Rais msaafu Ali Hassan Mwinyi
(aliyevaa suti ya kijivu) akipewa maelezo mafupi na Ofisa Uhusiano wa
Benki ya Posta Tanzania (TPB), Noves Mosses (wa kwanza kulia)
alipotembelea banda la benki hiyo leo katika Viwanja vya Mwalimu Julius
Nyerere-Sabasaba leo. Kutoka kushoto ni Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha,
Bi. Ingiahedi Mduma akifuatiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ramadhano
Khijjah.
Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi
(kulia) akipata maelezo kutoka kwa wafanyakazi wa Benki ya Posta nchini
(waliovaa flana za kijani kulia) alipotembelea banda hilo leo.
BENKI
ya Posta Tanzania (TPB) mwakani imejipanga kuhakikisha inaweka
utaratibu mzuri utakaowawezesha wananchi vijijini hasa wakulima kuweza
kutumia huduma za kibenki maeneo ya vijijini.
Akizungumza
na Thehabari.com leo jijini Dar es Salaam kuelezea mafanikio ya TPB ya
miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, katika maonesho ya maadhimisho ya
sherehe hizo, Ofisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Bi. Noves Moses amesema lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha huduma zao zinamfikia Mtanzania wa kawaida vijijini.
Alisema
kwa sasa Benki ya Posta inatoa huduma za kibenki katika wilaya zote
nchini ambayo imeweza kuwanufaisha baadhi ya wananchi wa kawaida
wakiwemo wakulima vijijini.
“Benki
ya Posta kwa sasa tuna matawi 28 nchi nzima, hii ni kwa maana ya mikoa
yote...na pia tunatoa huduma zetu za kibenki kwa mawakala 151 wa Shirika
la Posta na Simu nchini, hivyo huduma zetu kwa kiasi kikubwa
zinawanufaisha hata wakulima wa vijijini tofauti na benki nyingine
zinazoishia mijini,” alisema Bi. Moses.
Aidha
akizungumzia mafanikio ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, alisema
TPB imepiga hatua kubwa kwa sasa kwa kipindi hicho hasa katika
kuongezeka kwa mtandao wa utoaji huduma kutoka tawi moja hadi kufikia
matawi 28. alisema maeneo mengine ni pamoja na kuifanya benki hiyo kutoa
huduma za kisasa zinazoenda na wakati.
“Awali
TPB wateja walikuwa wanatumia vitabu vidogo, ambapo kila mteja alikuwa
akipewa huduma na kumbukumbu zake kuhifadhiwa kwenye kitabu chake na
benki…sasa hivi hatutumii tena vitabu mteja anatumia kadi ambayo pia
imeunganisha katika mitandao mingine ya benki (Umoja Switch) hivyo
kumuwezesha mteja wetu kupata huduma za ATM katika wigo mpana,” alisema
Ofisa Habari huyo.
Pamoja
na huduma hizo, pia ameongeza kuwa TPB inatoa huduma za haraka kwa
wateja wake na nafuu ukilinganisha na benki nyingine nchini hivyo
kuwataka Watanzania kujitokeza na kujiunga na benki hiyo ya Kizalendo
ambayo inamilikiwa kwa asilimia kubwa na Serikali yenyewe.
“Watanzania wana kila sababu ya kutuunga mkono maana hii ni benki yao,
inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 75. Lengo letu ni kuhakikisha
tunamfikia Mtanzania wa kawaida kijijini, tumeanza na TPB Popote yaani
huduma inayotoa huduma zote za kibenki kwa wateja wetu kupitia simu ya
mkononi,” alifafanua Bi. Moses.
Mwisho.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)