Ujumbe
wa ubalozi wa China ukiongozwa na Balozi wake nchini Tanzania Lou You
Qing (kulia), uliofika nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko Mbweni kwa ajili ya
kujitambulisha na kubadilishana mawazo.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na
balozi wa China nchini Tanzania Lou You Qing, wakati ujumbe wa ubalozi
huo ulipofika nyumbani kwake Mbweni kwa ajili ya kujitambulisha na
kubadilishana mawazo. Katikati ni mkalimani wa lugha ya Kichina na
Kiingereza Fang Wang.Picha na Salmin Said-Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa
Rais Zanzibar
---
China imesema itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu, afya, kilimo na utafiti.
Balozi
wa China nchini Tanzania Bw. Lou You Qing ambaye aliongoza ujumbe wa
ubalozi huo, ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Balozi
Qing na ujumbe wake walifika nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais
huko Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, kwa ajili ya kujitambulisha
rasmi na kubadilishana mawazo juu ya maeneo tofauti ambayo China na
Zanzibar zinaweza kushirikiana.
Amesema
China iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza kilimo cha
mpunga pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maendeleo, ikiwa ni pamoja
kuyaalika makampuni ya kichina kwa ajili ya kuangalia namna yanavyoweza
kusaidia katika ujenzi wa bandari mpya ya kibiashara Zanzibar.
Balozi
Qing amesema China na Zanzibar zina historia ya muda mrefu katika
nyanja mbali mbali zikiwemo siasa na uchumi, na kutaka mashirikiano
hayo yaendelezwe kwa maslahi ya pande hizo mbili.
Amefahamisha
kuwa uhusiano huo wa kunufaishana, sana unaonekana kukua kwa kasi
kubwa kutokana na kuwepo na mawasiliano ya karibu miongoni mwa wananchi
wa pande hizo mbili, na kwamba hali hiyo itahamasisha kasi ya
maendeleo hapa Zanzibar.
Amesifu
juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha miundominu ya kiuchumi, sambamba na kudumisha hali ya amani,
mambo ambayo ni muhimu katika kuchochea maendeleo.
Amesema
hatua hizo muhimu, zinaweza kuisadia Zanzibar kupiga hatua kubwa za
maendeleo ikizingatiwa kuwa inazo rasilimali muhimu zikiwemo historia,
utamaduni, bahari na jiografia ya visiwa vya Zanzibar ambavyo ni muhimu
katika kukuza sekta ya utalii.
Amebainisha
kuwa kihistoria China ilikuwa nchi maskini, lakini imeweza kupiga
hatua kubwa za maendeleo kutokana na mipango na mikakati imara
iliyojiwekea ambapo Zanzibar inaweza kujifunza na kukuza uchumi wake.
Nae
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema
Zanzibar inayo mengi ya kujifunza kutoka kwa marifiki zao wa China
katika jitihada zake za kujikwamua kiuchumi.
Amesema
hatua ya Serikali ya China kukubali kuwapeleka mawaziri na maofisa wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenda kujifunza nchini China ni
muhimu katika kufikia malengo yake iliyojiwekea.
Maalim
Seif amepongeza mchango wa Serikali ya China katika kukuza maendeleo
ya Zanzibar ambapo nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia
maendeleo ya sekta mbali mbali zikiwemo elimu, afya na Michezo.
Amesema
msisitizo wa mashirikiano kwa sasa unapaswa kuekezwa katika sekta za
viwanda vidogovidogo, kilimo, utafiti na utalii, ambapo China ina
uzoefu mkubwa katika nyanja hizo.
Amesema
Zanzibar ambayo inakabiliwa na tatizo la uhaba wa ardhi, inajipanga
kuendeleza sekta hizo za kiuchumi hasa kilimo cha umwagiliaji ambacho
kinaweza kuinufaisha Zanzibar na hatimaye kupunguza utegemezi wa
chakula kutoka nchi nyengine.
Sambamba
na hilo Maalim Seif amesema serikali inajipanga kutekeleza mpango wake
wa kujenga bandari kubwa ya kibiashara katika eneo la Mpigaduri, na
kuiomba China kuangalia uwezekano wa kusaidia utekelezaji wa mpango
huo.
Amesema
kufanikiwa kwa mpango huo, kutairejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa
kituo kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo meli
kubwa za mizigo na kitalii zitaweza kufunga gati na kuwawezesha
wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila usumbufu.
Amefahamisha
kuwa inawezekana kwa Zanzibar kujikwamua kiuchumi, kwa kutumia uzoefu
wa China ambayo katika kipindi cha miaka 40 iliyopita ilikuwa nchi
maskini na sasa uchumi wake unaendelea kukua kwa kasi kubwa kuelekea
kutawala uchumi wa dunia.
Na
Na Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)