Pages

MBUNGE wa Viti Maalumu CCM Mkoa wa Singida, Martha Gwau atoa bima za afya 400 kwa wanawake




MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Mkoa wa Singida  Martha Gwau ametoa bima za afya kwa wanawake 400 mkoani hapa ili ziwasaidie kupata matibabu. Gwau alitoa bima hizo jana wakati akihutubia kwenye kongamano la wanawake Mkoa wa Singida lililofanyika Ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma ambapo pamoja na mambo mengine walitafakari siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwa madarakani na mafanikio ya wanawake hapa nchini huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Wanawake ni Nguzo ya Maendeleo’ Kazi iendelee.

” Bima hizi  ni  zawadi ya Afya kutoka katika mfuko wa ofisi yangu na nijuhudi za kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan katika kuboresha afya za akina mama kwani bila afya hakuna maendeleo na ili maendeleo yaje na kufanya kazi kwa bidii ni budi kila mtu kuwa na afya njema, hivyo nimeamua kugharamia suala la afya kupitia mfuko wa bima wa CHF kwa wanawake hawa ambao ni sawa na kaya 400 huku wanufaika wakiwa 2400 pamoja na watu wenye uhitaji maalumu“.alisema Gwau.

Alisema bima hiyo itakuwa  ya watu sita kutoka kwenye kila familia ya wanawake hao 400. Gwau alisema mwaka huu ameanza na kaya 400 lakini matarajio yake ni kufikisha kaya 1000 na wanufaika wakiwa zaidi ya 5000 itakuwa vizuri zaidi na anafanya hivyo kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwatumikia watanzania katika sekta ya afya.

Pia Gwau alisema kuanzia kesho atatoa utaratibu kwenda kwenye halmashauri zao ambako anatoka kila mwanamke kwa ajili ya kujisajili ambapo wanatakiwa watu sita yaani baba, mama na watoto wanne walio chini ya umri wa miaka 18.

 Gwau alitumia kongamano hilo kwa ajili ya kuwashukuru wanawake hao kwa kumchagua kwa kura nyingi na kuwaomba ushirikiano ambapo pia alieleza mipango na mwelekeo wake wa kazi za maendeleo mkoani Singida.

Alisema ataanza ziara zake za kikazi katika wilaya zote na kata ili kwa pamoja waweze kutatua kero za wanawake huku vipaumbele vyake vikiwa ni kuwainua wanawake kiuchumi na kuwapatia elimu na mafunzo mbalimbali na kuijenga Jumuiya yao ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT)

Alisema katika masuala ya kuwasaidia wanawake atakuwa akifanya kwa awamu kulingana na atakavyo jaliwa lakini ya kiutendaji yatakuwa wilayani ambapo aliwaomba wamshike mkono, wamuelekeze, wamshauri na kumkoasoa lengo likiwa ni kuijenga Singida.

Aidha Gwau aliwaomba wanawake hao kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ni mwanamke wa kwanza hapa nchini kushika wadhifa huo mkubwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambapo alisema kwa umoja wao wanapaswa kuonesha mshikamano na jinsi walivyo tayari kufanya naye kazi akiwa katika nafasi hiyo na kumuombea kwa Mungu.

Katika hatua nyingine aliwataka wanawake hao kuchangamkia fursa ya kilimo cha alizeti kwa kuwa ndio zao kubwa la biashara mkoani hapa na Serikali imeweka nguvu ya kulilima kwenye  mikoa mitatu ya Singida, Dodoma na Simiyu.

Pia aliwaomba  madiwani wanawake kusimamia na kuwashauri wanawake kuchangamkia mikopo kutoka katika halmashauri zao kwaajili ya kujiletea maendeleo na kuinua uchumi wa mwanamke.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Mkoa wa Singida Alhaji Juma Kilimba ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo alimshukuru Gwau kwa kuandaa kongamano hilo na kuwashukuru wanawake hao kwa kumchagua kuwa mbunge.

Aliwataka wanawake hao kuwa wamoja na kushirikiana kwa kila jambo sambamba na kuimarisha jumuiya yao ili chama hicho kiendelee kuongoza nchi.

Katika kongamano hilo Gwau aliwaalika wataalamu ambao walitoa mada kuhusu masuala ya afya hususani namna ya kujikinga na ugonjwa wa corona na umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)