Uchaguzi wa wajumbe 9 wa Bunge la Afrika Mashariki Aprili - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Uchaguzi wa wajumbe 9 wa Bunge la Afrika Mashariki Aprili

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
____________

Katibu wa Bunge anatoa Taarifa kwa Umma kwamba, Uchaguzi wa wajumbe tisa (9) watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia tarehe 10 hadi 20 Aprili, 2012.

Uchaguzi huo wa Wabunge wa  Bunge la Afrika Mashariki unafanyika kwa kuzingatia kuwa maisha ya Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006, yatafikia ukomo wake  04 Juni, 2012.

Pamoja na Taarifa hii, Katibu wa Bunge ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo, atatoa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusika, kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni tarehe 10 Aprili, 2012, saa kumi (10.00) Jioni, na pia kuhusu siku ya uchaguzi ambayo ni tarehe 17 Aprili, 2012 saa tano (5.00) Asubuhi, mara au mapema baada ya Kipindi cha Maswali. 

Aidha, katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge pia atatoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na Wagombea wa Vyama vyote vya Siasa vyenye uwakilishi Bungeni kuhusiana na Uchaguzi huo, kwa ajili ya  kuviwezesha kuanza mchakato wa kuwapata Wagombea kupitia Vyama hivyo, ambao majina yao yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.

Kwa Taarifa hii, watu ambao wanazo sifa za kugombea na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wanaweza kuanza mchakato wa kuteuliwa kuwa wagombea wa uchaguzi huo, kupitia Vyama vyao vya Siasa.


Taarifa hii imetolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages