Meneja uzalishaji kutoka Kampuni ya
Usambazaji kazi za wasanii ya Steps Entertainment (Kulia) akifafanua masuala
mbalimbali kuhusu kazi zinazofanywa na kampuni hiyo kwenye Jukwaa la Sanaa
linalofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA.Kushoto ni Katibu Mtendaji wa
BASATA,Ghonche Materego
Kushoto ni Katibu Mtendaji wa
BASATA,Ghonche Materego akiongea na wasanii kuhusu usambazaji wa kazi zao kwenye
Jukwaa la Sanaa wiki hii.Wengine kutoka kulia ni watendaji kutoka Kampuni ya
Usambazaji ya Steps Claud,Jairay na Kambarage
Afisa anayeshughulikia maudhui ya
kazi za Filamu kutoka Bodi ya Filamu Bw.Tairo akieleza kuhusu zoezi la ukaguzi
wa kazi za filamu
Msanii wa Filamu Michael Sangu akihoji
masuala mbalimbali kuhusu usambazaji wa kazi zao kwa Watendaji wa Kampuni ya
Usambazaji ya Steps.Mjadala ulikuwa mzito
Mdau huyu naye alikuwa ameandaa
nondo za kutosha kwa ajili ya kupata ufafanuzi na maelezo kuhusu usambazaji wa
kazi za wasanii nchini
Wasanii wakifuatilia mjadala
kuhusu mikakati ya kuboresha usambazaji wa kazi za wasanii nchini
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) kupitia program yake ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa imewakutanisha
wasanii na moja ya Kampuni ya usambazaji kazi zao ya Steps Entertainment kwa
lengo la kuja na mikakati ya pamoja ya uboreshaji wa soko.
Wakizungumza kwenye Ukumbi wa
Baraza hilo,wasanii wengi walitupa lawama kwa wasambazaji hao kwa kile
walichodai kwamba,wamevuruga mfumo wa usambazaji wa kazi zao hapa nchini kiasi
cha kufanya wasambazaji wengine waliokuwepo kushindwa kuhimili.
Walizitaja sababu
zilizosababisha kuvurugika kwa mfumo wa usambazaji wa kazi za wasanii kuwa ni
pamoja na wasambazaji hao kushusha bei za CD/DVD hadi shilingi elfu
moja,kutokusambaza kazi za wasanii wanaochipukia hadi zishirikishe wasanii
maarufu na kutokuwepo kwa mfumo eleweka wa bei.
Sababu zingine ni wasambazaji
kuwabana wasanii wenye majina (maarufu) kushirikiana na wale
wanaochipukia,ununuaji wa hakimiliki za wasanii kinyume cha sheria za
hakimiliki,kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa kugawa kazi za wasanii kwenye madaraja
na sababu nyingine nyingi.
“Leo hii CD zinauzwa mtaani kwa
shilingi elfu moja,hivi kweli kazi za wasanii wa Tanzania zimefikia kiwango cha
kuuzwa kwa shilingi elfu moja?Ni msambazaji gani ataweza kuhimili ushindani
wakati kuna kampuni imeshusha thamani ya kazi za wasanii kwa kiwango hiki?
Alihoji Michael Sangu ambaye ni Msanii wa Filamu.
Akijibu hoja za wasanii,Meneja
wa Uzalishaji wa Kampuni ya Steps Entertainment, Kambarage Ignatus alisema
kwamba,Kampuni yake inafanya biashara hivyo inajikita katika kutafuta faida na
kusambaza kazi zenye ubora na kuuzika.
Aidha alikanusha shutuma kwamba
kampuni yake imekuwa ikiwabana wasanii maarufu wasifanye kazi na wale
wanaochipukia huku akisema kwamba,usambazaji wa kazi yoyote ya msanii ni
makubaliano baina yake na kampuni ambayo yanakuwa kwenye mkataba.
“Kampuni ya Steps inafanya
biashara na kuhitaji faida hivyo, inanunua na kusambaza kazi zenye ubora na
zinazokubalika kwa wateja.Hatuwezi kusambaza kila kazi ya msanii,wasanii ni
wengi sana ila tunalenga zile zenye ubora na kuuzika”alisisitiza
Kambarage.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji
wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,tatizo linalojitokeza ni kwa baadhi ya
wasanii ama kutozingatia mikataba au kutokujua umuhimu wake hivyo kuahidi
kuandaa programu maalum ya elimu ya mikataba kwa wasanii.
“Ndugu zangu kupitia Jukwaa hili
nimejifunza kwamba,wasanii hatuzingatii mikataba na hata hatuoni umuhimu
wake.Baraza sasa linajipanga kuwaleta wataalam mbalimbali wa mikataba na
hakimiliki ili kuwajengea uelewa wasanii” aliahidi Materego.
Aidha,aliwaahidi wasanii
kwamba,BASATA kwa kushirikiana na Mashirikisho ya Sanaa nchini litaandaa
utaratibu wa kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa bei unaoeleweka kwa kazi za
wasanii.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)