toka Tanzania Bara ni Prof.
Mwesiga L. Baregu, Nd. Riziki Shahari Mngwali, Dr. Edmund Adrian
Sengodo Mvungi, Nd. Richard Shadrack Lyimo, Nd. John J. Nkolo, Alhaj
Said El- Maamry, Nd. Jesca Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba J. Kabudi,
Nd. Humphrey Polepole, Nd. Yahya Msulwa, Nd. Esther P. Mkwizu, Nd.
Maria Malingumu Kashonda, Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb), Nd. Mwantumu
Jasmine Malale Na Nd. Joseph Butiku. 2
Wajumbe
wengine 15 ni kutoka Tanzania Zanzibar. Wajumbe hao ni Dkt. Salim Ahmed
Salim, Nd. Fatma Said Ali, Nd. Omar Sheha Mussa, Mhe. Raya Suleiman
Hamad, Nd. Awadh Ali Said, Nd. Ussi Khamis Haji, Nd. Salma Maoulidi,
Nd. Nassor Khamis Mohammed, Nd. Simai Mohamed Said, Nd. Muhammed Yussuf
Mshamba, Nd. Kibibi Mwinyi Hassan, Nd. Suleiman Omar Ali, Nd. Salama
Kombo Ahmed, Nd. Abubakar Mohammed Ali na Nd. Ally Abdullah Ally Saleh.
Mapungufu tunayoyaona;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona mapungufu makubwa mawili kwa tume hii
i) Kuwemo kwa mbunge na mjumbe wa baraza la wawakilishi
ii) Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine mfano vijana
Wawakilishi kuwa wajumbe
Kituo
hakikubaliani kabisa na uteuzi wa wakilishi wa wananchi (Mbunge na
Mjumbe wa Baraza la wawakilishi). Wajumbe hawa ni Mhe. Al-Shaymaa J.
Kwegyir (Mb) Tanzania Bara na Raya Suleiman Hamada mwakilishi Baraza la
Wawakilishi Zanzibar.
Sababu
kubwa za kutokukubaliana na uteuzi wa wajumbe hawa ni kuwa kwanza, hawa
watashiriki kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (constituent
assembly) kwa hiyo kuna ‘mgongano ulio dhahiri wa kimaslahi’. (kwa mujibu wa vifungu cha 6 na 22 (1) (a) na (b) vya sheria Namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba, 2011)
Pili
wananchi wanaowawakilisha watanyimwa haki yao ya kuwakilishwa kwa
kipindi chote cha miezi 18 mpaka ishirini ambacho tume itafanya kazi
kwa mujibu wa sheria.
Tatu,
kuna majina mengi ambayo mheshimiwa Rais alipelekewa yenye sifa za
kutosha angeweza kuwateua. Kulimbikiza kazi nyingi kwa watu wale wale
si afya kwa demokrasia.
Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine
Katika
tume hii tumeona kuna uwakilishi finyu sana wa makundi kwa mfano
wanawake wako 10 kati ya 32, yaani sawa na asilimia 27% tu!
Tungetegemea asilimia 50% kwa 50% kwani Tanzania imesaini na kuridhia
mkataba wa nyongeza wa maendeleo ya kijinsia kusini mwa Afrika yaani
SADC Gender Protocol. Pia 3
Tanzania
ina asilimia ya 51 ya idadi ya wanawake ambao miongoni mwao wengi wana
utaalamu na sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.
WITO
I) Tunapenda
kutoa wito kwa serikali kuwa mchakato wa Katiba ni wa muhimu sana
hautakiwi kuchukuliwa kwa wepesi. Mchakato huu unajenga mustakabali wa
Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Hivyo katika maamuzi yote
yanayochukuliwa, kuwe na jicho la HAKI ZA BINADAMU na utawala wa
sheria.
II) Pia
tunapenda kutoa wito kwa WANANCHI wote wa Tanzania, mijini na vijijini,
wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara, TUSHIRIKI kwenye mchakato
huu. Tunawasihi kuwa Tume ya Katiba itakapokuja kwenye maeneo yetu
tuhudhurie mikutano yote na kutoa maoni yetu juu ya Katiba Mpya.
Wananchi
katika makundi au mtu mmojamoja anaweza kupeleka maoni ya maandishi
kwenye tume mara anuani itakapojulishwa kwa wananchi.
III) Mwisho
tunatoa wito kwa tume kuhakikisha watu wote wanatoa maoni yao bila
ubaguzi. Makundi yote ya jamii yafikiwe (Wanawake, wanaume, watu wenye
ulemavu na watoto wenye umri wa kutoa maoni).
Asanteni kwa kunisikiliza,
Dr. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi mtendaji- LHRC
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)