Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa ukosefu mkubwa wa ajira na nafasi za kujiendeleza kwa
vijana wa Afrika ni bomu linalosubiri kulipuka na linalohitaji majawabu
ya haraka kulizuia lisilipuke.
Rais Kikwete amesema
kuwa ni wajibu na jukumu la viongozi wa Afrika kuwekeza ipasavyo katika
vijana ili kuwawezesha kutimiza nafasi yao ya Kihistoria kwa sababu
vijana ndio mhimili wa leo na kesho wa “familia , jamii zetu na mataifa
yetu.”
Rais Kikwete ameyasema
hayo Alhamisi, Juni 30, 2011, wakati alipokuwa akizungumza katika
Mkutano wa 17 wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU)
unaotarajiwa kumalizika Julai 01, 2011 katika Ukumbi wa AU wa Palace of
Conferences katika kijiji cha kisasa cha Sipopo, nje kidogo ya mji
mkuu wa Malabo, ulioko katika Kisiwa cha Bioko cha Equatorial Guinea.
Akichangia katika
mjadala wa mada kuu ya Mkutano wa mwaka huu ya “Uharakishaji wa
Uwezeshaji wa Vijana kwa Maendeleo Endelevu”, Rais Kikwete amependekeza
njia kuu za kusaidia kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na hata
nafasi za kujiajiri kwa vijana wa Afrika.
“Afrika ni bara dogo kwa
umri kwa sababu ya wakazi wake wengi ni vijana na ongezeko la watu
kwenye Bara hili ni kubwa kuliko eneo jingine duniani. Lakini vijana wa
Afrika wanakabiliwa na changamoto nyingi, kubwa kuliko zote ikiwa ni
ukosefu wa ajira.
“Ni bomu ambalo
likiachiwa bila kushughulikiwa ipasavyo, litakuwa chanzo kikubwa cha
kuyumba kwa nchi zetu zote,” Rais Kikwete amewaambia viongozi wenzake
na kuongeza:
“Mageuzi
tuliyoyashuhudia katika nchi za Kiarabu yanaweza kuwa ni mwanzo tu.
Vijana katika Afrika ni asilimia 37 ya watu wote walioajiriwa lakini
bado vijana ni asilimia 60 ya watu wasiokuwa na kazi katika Bara letu.
Sisi, wazazi, viongozi wa Serikali zao tuna wajibu maalum kwa vijana
wetu. “
“Kwanza kabisa ni lazima
tuhakikishe kuwa vijana wetu wanakua na kuwa watu wazima katika afya
njema, tuhakikishe kuwa wanapata elimu bora na tufanikishe wapate ajira
za heshima na zenye malipo mazuri. Siyo kazi rahisi lakini ni lazima
tuifanye.”
Kuhusu nini kifanyike,
Rais Kikwete kwa kutumia uzoefu wake wa kuwa mjumbe wa Tume ya
Denmark-Afrika Kuhusu Ajira kwa Vijana Katika Afrika amesema kuwa hatua
kubwa ambazo viongozi wa Afrika wanapaswa kuzichukua ni pamoja na
kubuni sera nzuri za kisiasa, kiuchumi na kijamii ambazo zinaweza
kusaidia kufungua uwezo mkubwa wa vijana wa Afrika.
Rais Kikwete amesema
kuwa sera hizo zilenge kuchochea ukuaji mkubwa zaidi wa uchumi,
ongezeko kubwa la uwekezaji katika uchumi wa Afrika, ongezeko la uwezo
wa ushindani na kuzalishwa kwa nafasi nyingi zaidi za ajira kwa vijana.
“Tunahitaji kubuni sera
mwafaka zitakazowawezesha vijana wetu kupata ujuzi ambao utawawezesha
kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe; sera ambazo zitawawezesha kujipatia
uwezo wa kuwa wazalishaji mali wa kuweza kuendesha biashara nzuri; sera
ambazo zitachochea maendeleo ya sekta binafsi ili sekta hiyo iweze
kuzalisha ajira kwa ajili ya vijana wetu, wasichana na wavulana,”
amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye
anashiriki Mkutano huo wa 17 wa AU anatarajiwa kuondoka mjini Malabo
kuelekea nyumbani kesho, Jumamosi, Julai 02, 2011.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
Malabo, Equatorial Guinea.
01 Julai, 2011
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)