Kamanda wa Polisi Mkoa Wa Kagera Henry Salewi
Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Tulawaka unaomilikiwa na Barick Gold
................
WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wenye silaha wamemuua polisi
aliyekuwa akilinda mgodi wa dhahabu wa Tulawaka unaomilikiwa na
Kampuni ya Barrick wilayani Biharamulo Mkoani Kagera na kutoweka
na bunduki aina ya SMG yenye risasi 46 aliyokua akitumia polisi
huyo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na polisi, zimemtaja
polisi aliyeuwawa kuwa ni PC Dickson mwenye namba G2626 ambaye
aliyeuwawa Ijumaa Machi 23, 2012 akiwa katika lindo lake katika
ukuta wa mgodi huo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Salewi amethibitishia
FikraPevu kifo cha PC Dickson ambaye alikuwa lindoni na polisi
wenzake wanne waliopelekwa katika mgodi huo kukabiliana na
wahalifu wenye nia ya kuingia mgodini na kupora dhahabu na
kuongeza kwamba mwili wa marehemu uligunduliwa na wenzake baada ya
tukio hilo.
“Mwili wake uligundulika jioni na askali wenzake. Walikuta
amepigwa na chuma cha kuchimbia madini kilichomtoboa kichwa mara
nne,h awa walikuwa na nia ya kumuua na kuchukua bunduki,”alisema
Kamanda Salewi
Pia alisema bunduki iliyoporwa ni SMG iliyokuwa na risasi 46 na
kuwa polisi hao kila siku huenda kulinda ukuta wa mgodi huo
asubuhi na kurudi jioni mbapo maeneo ya mgodi huo yamezungukwa na
mapori makubwa ambayo hutumiwa na wahalifu.
Mwili wa polisi huyoi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 29
utasafirishwa leo kwenda nyumbani kwao wilaya ya Sumbawanga mkoani
Rukwa. Marehemu PC Dickson ameacha mke.
Kamanda Salewi amesema polisi wanaendelea na msako mkali wilayani
humo ili kuwabaini wahalifu hao.
Mauaji hayo yametokea katika wiki ile ile ambayo wachimbaji
wawili wa madini ya dhahabu wilayani Chato wakiuwawa kwa kuchomwa
moto na wachimbaji wenzao baada ya kuwatuhumu kujihusisha na
vitendo vya uhalifu.
Wachimbaji wadogo katika machimbo ya Mataba katika tukio la
Marchi 19, waliwateketeza kwa moto Jumanne William (35) na Juma
Magesse (40)kwa tuhuma za uhalifu.
Akifafanua tukio hilo Salewi alisema kuwa wachimbaji hao
walimkamata Jumanne baada ya kumuona amevaa koti alilodaiwa kupora
katika tukio la uhalifu la Februari mwaka huu ambapo baadhi ya
wachimbaji waliporwa madini.
Alisema baada ya kumshuku mtuhumiwa huyo walimkamata na kumhoji
na kukiri kuhusika na tukio hilo ambapo aliwapeleka kwa mtuhumiwa
mwingine Juma Magesse na baada ya kuwafikisha watuhumiwa wote
walipigwa na kuuwawa kisha kuchomwa moto.
Aidha Kamanda Salewi alisema watuhumiwa wanne wanashiliwa kwa
mahojiano ya tukio hilo, ambapo alikemea vitendo vya wananchi
kujichukulia sheria mikononi dhidi ya wahalifu na kuwataka
kuwafikisha wenye vyombo vya sheria.
Katika tukio jingine Kamanda Salewi alisema ya kuwa watu wawili
wilayani Karagwe wanashikiliwa baada ya kukamatwa wakiwa na silaha
aina ya bastola bila ya kuwa na kibali. Alisema watuhumiwa hao
walikamatwa Machi 14, 2012 wakishukiwa kwenda kufanya uhalifu
katika kituo cha mafuta.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Apoliti John (33) na Mushabe
Johnbosco wote wakazi wa kijiji cha Kibingo Wilayani humo ambao
walikamatwa baada ya polisi kusimamisha na kulipekua gari
walilokuwa wakisafiria.
Alisema hatua hiyo ilitokana na taarifa za raia wema ambapo
hakuna polisi wanaendelea na uchunguzi na taarifa za awali zinadai
kuwa walikuwa wanakwenda kupora katika kituo cha mafuta cha
Omugakorongo.
Habari imeandikwa na Phinias Bashaya-Kagera
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)