Na Mwandishi wetu
WAKATI taarifa ya Kamati ya wabunge wa CCM chini ya Waziri
Mkuu,
Mizengo Pinda, juzi iliridhia mawaziri wote wanaokabiliwa na tuhuma za
ubadhirifu kwenye wizara zao wajiuzulu, jana Rais Jakaya Kikwete
aliwasili nchini akitokea Brazil akiwa na msimamo tofauti.
Taarifa
zinasema kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Kikwete na Pinda
yaliyolenga kunusuru serikali yao lakini walitofautiana kuhusu hatua
inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.
Msimamo
wa Pinda inadaiwa kuwa anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma
waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini Rais Kikwete amesema
mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la
upepo tu, liachwe litapita.
Tanzania Daima Jumapili limeelezwa kuwa rais anakataa shinikizo hilo kwa madai serikali haipaswi kuyumbishwa yumbishwa.
Miongoni
mwa mawaziri wanaopaswa kuondoka ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo;
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami na naibu wake, Lazaro
Nyalandu; Waziri wa Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa, George
Mkuchika na naibu wake, Aggrey Mwanri; Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda
na naibu wake, Lucy Nkya na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu.
Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Habari
zinasema Rais Kikwete na Pinda walitofautiana juu ya hatua dhidi ya
mawaziri hao, hivyo kuwafanya baadhi ya mawaziri kutamba mitaani kuwa
hawang’oki madarakani kwa sababu tayari bosi wao ameonyesha kutounga
mkono tuhuma zinazoelekezwa kwao na wabunge wa upinzani na CCM.
Habari hizi zinasema pia kwamba Pinda amekuwa hafurahishwi na msimamo wa ‘bosi’ wake, hasa katika kushindwa kutoa uamuzi mgumu.
Zinadai
kuwa rais amekuwa na tabia ya kuacha upepo uchukue nafasi yake wakati
Pinda anataka baadhi ya watu wawajibike bila kujali nyadhifa zao au
ukaribu na kiongozi mkuu wa nchi ili kurejesha imani ya serikali kwa
wananchi.
Pinda
inadaiwa amekuwa akitaka maamuzi magumu yafanyike, kwakuwa yeye ndiye
anayesulubiwa na maswali pamoja na hoja za wabunge wawapo bungeni.
Baadhi
ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili, wameweka wazi kuwa
kama Rais Kikwete ataamua kuwalinda na kuwatetea mawaziri wake basi
watawaondoa kwa mkakati tofauti utakaomlazimisha rais kukubaliana na
hoja za wabunge.
Baadhi
ya wajumbe waliozungumza na gazeti hili waliweka wazi hatua hiyo
inahitaji muda na mipango madhubuti na wao wapo tayari kufanya hivyo,
kwani nchi inazidi kudidimia kwenye umaskini huku watu wake wakikosa
huduma muhimu za kijamii.
Walisema
kwa muda mrefu wamekuwa wakiwalalamikia watendaji wa serikali na chama
tawala lakini rais amekuwa mgumu wa kuyashughulikia matatizo hayo.
Wanasema
rais ndiye kikwazo kikubwa cha maendeleo ya chama chao na serikali,
hasa kwa kuwateua mawaziri, wakurugenzi na maofisa wengine bila
kuangalia uwezo wao wa kiutendaji.
“Kaka
kwenye Bunge la Februari kuna mbunge alitoa kauli kuwa kama tunaona
mambo hayaendi serikalini tupige kura ya kutokuwa na imani na rais, watu
walimshambulia. Sasa tunaona umuhimu wa kauli yake ile,” alisema mbunge
mmoja.
Tanzania
Daima Jumapili, limedokezwa makada wa CCM wameanza kuingiwa na hofu ya
kubomoka kwa chama chao hasa baada ya makada wenzao kuanza kujiunga na
vyama vya upinzani.
Wanasema
wakati makada wa chama hicho wakiendelea kukihama uongozi wa CCM
hauonekani kuchukua hatua zinazostahiki dhidi ya viongozi wanaochangia
wananchi wakose imani na chama tawala.
Mbunge
wa Ludewa, Deo Filikunjombe, aliweka wazi kuwa wabunge wa CCM ni lazima
wakemee ubadhirifu kwakuwa Tanzania si mali ya CCM.
Mbunge huyo alikwenda mbali kwa kumtaja Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, kuwa ni mwizi, mwongo na mbadhirifu wa mali za umma.
Mawaziri wasuasua kuwasilisha barua
Hadi
jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hajapokea barua ya kujiuzulu
kutoka kwa waziri yeyote huku akiweka wazi kuwa kesho atatoa taarifa
kamili juu ya jambo hilo.
Juzi
vyombo vya habari vilipata taarifa kutoka kwenye kikao cha wabunge wa
CCM kuwa baada ya wabunge kuzituhumu baadhi ya wizara kukithiri kwa
ubadhirifu mawaziri wake wameamua kujiuzulu.
Taarifa
hizo zilidokeza kuwa mawaziri hao walishinikizwa kuachia nyadhifa zao
ili kukinusuru chama na serikali dhidi ya hasira za wananchi wanaokerwa
na ufisadi.
Chami atoboa siri
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, amejitetea kuwa wizara yake
haimlindi Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, kama alivyotuhumiwa
na baadhi ya wabunge.
Alisema
amesononeshwa na taarifa ya ukaguzi wa CAG juu ya TBS iliyotolewa kwa
waheshimiwa wabunge bila yeye mwenyewe au wizara kupewa nakala kwa
kipindi cha wiki nzima.
Alisema
kuwa baada ya kusikia kuwa waheshimiwa wabunge wengi wanayo taarifa
hiyo na hata naibu wake kukiri bungeni kwamba taarifa imetoka wakati
yeye hana nakala, alikwenda kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah
na kuiomba nakala ya taarifa hiyo.
Alibainisha
kuwa baada ya kufanya ufuatiliaji katika ofisi ya CAG ilikiri kuigawa
kwa wabunge na kusahau kuipeleka kwa wizara hiyo ambayo ndiyo
inayohusika.
“Hapa
wasomaji wapime wenyewe. Inawezekanaje taarifa ya CAG iliyoandikwa
kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara yangu, iwafikie wabunge huku
wizara yangu itakayotakiwa kuifanyia kazi taarifa yenyewe haipewi
nakala, eti kwa kughafilika?
“Ni
ukweli ofisi ya CAG walighafilikiwa, au jambo hili limesukwa ili
kuniaibisha mimi mbele ya Watanzania, rais aliyeniteua na hasa wapiga
kura wangu wa Moshi Vijijini?” alihoji.
Nundu ajitetea
Naye
Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alisema tuhuma dhidi yake
zilizoelekezwa na baadhi ya wabunge, hazina ukweli na zimelenga
kumchafua.
Alisema
kilichoelezwa na Kamati ya Miundombinu ni uongo na uzushi, kwani
nyaraka walizozitumia kuorodhesha tuhuma dhidi yake si halali.
Kuhusu
kuingilia utendaji wa Mamlaka ya Bandari kwa masilahi binafsi, alisema
si kweli, akaongeza kuwa kinachomponza ni kuipinga kampuni inayotetewa
na menejimenti isipewe zabuni ya kufanya upembuzi yakinifu peke yake na
kwenda kukopa na baadaye iruhusiwe kujenga gati namba 13 na 14.
“Wanasema
namtaka mwekezaji ambaye makubaliano yanaonyesha atamiliki gati hilo
kwa miaka 45. Nachelea kusema ni uongo na uzushi,” alisema Nundu.
Mkuchika apata kigugumizi
Naye
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, alipoulizwa juu ya suala hilo
alishindwa kukubali wala kukataa iwapo ataandika barua ya kujiuzulu.
Alimtaka mwandishi amuulize Katibu wa Kamati ya Uongozi.
Chanzo Tanzania Daima 22/april/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)