Na Mwandishi Wetu
MBUNGE
wa Jimbo la Lindi Mjini, Salum Baruany amewashauri watu waliowahi
kusoma katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania kushirikiana katika
kufanikisha tamasha la kuchangia maendeleo ya elimu kwa ajili ya mikoa
hiyo.
Baruany
aliyasema hayo juzi katika kikao cha maandalizi ya tamasha la
kuchangia maendeleo ya elimu kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma
kilichofanyika Ukumbi wa Imasco, Temeke jijini Dar es Salaam.
Akiwa
mmoja wa waalikwa wa vikao hivyo vya kila wiki, Baruany alielezea
kukunwa kwake na ubunifu wa baadhi ya wanafunzi walioamua kuwahamasisha
wenzao kukumbuka walikotoka kielimu, kwa lengo la kuwainua wengine.
“Nawapongeza
sana. Ni wachache wanaoweza kukumbuka walikotoka, hasa kielimu. Hapa
mmelenga, mikoa ya kusini iko nyuma kielimu, naamini wa kusaidia
kupandisha hadhi ni ninyi wenyewe mliosoma kule na wadau wengine
wanaoguswa na suala hili.
“Msikate
tamaa, mtafanikiwa. Cha msingi ni kuwashirikisha na kuwashawishi
wengine waliosoma ana kuwa karibu na mazingira ya kielimu ya mikoa hii.
Nchi hujengwa na wananchi wenye moyo, nanyi kwa kuguswa
kwenu, naamini elimu ya kusini itainuka kwa sababu ni vigumu mtu mmoja
mmoja kuchangia na bado maendeleo ya kweli yakaonekana, bali kupitia
mshikamano kama wenu,” alisema mbunge huyo.
Naye
Mratibu wa tamasha hilo, Asanterabbi Mtaki, licha ya kumshukuru mbunge
huyo kwa nasaha zake, aliwataka wadau wa elimu nchini kuungana na
waliosoma mikoa ya kusini ili kufanikisha azma ya kuiinua kusini
kielimu.
“Tangu
awali tumeelezea hali ya elimu ya mikoa ya Kusini, kwa kweli si nzuri
na inahitajika nguvu ya ziada, ndiyo maana tumeungana kuhakikisha
tunafanikisha kitu kwa ajili ya shule za kusini na wanafunzi wake, hasa
yatima, walemavu na wasiojiweza ili wapate haki ya kupata elimu bora,”
alisema Mtaki.
Alisisitiza
kuwa, kasi ya maandalizi ya tamasha hilo inaridhisha na kuongeza kuwa,
nafasi ya waliosoma kusini kuchangia mawazo bado ipo, hasa kupitia
vikao vya kila mwisho wa wiki vinavyofanyika ukumbi wa Imasco.Kwa Hisani Ya Full Shangwe Blogu
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)