Waziri wa Uchukuzi Mh. Omar Nundu akipiga
kengele kama ishara ya kuorodheshwa rasmi kwa shirika la ndege la Precision Air
katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi wa
Precision Air Bw. Michael Shirima na mwakilishi wa mamlaka ya hisa nchini
Tanzania Bw. Godfrey Malekano.
Dar es Salaam Desemba 21 2011. Precision Air PLC leo
imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya hitimisho ya Uuzaji
wa Hisa katika soko la Awali. Uorodheshwaji huo uliendana na
sherehe maalum uliohudhuriwa na mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Omar
Nundu katika ukumbi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, pamoja na muasisi wa
shirika hilo la ndege Bw. Michael Shirima, Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Hisa la
Dar es Salaam Bw. Gabriel Kitua na mwakilishi wa Mamlaka ya Hisa Tanzania Bw.
Godfrey Malekano.
Akizungumza wakati wa uorodheshwaji
huo Waziri wa Uchukuzi Mh. Omar Nundu ameipongeza shirika la ndege la Precision
Air kwa kuweza kuwa kinara wa usafiri wa anga nchini hadi kuweza kufikia hatua
ya kuuza hisa zake pamoja na kujiorodhesha katika soko hilo la Dar es Salaam. “Nawapongeza sana Precision Air, na
napenda kuchukua fursa hii kutoa ahadi kama serikali kwamba tutajitahidi
kuboresha sera na miundombinu yetu ili kuweza kuinua ushindani pamoja na
kuwasaidia mashirika kama yenu kuweza kufanya biashara katika mazingira bora
zaidi,” alisema Waziri Nundu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Precision
Air Bw. Shirima alisema, “Kwanza kabisa, nawashukuru Mamlaka ya Hisa nchini
Tanzania na Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kutuongoza na kutulea kwa moyo wa
dhati kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato huu. Tunaazimia kuendelea
kushirikiana pamoja nanyi ili kuweza kutimiza lengo letu la pamoja la kuongeza
thamani ya mwenye hisa katika kampuni; hasa hasa kwa wanahisa watarajiwa.”Bw. Shirima pia aliwashukuru na
kuwapongeza wanahisa wapya wa Precision Air; “Awali juu ya yote kuna wale
washirika ambao pamoja na kwamba ni wawekezaji wapya, kuanzia leo katika tukio
hili watakuwa wanahisa wa shirika hili la ndege. Napenda kusema ahsante na
hongereni sana kwa ujasiri na sifa
mlioweza kupatia shirika hili.”
Kwa upande wake naye Mkurugenzi Mkuu
wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Gabriel Kitua alisema kwamba Precision Air
ni shirika la 18 kuorodheshwa katika soko hilo, inayofanya Soko la Hisa la Dar
es Salaam kushika nambari mbili kwa upande wa Afrika mashariki. Jumla ya wawekezaji 7,056 (Elfu saba na hamsini na sita)
walishiriki katika Uuzwaji wa Hisa katika Soko la la Awali (IPO) iliyoanza
tarehe 7 Oktoba na kumalizika Novemba 4 2011. Shirika limekusanya jumla ya shilingi
za kitanzania bilioni 12 ambazo ni asilimia 43.18 ya kiasi kilichoombwa. Kwa
kiasi kikubwa walioomba kununua hisa walikuwa wawekezaji wadogo wa ndani pamoja na Mashirika ya Kitanzania kama
ilivyokusudiwa.
Shirika pia hapo nyuma liliwasilisha
kwa Mamlaka husika mpango wa kifedha kuonyesha jinsi fedha zilizokusanywa
zitakavyotumika na mikakati ya kujaza pengo kuhakikisha malengo ya shirika
yanafanikiwa kwa ufanisi mkubwa. Pamoja na ukusanyaji fedha kuwezesha
upanuzi, shirika pia lilikusudia kuongeza umiliki wa umma hasa wananchi wa
Tanzania. “Tunawashukuru wote walioshiriki kama
ilivyothibitishwa na wingi wa ushiriki wao na tunafurahi kuwa zoezi la uuzaji
wa hisa za shirika umefanikisha malengo yote mawili ya ukusanyaji wa mtaji na
kuongeza wigo wa umiliki wa shirika kwa
Watanzania,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Precision Air Bw. Alfonse Kioko.
“Ushiriki mkubwa wa Watanzania ni
ushahidi wa kutosha kuwa wananchi wanaimani na matumaini kwa shirika lao la
ndege. Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia kuwa uwekezaji wao utakuwa wa ufanisi,” Bw. Kioko
aliongeza. “Mpango wa kuongeza
vituo vya usafiri na mtandao
ulioko utaendelea. Pia shirika limeanzisha mpango kabambe wa kuimarisha huduma
zake kwa wateja,” Kioko alisema.
Mwisho.
Imetolewa na Ofisi ya Mawasiliano
Nambari: 0786404010/0712223839
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)