JK abariki posho mpya za wabunge - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

JK abariki posho mpya za wabunge

Rais Jakaya Mrisho Kikwete
KILA MMOJA KULIPWA 330,000 KWA SIKU, ZITTO, MAKAMBA, KIGWANGALA WASULUBISHWA KWA KUZIPINGA
Waandishi Wetu, Dodoma  
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema tayari Rais Jakaya Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku.  Kupitishwa kwa posho hizo ambazo ziliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili, kunafanya sasa mbunge kupokea Sh330,000 kwa siku; Sh200,000 zikiwa ni posho ya kikao, Sh80,000 posho ya kujikimu na Sh50,000 nauli.  

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha utanguzi cha wabunge jana, zilidai kuwa baada ya Pinda kutoa taarifa hiyo, wabunge walishangilia huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akisimama na kudai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa hajasaini kuidhinisha posho hizo.  

Hatua hiyo ilisababisha Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Juma Nkamia (CCM), kusimama na kuhoji iwapo Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya Pinda kusimama na kuthibitisha kusainiwa kwa posho hizo akisema siyo ajabu kwani hata watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh150,000 na Sh200,000.  Hata hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia baada ya kusainiwa kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya kazi za ubunge.  

Katika kikao hicho baadhi ya wabunge wanadaiwa kuwashambulia Zitto, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis Kigwangwala kwamba wamekuwa mstari wa mbele kupinga posho hizo hadharani.  Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye anadaiwa kwamba aliungana na Pinda kuthibitisha kwamba Rais Kikwete ameidhinisha posho hizo mpya, pia aliwashambulia wabunge wanaozipinga akisema kwamba wanafuta umaarufu wa kisiasa.

“Wanachotafuta ni umaarufu wa kisiasa tu, mimi ninavyojua umaarufu wa kisiasa unakuja kwa kufanya kazi za kibunge za wananchi lakini siyo kupinga posho,” chanzo chetu cha habari kilimnukuu Makinda.

Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa anadaiwa kwamba alitumia mafumbo  kuwashambulia wabunge hao ambao wamejitokeza kupinga nyongeza hiyo ya posho.  Kauli hiyo inadaiwa kuungwa mkono na Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba ambaye alidai kuwa hawezi kumsemea Zitto kwa sababu ni kawaida yake kupinga, lakini akaelekeza shutuma zake kwa Makamba kwamba ameanza kupinga baada ya kugharamiwa na CCM. “Januari anapinga posho hizo kutokana na CCM kumpa gari, nyumba na analipwa na chama,” kilisema chanzo chetu kikimkariri Nkumba.

 Pia, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), anadaiwa kumshambulia Zitto kuwa lazima apinge posho hizo kwa sababu, anapewa fedha na wafadhili kutoka nchi za nje.  “Shelukindo anasema amefanya ziara nje na kuhakikisha kuna wahisani wanamfadhili Zitto kwa hiyo ana haki ya kupinga posho hizo,” chanzo chetu hicho kilimkariri Shelukindo.
 
Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya mashambulizi hayo, Dk Kigwangwala alisimama kutetea msimamo wake kwamba ongezeko hilo halina ‘mashiko’ na haliwezi kuelezwa mbele ya umma likaeleweka, lakini alizomewa na wabunge wengi huku wakimtaka kukaa chini.  

Hatua hiyo ilisababisha Zitto kusimama na kueleza kuwa tatizo la wabunge kwamba wana fikra finyu, kauli ambayo alitakiwa na wenzake kuwaomba radhi kuwa amewatukana.  “Zitto ametumia Kiingereza kuwa tatizo la wabunge ‘we think small’,  Shelukindo na (John) Komba wakaja juu wakitaka kuwaomba radhi kwa kuwatukana,” chanzo chetu kilieleza.  Zitto anadaiwa kusema wabunge walitakiwa kujenga hoja ya kuongeza fedha za mafuta ya gari wanayolipwa hivi sasa Sh2.5 milioni kwa mwezi, kutokana na kupanda kwa nishati hiyo, lakini siyo posho.  

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alinukuliwa akisema matatizo ya posho yamefikia hapo baada ya kuonekana ni ya watu binafsi siyo mfumo hivyo, wanaopinga wanaonekana kama wanatafuta umaarufu na wana vipato vya fedha, akaitaka kamati ya uongozi ijadili na kupata mwafaka badala ya wajumbe kutofautiana mbele ya umma.  Wabunge wengine wanaodaiwa kutetea posho hizo ni Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Jenister Mhagama (Peramiho CCM).

 Msimamo wa January
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Makamba alijibu: “Si sahihi kwangu kutoa taarifa za kikao cha ndani. Lakini msimamo wangu kwenye suala hilo unajulikana na haujabadilika.  Msimamo wa CCM ulishawekwa wazi na sote tunaujua. Nitalizungumzia suala hili kwa kirefu katika siku zijazo.”

Kuhusu taarifa kwamba anagharamiwa na CCM, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka kiulizwe chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu taratibu za kuwagharamia viongozi wa chama chake ambao ni wabunge alisema: “Mbunge au kiongozi yeyote wa chama mwenye nafasi nyingine anagharamiwa na chama pale anapokwenda kufanya shughuli za chama tu na si vinginevyo.”

“Kwa hiyo kama ni mbunge suala la mafuta, dereva, mahali pa kulala na mahitaji mengine anagharamiwa na taasisi anayoifanyia kazi na siyo chama.”

“Kwa mfano, mimi kwenye sekretarieti hata posho za vikao huwa sichukui, nadhani na mwenzangu January naye sidhani kama huwa anachukua posho, kwa sababu tukifanya hivyo ni kama tunakiumiza chama, huo ndiyo msimamo wetu na uko wazi wala siyo kificho.”

Kwa upande wake, Zitto alisema jana kwamba hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo na badala yake kuahidi kwamba atalizungumza leo atakapokutana na waandishi wa habari.

Wabunge walia njaa
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilisema wabunge hao walilalamikia kucheleweshwa kulipwa posho zao za wiki mbili walizokaa Dar es Salaam wakati wa vikao vya kamati.

Walidai hivi sasa wanaishi kwa shida huku wakihoji sababu za kucheleweshewa.

Imeelezwa kwamba Spika Makinda alidai kuwa fedha hizo zipo na kwamba  kilichochelewesha ni uhakiki wa wabunge waliohudhuria vikao.

Makinda alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipwa posho za vikao bila kuhudhuria, hatua ambayo imesababisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuhoji maswali mengi.

CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages