Mhe.Naibu Katibu Mkuu Asha-Rose Migiro
akibadilishana mawazo na Waheshimiwa Wabunge John M. Cheyo na Betty
Machunge wakati alipowakaribisha Ofisini kwake Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa.Wabunge hao wapo hapa wakihudhuria mkutano wa wabunge ambao
Naibu Katibu Mkuu aliufungua. Wabunge hao wanaliwakilisha Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo.

Mhe. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Asha-Rose Migiro akifungua mkutano wa siku mbili wa wabunge kutoka
mabunge mbalimbali duniani mkutano huo unafanyika kwenye makao makuu ya
Umoja wa Mataifa New York, kushoto kwake ni Rais wa Baraza Kuu la 66 la
Umoja wa Mataifa, Bw. Nassir Abdulazizi Al-Nasser na kulia ni Katibu
Mkuu wa IPU Bw. Anders B. Johson.
Na Mwandishi Maalum- New York
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Asha-Rose Migiro amewahimiza wabunge kuweka mbele maslahi ya wananchi
wanaowawakilisha.
Ameyasema hayo jana Jumatatu, wakati alipokuwa
akifungua mkutano wa siku mbili unaowakutanisha wabunge kutoka mabunge
mbalimbali duniani, ufunguzi uliomshirikisha pia Rais wa Baraza Kuu la
66 la Umoja wa Mataifa, Nassir Abdulaziz Al-Nasser.
Katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Umoja
wa Mataifa na Muungano wa Mabunge ( IPU),Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania linawakilishwa na wabunge wawili, Mhe.John M.Cheyo na
Mhe.Betty Machangu.
“ Mkiwa ni wabunge kazi yenu si kupitisha
sheria tu na kusimamia utendaji wa serikali. Bali mnatakiwa kuwajibika
kisiasa kwa kuwasikiliza wananchi na kuelezea matakwa yao”,Akasisitiza
Migiro.
Naibu Katibu Mkuu amewaambia wabunge
hao,wakiwamo pia baadhi ya maspika,kwamba,uwajibikaji wa kisiasa na
utawala wa kidemokrasia haviwezi kutengenishwa kwa kuwa vyote ni muhimu
katika kuchagiza maendeleo ya binadamu, haki na amani.
“ uwajibikaji wa kisiasa ni muhimu sana katika
kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa. Baadhi ya
Changamato hizo ni pamoja na umaskini, vurugu, na uhalifu wa kupangwa
mambo ambayo yanashamiri katika nchi ambazo hakuna
uwajibikaji”akabainisha Migiro.
Akasema kuwa taarifa ya Bank ya Dunia
imeonesha kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, makosa ya jinai, vurugu na
hata ugaidi na uhalifu wa kupangwa ni mambo yanayoota mizizi na kukua
katika nchi ambazo ama utawala wa sheria ni dhaifu au taasisi zake
zimeghubikwa na ufisadi.
Hata hivyo Migiro amewaeleza wabunge hao
kwamba hakuhitajiki utafiti kama huo ulioofanywa na Bank ya
Dunia,kufahamu kwamba kuongezeka kwa vitendo vya halifu kunasababishwa
na serikali kandamizi.
Akatoa mfano kwa kutaja vunguvungu la kisiasa
linaloendelea hivi sasa Mashariki ya Kati maarufu kama Arab Spring,
ambako anasema vuguvugu hilo limeamsha hamasa hususani kwa vijana,
hamasa ya kutaka kuwepo na serikali za kidemokrasia, zinazowajibika na
zenye kuheshimu misingi ya haki za binadamu.
Akasema anafahamu vema changamoto
wanazokabiliana nazo wabunge kwa sababu hata yeye aliwahi kuwa mbunge.
Hata hivyo akasema yapo mambo kadhaa ambayo
wabunge kwa kushirikiana na serikali zao yanaweza saidia kuzuia au
kupunguza mitafaruku ya kisiasa na vitendo vya uhalifu.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kujenga
mazoea ya uwajibikaji, kufanya uchanguzi wa mara kwa mara na
unaozingatia utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa
kukusanyika na kutoa mawazo na kuongeza idadi ya wanawake mabungeni.
“ Lakini uwajibikaji unakwenda mbali zaidi ya
hapo” anasema Migiro. “ Ni kwa kuhakikisha ushiriki wa wananchi na hasa
vijana katika mambo ya siku hadi siku, kwa kutimiza hayo na mambo
mengine wabunge mnaweza kujenga daraja imara kati ya wananchi na
serikali zao” akasisitiza Migiro.
Aidha Migiro ameyataka mabunge yote duniani
yawajibike katika kuzuia vitendo vya rushwa.
Ajenda muhimu zinazojadiliwa na wabunge hao
katika mkutano huo wa siku mbili ni pamoja na, uhusiano kati ya Umoja wa
Mataifa na Mabunge , nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kusimamia na
kuimarisha dhana ya uwajibikaji, na fursa na changamoto zinazowakabili
vijana katika ushiriki wao katika demokrasia.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)