TAARIFA KWA UMMA
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea kuchambua wasifu wa
wajumbe walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa tume ya
mabadiliko ya katiba.
CHADEMA
kitatoa tamko juu ya uteuzi wa tume husika baada ya uchambuzi
kukamilika wa kutafakari iwapo uteuzi husika umezingatia matakwa ya umma
na dhamira ya kujenga muafaka wa kitaifa wa kuwa na katiba mpya na
bora.
Pamoja
na kutaja majina ya wajumbe wa tume, CHADEMA kilitarajia kwamba Rais
Jakaya Kikwete angeeleza pia ratiba ya kufanyika kwa marekebisho mengine
muhimu ya awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya
kutunga katiba mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha
wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia
katika hatua husika.
Katika
muktadha huo, Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) iliyoundwa tarehe 20 Novemba 2011 kwa ajili ya
kukutana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ya
mwaka 2011; itafanya kikao chake karibuni kupitia taarifa ya uchambuzi
unaoendelea kufanywa juu ya uteuzi uliofanyika wa wajumbe wa tume na
tamko litatolewa kwa umma kuhusu mchakato huu muhimu kwa maslahi ya
taifa.
Itakumbukwa
kwamba tarehe 27 na 28 Novemba 2011 Rais Kikwete alifanya mkutano wa
siku mbili na viongozi wa CHADEMA kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko
ya katiba na pande mbili kukubaliana kuhusu haja ya sheria husika
kufanyiwa marekebisho kwa mashauriano na wadau mbalimbali kwa lengo la
kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa katiba mpya.
Kamati
Maalum ya CHADEMA ilikutana tena na Rais tarehe 21 Januari 2012 Ikulu
Dar es salaam ambapo kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe
ilitaarifiwa hatua ambayo ilifikiwa na serikali katika kuanza kuiboresha
sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ili ikidhi mahitaji ya
kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na mashauriano
na wadau mbalimbali.
Tarehe
22 Januari 2012 Kamati Kuu ilipokea na kujadili taarifa ya Kamati
Maalum kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na kujulishwa
hatua ambazo serikali ilifikia katika maandalizi ya kuifanyia
marekebisho tajwa katika Mkutano wa Sita wa Bunge unaotarajia kuanza
tarehe 31 Januari 2012.
Kamati
Kuu iliamua kwamba Kamati Maalum iendelee kufanya mawasiliano na
mashauriano na Rais Kikwete na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inafanyiwa marekebisho ya
msingi kabla ya mchakato wa kukusanya maoni kwa mujibu wa sheria husika
haujaanza.
Kamati
Maalum ilitakiwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio matatu ya
Kamati Kuu yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu
mchakato wa katiba mpya; maudhui ya maazimio hayo ni kama ifuatavyo:
Mosi;
“kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka
utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la
kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya,
Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha
wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki”.
Pili;
“Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya
uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa
Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sheria
hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo”.
Tatu;
“viongozi wote wa chama na wa kuchaguliwa katika ngazi zote kufanya
mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa
kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma
wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi”
Imetolewa tarehe 07 Aprili 2012 na: John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)