Lakini Dk Slaa alifarijiwa na wafuasi hao wa Chadema baada ya kumueleza kuwa watampa kura za urais, lakini hawatampa waziri huyo wa zamani kura za ubunge.
Tukio hilo lilitokea jana, katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kibondo Mjini ambako Dk Slaa alipata wakati mgumu kumnadi Ntagazwa, ambaye alitangaza kuihama CCM na kujiunga Chadema Agosti 7 mwaka huu.
Wakati Dk Slaa akijaribu kumnadi, wananchi walipiga kelele wakieleza kuwa hawatamchagua waziri huyo wa zamani wa Ardhi, Maliasili na Utalii na ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira.
Hali ya hewa kwenye mkutano huo wa kampeni ilianza kubadilika baada ya Dk Slaa kumaliza kuhutubia na kuanza kuwaombea kura wagombea ubunge na udiwani.
"Mtamchagua Ntagazwa," aliuliza Dk Slaa lakini akajibiwa kwa sauti moja: "Hatumchagui!"
Dk Slaa aliendelea kusema: “Kama mnavyomjua Ntagazwa ni mwadilifu na ninahitaji kufanya naye kazi katika serikali yangu. Haya nauliza tena ni wangapi watampa kura Ntagazwa na wangapi hawatampa?"
Wakiwa wameshonyesha mikono yao juu, wananchi hao walijibu kwa pamoja na kwa kelele kubwa zaidi wakisema: "Ntagazwa hatumpiii."
Baada ya kuona hali ni mbaya, Dk Slaa alisema: “Haya sasa; maamuzi mtayafanya wenyewe. Unajua tukiwa madikteta sio vizuri. Siwezi kuwalazimisha mmchague Ntagazwa kwa sababu najua ninyi mna maamuzi yenu.”
Baada ya majibu hayo, Dk Slaa alisema ni vyema wananchi kueleza hisia zao na kuweka wazi msimamo wao, lakini akamwita Ntagazwa ili asalimie wananchi hao.
Aliposimama Ntagazwa na kusalimia hakuomba kura badala yake aliwaomba wananchi hao kuichagua serikali ya Chadema kwa kumpa kura Dk Slaa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mgombea ubunge anayeungwa mkono katika jimbo hilo ni Felix Mkosamali kutoka chama cha NCCR-Mageuzi, ambacho kwa muda mrefu sasa kinaonekana kuwa na nguvu kwenye jimbo hilo.
Akihutubia kwenye mkutano huo, Dk Slaa alisema serikali ya CCM inavuruga msingi wa umoja wa Watanzania uliojengwa na rais wa serikali ya awamu ya kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema ujenzi wa shule za kata unawafanya watoto wa Kitanzania kusoma kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha sita katika eneo alilozaliwa, hali aliyoielezea kuwa iwanyima Watanzania uzalendo na fursa ya kuijua nchi yao .
“Nchi hii ilijengwa kwa gharama kubwa na Nyerere, lakini CCM inaweka matabaka; inawajengea ubaguzi watoto wa kitanzania; taifa linameguka,” alisema.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kufanya maamuzi magumu kama yale aliyoyafanya Nyerere, kwa kuikataa CCM na kuinyima kura Oktoba 31.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)