John Mnyika
Taarifa kwa Umma kuhusu mgomo wa madaktari
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeguswa na mgomo
unaondelea nchini na kimesikitishwa na udhaifu wa serikali katika
kushughulikia kwa wakati madai ya madaktari nchini.
CHADEMA kinatambua kwamba uzembe na ufisadi katika serikali kwenye
sekta ya afya unaligharimu taifa na maisha ya wananchi. Hivyo, CHADEMA
inaitaka serikali kukamilisha kwa haraka majadiliano na madaktari na
kutimiza madai yao ili kuepusha madhara zaidi kwa umma.
CHADEMA inaitaka serikali irejee mapendekezo yaliyotolewa na chama
kupitia tamko la Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr Wilbroad Slaa kuhusu
mwelekeo wa taifa kwa mwaka 2012 kwamba Kipaumbele kikuu cha Kijamii
kiwe kushughulikia vyanzo vya migogoro katika maeneo mbalimbali badala
ya kukabiliana na matokeo.
Iwapo serikali ingezingatia msingi wa tamko hilo ambalo linapatikana kupitia www.chadema.or.tz;
mgogoro huu kuhusu madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya na
serikali usingefikia hatua ya kuleta madhara kwa wananchi.
Aidha, CHADEMA inawapa pole wananchi ambao wameathirika na migomo
inayoendelea na kuzingatia kwamba mgomo huo umesababishwa na udhaifu
katika serikali.
CHADEMA kimewasiliana na Waziri Kivuli wa Afya na Ustawi wa Jamii
Gervas Mbassa (Mb) ili kuungana pamoja na madaktari na wafanyakazi
wengine wa sekta ya afya katika kufuatilia madai yao.
Iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kutatoa mgogoro unaondolea
na kushughulikia madai ya wafanyakazi wa sekta ya afya, viongozi wakuu
wa CHADEMA watatoa tamko kuhusu hatua za ziada ambazo chama kitachukua
ili kuhakikisha kwamba umma hauendelei kupata madhara ya udhaifu wa
serikali.
CHADEMA kinatoa mwito kwa umma wa watanzania kuwaunga mkono madaktari
na watumishi wengine wa sekta ya afya katika hospitali na zahanati za
umma kama sehemu ya kuboresha huduma katika maeneo husika.
Madai ya madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini
yasiposhughulikiwa kwa wakati na kwa ukamilifu watumishi husika
wanaweza wasiwe kwenye mgomo wa wazi kama ilivyo kwa baadhi ya
hospitali na zahanati nchini lakini wataendelea na migomo baridi kwa
kutoa huduma mbovu au kuacha kazi kwenye maeneo ya umma na wengine
kwenda kufanya kazi nje ya nchi wakati kukiwa na uhaba wa watumishi
nchini.
Aidha, pamoja na migomo inayoendelea CHADEMA kinatoa rai kwa
madaktari na watumishi wengine wa umma kuhakikisha maisha ya wagonjwa
walio katika hali ya hatari yanaokolewa.
CHADEMA kinatoa mwito kwa wadau wote kuunganisha nguvu katika
kuisimamia serikali kushughulikia madai ya madaktari na wafanyakazi
wengine wa sekta ya afya kwa haraka ili kuepusha madhara zaidi kwa
umma.
CHADEMA kingependa umma uzingatie kwamba tangu Mwalimu Nyerere
aondoke madarakani mwaka 1985, Serikali ya CCM imeongeza wingi wa
majengo mbalimbali kwenye sekta ya afya hata hivyo imeshindwa kusimamia
utoaji bora wa huduma za afya katika zahanati, hospitali na vituo vya
afya. Kutokana na mfumo mbaya wa usimamizi wa sekta ya afya, misingi
imara ya kuimarisha sekta ya afya iliyowekwa baada ya uhuru imevunjwa
na kubomolewa ikiwemo katika masuala yanayohusu kujali maslahi ya
watumishi wa umma katika sekta hii muhimu.
Hali hii imefanya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa na nakisi ya
watumishi asilimia 48% na takwimu zinaonesha kuwa 18% ya wafamasia,
15% ya madaktari, 13% ya madaktari wasaidizi waliacha vituo vyao vya
kazi na kwenda kutafuta kazi kwenye mashirika ambayo yanalipa mishahara
mikubwa na mizuri. Nakisi hii itaongezeka zaidi iwapo madai ya msingi
ya madaktari na watumishi wengine hayatashughulikiwa na serikali
itaendelea kuchelewa kushughulikia migogoro na migomo mingine
inayoendelea.
Serikali ya CCM irejee ilani ya CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2010 kifungu cha 3.3 ambapo chama kimeeleza bayana namna ambavyo
serikali inaweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa sekta ya afya ili
kuweza kuwavutia wataalamu kubakia nchini badala ya kwenda kugoma au
kwenda kutafuta kazi nje ya nchi kutokana na malipo mazuri huko.
Aidha, katika ilani hiyo CHADEMA imeeleza bayana kwamba ipo haja ya
malipo ya mazingira magumu kutolewa kwa watumishi wa afya wanaofanya
kazi katika maeneo na kada maalum.
Imetolewa tarehe 25 Januari 2012 kwa niaba ya CHADEMA na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)