MVUTANO MKUBWA WAIBUKA SINGIDA NAKUPELEKEA MADIWANI WA CHADEMA KUTOLEWA MEZA KUU…!!! - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MVUTANO MKUBWA WAIBUKA SINGIDA NAKUPELEKEA MADIWANI WA CHADEMA KUTOLEWA MEZA KUU…!!!


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singidan Selestine Yunde akifungua kikao cha baraza la madiwani. Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Illuminata Mwenda na kushoto ni Makamu Mwenyekiti  Higa Mnyawi.
Diwani Christowaja akiuliza swali mbele ya baraza la madiwani.
Diwani Christowaja Mtinda (wa pili kutoka kulia) na Christina Muhwai (wa kwanza kulia)wakitolewa meza kuu.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida waliohudhuria kikao cha baraza cha la madiwani.Picha zote na Nathaniel Limu
-
Na Nathaniel Limu
Bundi bado anaendelea kuunguruma ndani ya vikao vya baraza la madiwani (full council) katika halmashauri ya wilaya ya Singida, baada ya kikao cha kawaida cha baraza kusimama kwa takribani saa moja, kuruhusu madiwani wawili wa CHADEMA kuondolewa meza kuu.
Madiwani walio ondolewa kwenye meza kuu ni Christowaja Mtinda na Christina Mughwai ambao wote hao ni wabunge wa viti maalum.

Madiwani hao walikubana na dhahama hiyo baada ya Christowaja kuuliza swali juu ya mapato na matumizi.Swali hilo lilipelekea madiwani wa CCM wapato 63 (madiwani wa CHADEMA wapo sita tu) kupinga swali hilo kuulizwa na kiongozi ambaye amekaa meza kuu, wakidai kuwa itifaki hairuhusu mjumbe kukaa meza kuu na kuuliza maswali, badala yake anatakiwa kujibu maswali.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Illuminata Mwenda, aliingilia kati na kukieleza kikao hicho kuwa madiwani hao wawili wa CHADEMA, hawakujipeleka meza kuu isipokuwa walitengewa viti kwenye meza hiyo na uongozi wa halmashauri.

hata hivyo, hoja hiyo ilipigwa vikali na madiwani wa CCM huku wakipiga piga kwa nguvu meza zao na kupaza sauti kuwa “watoke huko meza kuu waje waungane na sisi huku chini”.
Baada ya hapo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Selestian Yunde aliagiza madiwani hao watengewe meza sawia na wenzao wa kata na wa viti maalum ambao sio wabunge.
Bundi huyo alianza kuunguruma mapema tu mara mwenyekiti Yunde alipomaliza hotuba yake ya ufunguzi wa  kikao hicho na kumruhusu msemaji wa kwanza, ambaye alikuwa ni diwani wa kata Mujughuda Frank Nyekele kuuliza swali.

Nyekele aliomba kuelezwa ni hatua gani zizochukuliwa dhidi ya diwani Christowaja kutokana na kitendo chake cha kutamka kuwa madiwani wa CCM, shida yao ni kulipwa posho tu na hawako kwa maslahi ya wananchi, swali ambalo liliungwa mkono na madiwani wa CCM kwa kupiga piga meza kwa nguvu kama kawaida yao.

Christowaja alijibu mapigo kuwa hatafuta wala kuomba radhi kwa matamshi yake hayo, kwa madai kwamba, madiwani wa CCM wametafsiri vibaya matamshi yake hayo.
Kama hiyo haitoshi, wakati Makamu Mwenyekiti Higa Mnyawi akisoma taarifa ya mapato na matumizi ya kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, alitamka kuwa yupo diwani mmoja anayejifanya yeye ni ‘diwani sanaa’, kwa malidai kuwa anaikwamisha halmashauri kukusanya mapato yake ya ndani.

Alidai kuwa ‘diwani sanaa’ huyo, amewakataza wananchi wa jimbo lake kulipa ushuru mbalimbali ukiwemo wa mazao.

Baada ya Mnyawi ambaye ni diwani wa kata ya Ikhanoda kumaliza kutoa taarifa yake, Christowaja alisimama na kuomba ufafanuzi wa maana halisi ya ‘diwani sanaa’ ili hali yeye anavyofahamu, ni kwamba madiwani wote wako sawa.

Ghafla mwenyekiti Yunde, aliingilia kati huku akionyesha wazi kukerwa na malumbano hayo na kusema “sasa naona mnataka kuanza kuniletea matatizo yenu, hapa hakuna diwani sanaa, madiwani wote tupo sawa, sitaki kusikia tena diwani yo yote anatamka ‘diwani sanaa”.
Katika kikao cha baraza la madiwani cha bajeti kilichopita hivi karibuni, kulitokea songombingo ya aina yake kati ya madiwani wa CCM na CHADEMA na kusababisha bajeti kupitishwa bila ya kusomwa kifungu kwa kifungu.

Kitendo cha kuwatoa meza kuu madiwani wa CHADEMA ambao ni wabunge, kimewagawa madiwani wa CCM katika makundi mawili, moja likidai kutolewa kwa wabunge hao ni sahihi, huku wengine wakidai kuwa wabunge hao wameonewa.
Wamedai kuwa miaka yote wabunge wa CCM wamekuwa wakikaa meza kuu na kuuliza maswali kama alivyofanya Christowaja.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages