Mbunge wa jimbo la Ubungo-Chadema Mh John Mnyika-
---
Nchi imeingia tena katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na
Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28
Julai 2012.
Hali hiyo ni matokeo ya Serikali kutozingatia tahadhari niliyoitoa
bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kwa
nyakati mbalimbali kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini juu ya hali tete iliyotarajiwa kuwepo na hatua zinazopaswa
kuchukuliwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.
Ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuisimamia Serikali nawataka
viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO) kuacha kuficha hali ya mambo na kuwaeleza ukweli
wananchi kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na hatua za haraka
zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Iwapo Wizara na TANESCO hawatatoa matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa
nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya
mgawo wa umeme uliojitokeza ili hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu
ambapo wajumbe wa kamati ya nishati na madini wenye wajibu wa kuisimamia
Serikali kwa niaba ya Bunge katika sekta hizo nyeti hawajateuliwa.
Aidha, pamoja na kutoa maelezo kuhusu mgawo wa umeme, Wizara ya Nishati
na Madini na TANESCO watumie nafasi hiyo pia kueleza hatua
zilizochukuliwa kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili kuhusu tuhuma za ufisadi
katika ununuzi wa vifaa na uzalishaji wa umeme wa dharura ikiwemo
kuhusu mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
Ikumbukwe kwamba mwanzoni mwezi Agosti 2012 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (NAOT) iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi
maalum wa hesabu za Shirika la Umeme (TANESCO) kufuatia tuhuma za
ubadhirifu wa fedha za umma zilitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani tarehe 27
Julai 2012 na Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya hoja
ya Serikali tarehe 28 Julai 2012.
Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO waeleze pia hatua iliyofikiwa
kuhusu uchunguzi mwingine uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi
wa Umma (PPRA) kuanzia mwezi Agosti 2012 wa mchakato wa ununuzi wa
mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme wa dharura kutokana
na tuhuma mbalimbali zilizotolewa bungeni kuhusu ununuzi huo suala
ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27 Julai 2012 liundiwe
kamati teule ya Bunge ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
27 Februari 2013
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)