KWANINI HAWATAKI KUJIBU HOJA? - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

KWANINI HAWATAKI KUJIBU HOJA?


 
Na Nova Kambota,

  Tangu kuibuka kwa maandamano ya CHADEMA ya mkoa kwa mkoa kuna mambo kadhaa yaliyojitokeza na yanaendelea kujitokeza ambayo yanadhihirisha kile ambacho wachambuzi hukiita “ ombwe la uongozi” , kwa kujua au kutojua tumeshuhudia mara kadhaa serikali ikiacha kila mwenye kuweza aisaidie serikali kujibu hoja na kibaya zaidi ni kuwa wasaidizi hawa wanaonekana kupwaya mno kwenye kujibu hoja za msingi badala yake wamegeuka kuwa waropokaji.

  Miongoni mwa watu wanaofanya kazi isiyowahusu ni pamoja na watendaji mbalimbali wa chama tawala CCM ambao wamekuwa na tabia hii inayorudisha nyuma maendeleo, viongozi hawa wa CCM wamelewa madaraka kiasi kwamba wanajiona wao ndiyo serikali na serikali ndiyo wao, wamefikia hatua ya kupindisha ukweli na kuendesha vituko na siasa za majitaka kwenye mambo ya msingi yanayogusa wananchi .

    Chukulia mfano wa hoja zinazotolewa na CHADEMA kwenye maandamano yao ambazo kwa hakika ni sauti za wananchi tena masikini kabisa ambao wanaiuliza serikali yao juu ya mustakabali wa maisha yao na watoto wao, cha kuhuzunisha ni kuwa licha ya mikutano hii ya CHADEMA kuwa ya halali kabisa kikatiba pia kuendeshwa kwa utulivu mkubwa bado serikali inachukulia kuwa ni uchochezi hivyo badala ya kuja na majibu ya msingi ya hoja zinazoibuliwa kwenye mikutano hiyo serikali imewaachia wanapropaganda wa CCM kuyumbisha nchi wanavyotaka.

     Hivi CHADEMA na wananchi wanapohoji juu ya ubabaishaji kwenye shule za kata kuna kosa hapo? au pale mwananchi mmoja wa Mbeya alipotaka kufahamu hiyo meli waliyoahidiwa ziwa Nyasa itakuja lini kuna kosa hapo?  au yule mwananchi wa Rukwa aliyetaka kufahamu lini serikali itahakikisha huduma za afya zinakuwa za uhakika? Au kuna tatizo lolote wavuja jasho wa nchi hii wanaposema kwa sauti kubwa kuwa hawataki kulipa madeni ya kubambikiwa kama Dowans? Hivi hapa kuna tatizo lolote? Kwanini serikali isitoe majibu ya kina kwa maswali haya badala yake wanaachiwa waropokaji? Au serikali inadhani wananchi masikini wa taifa hili wanashiba kejeli za viongozi wa CCM?

     Wakati wananchi wanataka kuona wezi wote wa mali za umma wanafikishwa mahakamani bila huruma tena pia wanataka kufahamu ufisadi unaonuka kwenye ofisi za serikali utakoma lini? cha ajabu anaibuka Nape Nauye katibu wa itikadi na uenezi wa CCM anamtuhumu Dr Slaa kuwa na yeye ni fisadi tu, hii ndiyo nini sasa?, hapa ndiyo watu wanahoji Nape katumwa na nani kuwadhihaki masikini wa taifa hili? Kwanini asikae kimya akamwacha Dr Shukuru Kawambwa akatujibu ni lini shule za kata zitaboreshwa? Itamgharimu nini Nape kukaa kimya ili Kikwete atwambie Dowans tunawalipa kwa misingi ipi? 

        Wananchi wanahoji kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha,  bei ya vitu imepanda na viongozi wa CHADEMA wanaitaka serikali kuhakikisha bei ya vitu inashuka ili kumsaidia mvuja jasho , haya ni mambo ya msingi sio mzaha kabisa, sasa Nape anaita waandishi wa habari kisha anasema Dr Slaa ni fisadi na Mbowe ni fisadi wakae kimya mara moja! , haya kama sio matusi ni nini? huu ni mzaha kwa wananchi na inabidi kukemewa haraka vinginevyo tabia hii itaendelea kukua mwisho wa siku tutamwona katibu mkuu wa CCM akisoma hotuba ya mwisho wa mwezi kwa niaba ya rais wa nchi, ndiyo inaonekana kama kichekesho ila hakika tunaelekea huko.

      Ni lazima kama taifa ifike sehemu tufahamu kuwa kuna mambo ya siasa na maisha ya watu hivyo tusiweke mzaha kwenye kila jambo ni lazima wananchi wanapoihoji serikali basi ni watendaji wa serikali wanaopaswa kujibu, viongozi wa chama wakae kimya waache kuropoka hovyo wakumbuke kuwa hii nchi ni yetu sote hivyo wasijifanye kujimilikisha. Sidhani kama serikali imefaidika kitu na majibu ya kejeli yanayotolewa na viongozi wa CCM kwa wananchi badala yake wananchi wanazidi kujenga chuki dhidi ya serikali yao .

       Wananchi wanaendelea kuuliza na wataendelea kuhoji kwanini viongozi wa serikali hawajibu hoja? Hakika hili litaendelea kuwaandama kokote walipo na kamwe haliwezi kupoozwa kwa kuwaruhusu viongozi wa CCM kuropoka hovyo bila mpangilio pasipo kujua kuwa wanazidi kukoleza chuki. Naam! imefika wakati sasa serikali iache kufanya vitu kwa mazoea, iache kutoa majibu ya zamani kwa maswali mapya halikadhalika iache kutoa majibu mepesi kwa hoja nzito, propaganda zozote za kuwatumia kina Nape na viongozi wengine wa CCM kuzima hoja za msingi za wananchi  hazina manufaa yoyote badala yake zinazidi kuibomoa na kuidhoofisha serikakali…..

Tafakari!
  
         0717  709618   /    0766-730256,
       novakambota@gmail.com,

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages