WANANCHI,WAANDISHI MKOANI MOROGORO WALAANI KITENDO CHA POLISI KUVAMIA OFISI ZA GLOBAL PUBLISHER - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WANANCHI,WAANDISHI MKOANI MOROGORO WALAANI KITENDO CHA POLISI KUVAMIA OFISI ZA GLOBAL PUBLISHER

 
Thadei Hifigwa, Katibu Mkuu wa Moro Press Club akihojiwa na mtandao huu ofisini kwake leo.
CHAMA cha waandishi wa habari mkoa wa Morogoro (Moro Press Club) na wananchi,  wamesikitishwa na kitendo cha askari wa kutuliza ghasia (FFU) kuvamia ofisi za  kampuni ya Global Publishers zilizopo Bamaga, Mwenge, jijini Dar es Salaam na kuwashambulia waandishi na wafanyakazi wa kampuni hiyo. 

Katika kauli na taarifa mbalimbali, wametaka wote waliohusika wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo ya askari kujiona wako juu ya sheria.

Akizungumza na mtandao huu katika ofisi za chama hicho zilizopo mjini Morogoro,  Katibu Mkuu wa chama hicho, Thadei Hifigwa,  alisema chama chake kimestushwa na taarifa za polisi kuingia chumba cha habari cha Global Publishers na kuwashambulia waandishi wa habari na wafanyakazi wengine waliokuwa kazini.

"Waandishi wote wa habari Mkoa wa Morogoro tunalaani vikali tukio hilo na tunatoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali askari wote walioshiriki  uovu huo, na tunawapongeza viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuchukua hatua za mwanzo dhidi ya wahusika na kuwafariji waathirika wa tukio hilo sambamba na kuomba radhi,”  alisema Hifigwa kwa hisia kali akivitaka vyombo vya usalama kufanya kazi kwa nidhamu bila kubugudhi raia.

Pia, akizungumza na mtandao huu nyumbani kwake maeneo ya Nane Nane mjini hapa leo asubuhi,  aliyekuwa mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini-Mashariki, Semindu Pawa, alisema amezipokea taarifa za tukio hilo kwa mashangao na masikitiko makubwa.

"Mimi toka kustaafu kwangu ubunge mwaka 2005 sikuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari lakini kwa hili la polisi kuvamia ofisi za magazeti na kupiga waandishi limeniuma sana,” alisema Pawa akishangaa kuongezeka kwa matumizi ya nguvu ya polisi dhidi ya raia.

Alitolea mifano ya matumizi ya nguvu nyingi dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu na mauaji ya jeshi hilo yaliyofanywa huko Arusha wakati wa maandamano  ya Chadema.
 
Mbunge mstaafu, Semindu Pawa, akipozi kwa picha baada ya mazungumzo na mtandao huu.
PICHA ZOTE NA DUNSTAN SHEKIDELE, / GPL, MOROGORO

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages