Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi
na Teknolojia, Habari na Utafiti { RAAWUZ } Bibi Mwatum Khamis Othman
akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bibi Mwatum aliambatana na Viongozi Waandamizi wa Chama hicho kufikisha
baadhi ya Kero zinazowakwaza Wafanayakazi wa Chama hicho katika maeneo
yao ya Kazi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Seif Ali Iddi akizungumza
na Ujumbe wa Jumuiya ya Viwanda ya Jamuhuri ya Sudan { Giad Industrial
Group } Ofisini kwa Vuga Mjini Zanzibar.
Kulia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ni Balozi wa Jamuhuri ya
Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed Ali.
Ujumbe wa Jumuiya ya Viwanda ya Nchini Jamuhuri ya Sudan { Giad
Industrial Group } ukifuatilia maelezo ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walipokutana Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Ujumbe huo uliongozwa na Balozi wa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr.
Yassir Mohammed Ali.
---
Wawekezaji wa Jamuhuri ya Sudan wameombwa kuangalia vyema mazingira ya
Zanzibar katika dhana nzima ya kuwekeza Vitega Uchumi vyao
vinakavyosaidia kushajiisha Uchumi wa Pande hizo mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli
hiyo hapo Ofisini kwake Vuga wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa
Jumuiya inayojishughulisha na Viwanda Nchini Sudan ya { Giad Industrial
Group } ukiongozwa na Balozi was Sudan Nchini Tanzania Dr.Yassir
Mohammed Ali.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria
kuimarisha Uchumi wake kupitia Sekta Tofauti ikiwemo ile yaViwanda kwa
kukaribisha Makampuni, Mashirika na Taasisi hisani.
Aliiomba Jumuiya hiyo ya Giad Industrial Group ya Sudan ambayo
imeshiriki na kupata ushindi katika maonyesho ya saba saba Mjini Dar es
salaam kujipanga vyema kuleta maombi yake ili ipate fursa ya kuwekeza
hapa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itakuwa tayari kuipa
mashirikiano Taasisi hiyo muhimu ambayo uzalishaji wa bidhaa zake
ambazo ni pamoja na fanicha unahitajika sana Nchini.
“ Zanzibar inahitaji takriban Madeski 25,000 katika Skuli zake Unguja na
Pemba ili kuondosha tatizo la vikalio kwa Wanafunzi wake. Hivyo kitendo
cha Jumuiya hiyo kuanzisha Tawi lake kunaweza kutatua kadhia hiyo”.
Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Mapema Balozi waa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed
Ali alisema Ujumbe wa Jumuiya hiyo upo Zanzibar kuangalia uwezekano wa
kuja kuwekeza Vitega Uchumi vyao Nchini.
Balozi Yassir alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif kwamba Uhusiano uliopo wa muda mrefu kati ya Tanzania na Sudan
ikiwemo Zanzibar kwa ujumla utaendelea kuimarishwa kwa ustawi wa Jamii
za pande zote mbili.
Ujumbe huo tayari umeshaahidi kufanya maandalizi ya kuandaa maombi ya
namna ya kuja kuwekeza Miradi yao hapa Zanzibar ndani ya kipindi cha
Mwezi Mmoja.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi amekutana na Uongozi wa
Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi na
Teknolojia, Habari na Utafiti { RAAWUZ } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Katika Mazunguimzo yao Katibu Mkuu wa Chama hicho cha Raawuz Bibi Mwatum
Khamis Othman alisema suala la ushirikishwaji wa Wafanyakazi katika
Bodi na Kamati za Uongozi ndani ya Taasisi za Kazi umesahauliwa kwa
kipindi kirefu sasa.
Bibi Mwatum alifahamisha kwamba endapo Uongozi katika sehemu za Kazi
ungekuwa ukiitumia vyema ile sheria nambari 10 ya Kamati za Uongozi
Makazini kusingekuwa na malalamiko mengi katika sehemu za Kazi.
Katibu mikuu huyo wa Chama cha RAAWUZ alivitaja vyuo viwili tu vya
Maendeleo ya Utalii Maruhubi na Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka ndivyo
pekee vyenye uwakilishi wa Wafanyakazi katika Kamati za Uongozi wao.
Bibi Mwatum na Ujumbe wake pia walizungumzia masuala kadhaa
yanayowakabili watendaji wa Taasisi za Kazi ikiwemo ukosefu wa uangalizi
wa afya wakiwa kazini,mishahara duni kwa wafanyakazi wazoefu pamoja na
bakaa ya fedha za Mishahara kwa wafanayakazi waliokatwa mishahara yao
wakati wa zoezi la mabadiliko ya mishahara.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja hizo Makamu wa Pili wa Raisn wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kwamba Serikali itaendelea
kushirikiana na Wafanyakazi katika Taasisi za kazi ili kuimarisha
ufanisi wa Kazi.
Balozi Seif alisema atahakikisha anaziandikia Taasisi zote katika kuona
ushiriki wa Wafanyakazi unapatikana vyema .
Aliueleza Ujumbe huo kwamba suala la Wafanyakazi wazoefu litaangaliwa
kutokana na mchango wao wa muda mrefu katika Taifa hili pamoja na
kusisitiza kuandaliwa utaratibu kwa wafanyakazi kupimwa afya zao.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)