Rais Jakaya
Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkurugenzi Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana, kufiatia kifo cha
mtangazaji maarufu wa siku nyingi wa shirika hilo, Halima Mohammed
Mchuka ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia leo, Alhamisi, Desemba
29, 2011 kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
“Nimepokea
kwa huzuni habari za kifo cha Halima Mohammed Mchuka. Nakutumia wewe
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) salamu za dhati
ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki. Nakuomba, kupitia kwako,
uniwasilishie salamu zangu kwa wafanyakazi wenzake katika TBC ambao
wamempoteza mwenzao na rafiki yao.” Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema ikimkariri Rais.
“Aidha,
nataka kupitia kwako niwatumie salamu zangu za rambirambi
wana-familia, ndugu na jamaa wote za marehemu. Wajulishe kuwa niko nao
katika wakati huu wa maombolezo na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia.
Nawaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu
yote ni mapenzi ya Mungu. Naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi
wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amen.” amesema Rais.
Rais amesema kuwa Mchuka ametoa mchango mkubwa katika nyanja ya utangazaji nchini. “Sote
tutaendelea kukumbuka weledi wake, uzalendo wake na ujasiri wake
katika utangazaji uliomsukuma kuwa Mwanamke wa Kwanza katika Tanzania
kutangaza mechi za mpira wa miguu”.
Amesema
ni dhahiri kuwa nyanja ya utangazaji imeondokewa na mtu muhimu na
namna nzuri zaidi ya kumuenzi Mchuka ni kwa watangazaji waliobakia
kuendelea kuiga mfano wake katika ubora wa utangazaji nchini mwetu.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)