TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati
ya Utendaji ya Taifa ya Chama Cha Wananchi (CUF) imefanya kikao chake
cha kawaida cha siku mbili mjini Zanzibar tarehe 30 – 31 Desemba, 2011
chini ya Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad.
Pamoja
na kujadili ajenda kadhaa za kawaida kuhusiana na mambo ya utendaji
katika Chama, Kamati ya Utendaji ya Taifa pia ilipata nafasi ya kupokea
taarifa ya kina kuhusu hali ya kisiasa ndani ya Chama kutoka kwenye
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama kupitia Kamati yake Ndogo ya
Nidhamu na Maadili. Taarifa hiyo ilijikita zaidi katika njama
zinazoendeshwa na wanachama 14 wakiongozwa na Mheshimiwa Hamad Rashid
Mohamed zenye mwelekeo wa kutaka kukivuruga Chama.
Kamati
ya Utendaji ya Taifa imeridhika kwamba kuna hoja za msingi na ushahidi
wa kutosha dhidi ya wanachama hao 14 unaoonesha kuhusika kwao na njama
hizo. Wanachama hao ni:
1. Hamad Rashid Mohamed2. Doyo Hassan Doyo
3. Shoka Khamis Juma
4. Juma Said Saanani
5. Yasin Mrotwa
6. Mohamed Albadawi
7. Mohamed Masaga
8. Doni Waziri
9. Yusuf Mungiro
10. Nanjase
11. Ahmed Issa
12. Tamim Omar
13. Amir Kirungi
14. Ayubu Kimangale
Kwa
mujibu wa Katiba ya Chama, kifungu cha 63 kinachozungumzia Wajibu wa
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kifungu cha 63 (1) (d) kinafafanua
wajibu huo kuwa ni “kulinda na kuendeleza heshima ya Chama na Serikali
zote halali za nchi.” Kifungu cha 63 (1) (j) kinaelezea wajibu mwengine
kuwa ni “kuwachukulia hatua za nidhamu viongozi na wanachama
wanaoshutumiwa kwa makosa mbali mbali kwa kufuata masharti ya Katiba hii
na kanuni zitakazotungwa mara kwa mara kwa mujibu wa katiba hii.”
Kwa
kuzingatia hali hiyo, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeridhika kwamba
kuna haja ya kutumia uwezo iliopewa chini ya kifungu cha 62 (1) cha
Katiba ya Chama kuitisha kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa la Chama ili kutafakari hali hiyo, kusikiliza tuhuma
zinazowakabili wanachama hao, kuwapa nafasi ya kuwasiliza na kujitetea
na kisha kuchukua hatua kama litakavyoona inafaa.
Kikao hicho cha Baraza kuu la Uongozi la Taifa kitafanyika Zanzibar, tarehe 04/01/2012 katika ukumbi wa hoteli ya Mazson.
Kamati
ya Utendaji ya Taifa inawaomba wanachama na wapenzi wote wa CUF
kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki na kutoa nafasi kwa vikao
vya Chama kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya Chama.
HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa na;
JULIUS MTATIRO,
NAIBU KATIBU MKUU (TANZANIA BARA),
KATIBU WA KAMATI YA UTENDAJI TA TAIFA (CUF NATIONAL CENTRAL COMMITTEE).
31 Disemba 2011,
ZANZIBAR.






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)