Serikali, kuanzia leo tarehe
01 Agosti, 2012, imewavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi 38,050 wa kutoka Burundi
wanaohifadhiwa katika kambi ya wakimbizi
ya Mtabila iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Uamuzi huu wa kuwavua hadhi
ya ukimbizi umefanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
kwa Mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Wakimbizi.
Kufuatana na Sheria hiyo
mkimbizi anapoteza hadhi ya ukimbizi kama mazingira yaliyomfanya kuwa mkimbizi
yatakuwa hayapo tena, na atavuliwa hadhi hiyo kama ataendelea kukaidi maagizo
halali ya kumtaka kurejea kwao kwa hiari.
Hatua ya kuwavua hadhi ya
ukimbizi wakimbizi hawa imefikiwa baada ya Serikali za Tanzania na Burundi na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kujiridhisha kuwa
hapakuwa tena na sababu ya kuendelea
kuwahifadhi wakimbizi hao baada ya hali ya amani kurejea nchini mwao na
hivyo kuwataka kurejea kwao.
Zoezi la kuwasaili wakimbizi
waliopo katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila lilifanyika kuanzia mwezi Septemba
hadi Desemba mwaka 2011 kwa lengo la kubaini kama walikuwepo wakimbizi wenye
sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini, ambapo ilibainika kuwa wakimbizi
38,050 hawakuwa na sababu za kuendelea kuwa wakimbizi.
Kufuatia matokeo ya zoezi
hilo, Kikao cha Pande Tatu, kilichojumuisha wawakilishi wa Serikali za Tanzania na Burundi na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kilifanyika jijini Bujumbura nchini
Burundi tarehe 22 Februari, 2012 na kukubaliana kwa pamoja kuifunga kambi ya
Mtabila ifikapo tarehe 31 Desemba, 2012.
Baada ya kuwavua hadhi ya
ukimbizi, raia hawa wa Burundi sasa wataendelea kusaidiwa kurejea kwao kwa
hiari hadi tarehe 31 Desemba mwaka huu, ambapo Kambi hiyo ya Mtabila itafungwa
rasmi, na wale ambao watakuwa hawajaondoka baada ya tarehe hiyowatachukuliwa
kuwa ni wahamiaji haramu, na kushughulikiwa kufuatana na Sheria ya Uhamiaji.
Historia ya hifadhi ya
wakimbizi hapa nchini ilianza tangu mwaka 1961 ambapo Tanzania ilikuwa na idadi
kubwa ya wakimbizi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, idadi ambayo katika miaka
ya tisini ilifikia takribani milioni moja, 641,386 kati yao wakiwa ni wakimbizi
kutoka Burundi.
Zoezi la kuwarejesha kwao wakimbizi wa Burundi lilianza rasmi
mwaka 2002 baada ya nchi yao kurejea katika hali ya amani na hadi sasa kambi nane
zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi toka Burundi zimefungwa. Kambi hizo ni Karago,
Mtendeli, Kanembwa na Nduta zilizokuwa wilayani Kibondo, na Muyovosi iliyokuwa
wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Kambi nyingine zilizofungwa
ni Kitali iliyokuwa wilayani Biharamulo, Lukole A na B zilizokuwa wilayani
Ngara, mkoani Kigoma.
Kambi ya wakimbizi ya
Mtabila ndiyo itakuwa ya mwisho kufungwa katika mlolongo wa kambi zilizokuwa
zikihifadhi wakimbizi kutoka Burundi hapa nchini.
Imetolewa na
Isaac J.
Nantanga:
MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO
YA NDANI YA NCHI
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)