Na Nova Kambota Mwanaharakati,
Mara kwa mara
huwa nasema tatizo kubwa la Tanzania yetu ni kupenda kupindisha ukweli, hii
imetufanya kuwa watu tusiopenda kufikiri kiasi kwamba tunalambishwa kila
linalokuja “tumekuwa madodoki kila uchafu tunasomba”. Naandika hivi kwa nia ya
kujenga si kubomoa, naandika hivi kwa mustakabali wa Demokrasia yetu ambayo
nathubutu kusema imetikiswa kupita maelezo huko Igunga na tusipokuwa makini
Taifa litadondoka siku za usoni.
Kwako Dr Kafumu ambaye umetangazwa kuwa mbunge wa Igunga
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), naomba unaposhangilia ushindi wako nikiamini
wewe ni msomi na mzoefu katika Nyanja za uongozi wa Taifa hili napenda usome
maandishi yaliyo ukutani kisha malizia kwa kuunganisha dots za ushindi wako
halafu niambie ikiwa ni kweli unaamini kuwa umeshinda kihalali? Au la niambie
kile ambacho kinaitwa “changamoto za uchaguzi Igunga” ni nini kama siyo
“mizengwe?”
Kama mchambuzi nisiyeegemea upande wowote nisingependa kutia
mwaa mtiririko huu wa hoja zangu kwa hiyo sitaegemea upande wowote bali
nitajadili kwa misingi ya hoja ili ikibidi kujibiwa pia nijibiwe kwa misingi ya
hoja vivyo hivyo, nataka kuibua hoja zenye mashiko ili zitufikirishe na kutupa
majibu ya kisayansi badala ya kumezwa na mawimbi ya watu wenye mkatiko wa
mirija ya fikra ambao wamebaki na ushabiki badala ya hoja kiasi kwamba wanatoa
majibu ya zamani kwa maswali mapya. Yafuatayo ni mambo manne ambayo yanatia doa
ushindi wa Dr Kafumu;
Kwanza Tume Ya
Uchaguzi;
Tume ya uchaguzi
ya nchi hii haina sifa nzuri na haiwezi kuwa na sifa nzuri mpaka iwe huru, hata
I gunga hali ni hivyohivyo tumesikia malalamiko dhidi ya tume hiyo lakini hasa
kwa aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni mteule wa rais na
bila shaka kwa kuunganisha mantiki haina shaka kuwa naye ni mwanachama wa CCM
au basi anaipenda kimoyomoyo. Uchaguzi wa Igunga ukipimwa kwa mizania hii ya
aina ya tume ya uchaguzi tuliyonayo ni vigumu sana kwa mtu mwenye kufikiri kwa
mantiki kuridhia matokeo ya uchaguzi huo.
Pili Siasa Uchwara;
Hapa inahitaji
moyo mgumu kuyasema lakini kwa vile tangu awali nilishasema kuwa lengo si
kufukua makaburi bali kuweka shada la maua juu ya makaburi basi acha niseme
hiki ambacho nakiita ni siasa uchwara. Kwanza kabisa jinsi serikali ya CCM
ilivyoruhusu kubofywa kwa kile kinachoitwa “kitufe cha udini”, ikumbukwe kuwa
hata wakati wa uchaguzi serikali bado ina jukumu la kuilinda katiba na
kuhakikisha amani haivurugwi aidha kupitia mirija ya udini wala ukabila,
nayasema haya kutokana na baadhi ya viongozi wa dini kuirushia makombora
CHADEMA tena wakaenda mbali kwa kutoa wito kwa baadhi ya waumini wa dini Fulani
kutompigia kura mgombea wa chamna hiko, lakini cha ajabu hata hiyo hoja ya DC
kuvuliwa hijabu imekwama kama gazeti nguli la Mwanahalisi lilivyofunua kuwa
Mama Fatuma Kimario uislamu wake una mashaka kutokana na yeye kuwa ni mke
halali wa Bw Kimario ambaye ni mkristu wa madhehebu ya Kikatoliki ambapo hata
mwanazuoni mashuhuri wa kiislamu nchini Sheikh
Issa Ponda amenukuliwa akisema kuhusu mwanamke au mwanaume wa kiislamu
kubadili dini Sheikh Ponda amesema “Hilo ni kosa kubwa sana”. Lakini cha kusikitisha kuwa wakati haya yote
yanatokea CCM walikaa kimya kana kwamba “hawakuliona kosa”, je tukisema kuwa
hii ilichangia Wana Igunga kupiga “kura za chuki” dhidi ya CHADEMA tutakuwa
tumekosea? Haya ni maswali magumu kuhusu ushindi wa Dr Kafumu.
Jambo la pili ambalo linaangukia kwenye siasa uchwara ni
pamoja na vitimbi vya rushwa na vitisho vya “kipuuzi” mfano gazeti la Dira
linamtaja mwenyekiti wa mtaa wa Nkokoto huko Igunga Bw Abed Motomoto (CCM) kuwa
amekutwa akigawa rushwa “live”kwa wanawake wa mtaa wake kwa lengo la
kuwashawishi kumpigia kura mgombea wa CCM (Dr Kafumu), lakini kama hili
halitoshi kuna hili la Mh Ismail Aden Rage kupanda na bastola ikining’inia
kiunoni halafu tunaambiwa kapewa adhabu ya kulipa laki moja, sasa ladda nitumie
fursa hii kumuuliza ndugu yangu Aden Rage kuwa alikuwa anamtisha nani na
bastola yake? Au nani kamwambia kuwa ni utamaduni wa kitanzania kuonyeshana
vyombo vya moto? Haya ni machache kati ya mengi yanayokinzana na maana ya
demokrasia pia kupoteza mantiki nzima ya “uchaguzi huru na wa haki”
Tatu kuchelewesha
matokeo;
Hili ni tatizo
linalotia huzuni sana kiasi kwamba nashawishika kuamini kuwa “bado tuna safari
ndefu”, nayasema haya kwasababu kwanza idadi ya watu waliojiandikisha ni
tofauti sana kwasababu waliopiga kura ni wachache wanaokadiriwa kuwa elfu
sitini (60,000) lakini cha ajabu hata kiasi hiki kichache cha kura kimechukua
masaa kibao zaidi ya kumi kuhesabu, hiki kama si kiroja ni nini? Au tuamini
kuwa kuna lililojificha nyyuma ya pazia hapa?
Nne Matumizi Ya
Nguvu;
Nalazimika kuyaandika haya kutokana na tabia inayozidi kukua
siku hizi ya polisi kutumia nguvu dhidi ya wananchi , matukio ni mengi lakini
hebu tutupie macho kwenye hili sakata la Igunga ambapo nasema kulikuwa na
matumizi ya nguvu yasiyo na msingi, mabomu ya machozi ya nini? Watu
walitawanywa kwasababu gani? Kwa mamlaka ya nani? Na faida ya nani? Je hii
ndiyo demokrasia tunayoitaka? Huu ndiyo tunaouita ushindi halali? Uhalali uko
wapi hapa?
Baada ya kuona upungufu huu , sasa tuone nini ambacho Dr
Kafumu anaweza kufanya ili kuienzi Demokrasia na kuwapa haki yao Wana Igunga;
1. Awe wa kwanza kulaani matumizi ya nguvu dhidi ya Wana Igunga
2. Awe wa kwanza kuhakikisha Ismail Aden Rage anachukuliwa
hatua kali za kimaadili
3.Awe wa kwanza kulaani harakati zozote za wanasiasa
kuingiza udini kwenye siasa
4.Awe wa kwanza kuomba radhi kwa niaba ya chama chake kwa
kukaa kimya au kushabikia siasa uchwara.
5 Awe wa kwanza ndani ya CCM na Tanzania kukataa ushindi huo
na kuitaka Tume kuitisha tena uchaguzi wa jimbo dogo la Igunga , hili lifanywe
pasipo kuangalia gharama za zoezi hilo, bali lifanywe ili kuuonyesha Ulimwengu
kuwa Dr Kafumu na CCM wameamua kusiamamia misingi ya Demokrasia pasipo kujali
gharama za hatua hiyo.
Haya ni mambo ya msingi kwa Dr Kafumu kuyasoma na kuyafanyia
kazi, hii itamjengea heshima sio tu ndani ya CCM bali kwa watanzania wote na
Ulimwengu mzima. Tafakari! A luta Continua!
Nova Kambota Mwanaharakati,
Wesneday, 5october,2011
Tanzania, East Africa.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)