Nimelazimika
leo Jumamosi, tarehe 18 Februari, 2012 kutoa taarifa hii kwa vyombo
vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa
habari jana (17/02/12) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu
ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa “sikunyweshwa sumu” ila
naumwa tu ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo wa ngozi
umesababishwa na nini!
Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi
umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia
mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake
unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha
matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye
tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati
sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa
kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala
ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya
kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said
Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi
wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza
kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha
katika barua hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa
Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo
mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani
(ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni
kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au
tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika). Pamoja na
kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne
yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya
dhati ya kupeleleza suala hilo:
(i) Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya
“wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu
hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki
chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa
kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa
Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa
Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo,
nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa
watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima
lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
(ii) Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya
ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya
kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na
majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa
ujumbe tosha wa kunipuuza.
(iii) Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya
ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale
wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya
kuwahamishia mikoa mingine!
(iv) ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP
ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama
habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa
faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi
karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa
Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho
ikawa kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa
Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.
Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji
lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa
karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua
wenyewe. Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama
nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya
kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata
kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi?
Si ni polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru, wamekuwa wakikerwa na
tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili
lichunguzwe kwa kina?
Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma
taarifa halisi ya matatibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na
kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa
kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa
na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi
kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu
ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti /kukiondoa huku
vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa
kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!
Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye
IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa
wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua.
Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may
pale ambapo haki inakanyagwa.
Tuendelee kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile
tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans,
EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania. Dk. Harrison G. Mwakyembe (Mb), NW-UJDar es Salaam18/02/12
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)