Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Lawrence Mafuru akimkabidhi Bi. Anna Leon Mushi tuzo ya ‘Mkurugenzi Mtendaji’ katika hafla ya kila mwaka ambayo benki hiyo ilikabidhi tuzo mbalimbali kwa wafanyakazi wake bora maarufu kama ‘Heshima Awards’ jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya NBC wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Lawrence Mafuru (wa sita kushoto mstari wa nyuma) katika hafla ya kila mwaka ambayo benki hiyo hukabidhi tuzo mbalimbali kwa wafanyakazi wake bora maarufu kama ‘Heshima Awards’ jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
.....................................
NA MWANDISHI WETU
JUMLA ya wafanyakazi kumi na tatu wa Benki
ya NBC Tanzania wamekabidhiwa zawadi mbalimbali kutokana na utendaji kazi wao
uliotukuka katika sherehe zilizofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Kwa kawaida kila mwaka NBC hutoa tuzo katika tukio
lijulikanalo kama ‘Heshima Awards’ ikiwa ni kama ishara ya Menejimenti ya NBC
kuridhishwa na utendaji kazi wa wafanyakazi wa benki hiyo kwa mwaka wa fedha
uliopita.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwatunukia
wafanyakazi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Lawrence Mafuru alisema kuwa hiyo
ilikuwa ni mara ya nne kwa wafanyakazi kutunukiwa Heshima Awards.
“Kila mwaka huwa tunaangalia vipengele vinne katika
tuzo zetu navyo ni Jamii; Wateja; Uongozi/Wafanyakazi na Fedha/Wanahisa,” alisema
Mafuru.
Washindi walikabidhiwa vyeti, fedha
taslimu huku majina yao yakipelekwa kushindanishwa kwenye tuzo za benki mama ya
NBC, ABSA.
“Wafayakazi
wote wa NBC walishiriki kuwachagua washindi hawa kwa kujaza fomu maalumu na
kutoa sababu za kuwachagua wastakaoshindania tuzo za fedha, shaba na dhahabu. Kisha
fomu hizo hukabidhiwa kwenye Kamati Maalumu ya Heshima Awards kwa shughuli za
kukamilisha zoezi lenyewe,” alisema Mafuru.
Washindi wa mwaka huu waliopata tuzo za dhahabu ni Rajab Maalim( tawi
la Zanzibar), Salma Yatera(tawi la Moshi), Jacqueline Sindano(tawi la Corporate,
Dar-es-Salaam), na Margareth Touwa(tawi la Mwanza) na zawadi kubwa kabisa ya hafla hiyo ya mshindi wa MD iliangukia kwa Anna Leon Moshi kutoka tawi la NBC Babati.
“Hakika tukio hili linahamasisha sana. Linaonyesha jinsi uongozi wa NBC
unavyowajali wafanyakazi wake,” mmoja wa waalikwa alisema baada ya washindi
kutunukiwa.
Washindi siku zote ni wale waliofanya jambo kubwa
litakalowashawishi wajumbe wa kamati na wafanyakazi wote wa benki kuamini kuwa
muhusika anapaswa kuzawadiwa.
Miongoni mwa mifano iliyowazi ni tukio la Desemba
mwaka jana wakati Luciana Kipiko alipopokea hundi yenye thamani ya Sh 46,750,000
iliyochukulewa kwenye Tawi la Corporate Dar es Salaam na kupelekwa tawi la Dodoma.
Baada ya kuishitukia, Luciana aliituma kwa fax Dar es Salaam ili
ithibitishwe na hata ilipothibitishwa bado Luciana aliitilia shaka na kuamua
kumpigia simu Meneja wa Corpaorate, na ikagundulika kuwa ilikuwa imeghushiwa.
“Kitu kama hicho kilitokea kwa mfanyakazi wa Tawi la
Mwanza, Margareth Touwa aliyeishitukia hundi ya Sh 221,000,000 iliyopelekwa na Mnada Enterprises Machi mwaka jana na kesi bado iko
mahakamani.
“Hivyo ni muhimu kama
si lazima kwa NBC kuthamini michango na kujitolea kwa dhati kunakofanywa na
wafanyakazi wa aina hii,” alisema MD.
Ends
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)