CCM Kumejaa Mizengwe Mingi, Tutapoteza Dola 2015 – UVCCM - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

CCM Kumejaa Mizengwe Mingi, Tutapoteza Dola 2015 – UVCCM

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Hussein Bashe, ameonya kuwa iwapo CCM hakitajadili matatizo ya wananchi sasa, kitarajie kupoteza dola mwaka 2015, kama ilivyotokea kwa chama tawala Zambia. Akizungumza katika Kata ya Kasamwa wilayani Geita katika maadhimisho ya miaka 33 ya kuanzishwa kwa UVCCM, Bashe alisema kuwa uchaguzi wa Zambia umemalizika na chama kilichoongoza kwa zaidi ya miaka 20 kimeondolewa madarakani, tukio linalopaswa kuwa funzo kwa CCM. Alisema CCM ya leo siyo ile ya miaka 10 iliyopita na kwamba ndani yake kumejaa migawanyiko mingi aliyoieleza kuwa haina maslahi kwa watu wanaowaongoza huku, akisema kumejaa mizengwe mingi na matokeo yake watu wamekuwa wakikimbilia upinzani. “Lazima tujiulize maswali kulikoni hali hii? Lakini majibu tunayo ni kwa sababu UVCCM imeshindwa kufikia mahitaji ya vijana wengi na sasa wanakichukia chama hiki.” Alisema vijana wengi wamezaliwa na kukua na kuukuta uhuru ambao leo, unasherehekewa na taifa kutimiza miaka 50. Wakati huo vijana wa CCM nao wakisherehekea miaka 33 ya kuzaliwa umoja wao, uhuru huo umetokana jitihada binafsi za wazee na vijana wa wakati ule, vijana wa sasa hawana habari na uhuru. “Nimeambiwa CCM tulishindwa uchaguzi katika Kata ya Kasamwa tuliyopo ambayo tunaadhimisha miaka 33 ya umoja wetu. Kata ipo chini ya Chadema na nimeambiwa hapa kumewahi kutokea vurugu. Labda niseme jambo moja kuwaambia Kasamwa uamuzi mlioyafanya wa kuchagua kutoka Chadema ni wenu na ndiyo demokrasia. Mmempa udiwani mbaye hatokani na CCM, lakini niwaombe tofauti za kisiasa zisiwagawe kufikia hatua ya kushambuliana.” “Nilipata taarifa kwamba mlifikia hatua ya kuchomeana nyumba hapa Kasamwa. Niwaombe vijana wenzangu haya maslahi ya kisiasa yasitugawe vijana wenzangu, tutofautiane kwa sera na itikadi, lakini tusivurugane, haisaidii mtu yeyote ikitokea vurugu hapa na vijana ndiyo watakuwa wa kwanza kuathirika.”

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages