Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
WIZARA
ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) wamewekeana saini ya mkataba na makampuni ya Ndovu resource na
Heritage Oil kutoka nchini Uingereza kwa ajili ya uchimbaji na
utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi katika Kisiwa cha Songosongo na
Ziwa Rukwa.
Akizungumza
katika hafla hiyo jana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
alisema uwekaji saini wa mikataba na makampuni hayo unaifanya Tanzania
kuwa na mikataba 23 na makampuni 17 ya utafutaji wa nishati ya mafuta
na gesi yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Alizitaja
nchi zenye makampuni hayo ni Australia, Uingereza, Ufaransa, Brazil,
Norway, Marekani, Canada na Nchi za Falme ya Kiarabu.
Waziri
Ngeleja alisema utiaji saini na makampuni hayo ni kielelezo cha sera
nzuri zilizopo katika sekta ya nishati na hivyo kuifanya Tanzania
kuendelea kuwa kivutio cha uwekezaji kwa kampuni mbalimbali za ndani na
nje ya nchi.
“Mikataba
hii imezingatia maslahi ya taifa pamoja na makampuni haya kufuata
sheria za nchi yetu ikiwemo suala zima la uhifadhi wa mazingira ambalo
ni jambo la msingi kwa wananchi wetu” alisema Ngeleja.
Aidha
Waziri Ngeleja aliitaka TODC kusimamia vyema masharti ya mikataba hiyo
ikiwemo fedha zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo ya watumishi wa
shirika hilo yanayolenga kuliwezesha taifa kupata wataalamu wake
wataosimamia vyema rasilimali za mafuta na gesi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TPDC, Yona Killagane alisema ujio wa makampuni hayo ni
fursa nzuri iliyopata Tanzania katika kufumbua vyanzo mbalimbali vya
nishati ya mafuta na gesi vilivyopo nchini.
“Kabla
ya kufikia hatua hii ya utiaji saini, tulichukua hatua za makusudi ili
kujiridhisha kuwa mikataba hii itazingatia maslahi ya taifa” alisema
Killagane.
Naye
Kamishina Msaidizi wa maendeleo ya gesi na petrol katika Wizara ya
Nishati na Madini, Prosper Victus alisema mikataba hiyo itagharimu kiasi
cha Dola Milioni 70 na shughuli hiyo ya utafutaji wa nishati hizo za
inatarajia kuchukua kipindi cha miaka 11 iliyogawanywa katika awamu 3 za
utekelezaji.
Alisema
kampuni ya Ndovu Resource itachimba nishati hiyo ya mafuta na gesi
katika eneo la songosongo mashariki wakati kampuni ya Heritage Oil
itafanya shughuli hiyo katika ziwa Rukwa.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Ndovu Resource, Brian Hall alisema kampuni yake
itaheshimu vipengele vya mkataba huo ikiwemo suala la uchangiaji wa
huduma za kijamii kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji wa
nishati hizo.
Kwa
upande wake, Makamu wa Rais wa Kampuni ya heritage Oil, Brian Smith
alisema kampuni yake itahakikisha suala la ajira kwa vijana linapewa
kipaumbele, kwani nia ya taasisi hiyo ni kuungana na Serikali katika
mapambano dhidi ya umaskini kwa wananchi wake.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)