Pages

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUTUMIA KITUO CHA KIBIASHARA NMB

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker akizungumza



Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SERIKALI mkoani Morogoro imewahimiza Wafanyabiashara wakubwa eneo hilo kukitumia Kituo cha Biashara kilichofunguliwa na Benki ya NMB ili kutambua fursa zilizopo katika kituo hicho pamoja na kuunganishwa na masoko ya ndani na nje hatua itakayo saidia kukuza uchumi wa mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Steven Kebwe alisema hayo wakati akizindua kituo hicho cha kibiashara mkoani Morogoro kilichoanzishwa na Benki ya NMB kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara wa mkoa huo.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, alisema NMB imeamua kuanzisha kituo hicho cha kibiashara baada ya Mkoa wa Morogoro kuwa na fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo shughuli za kilimo, uchimbaji madini na masuala ya kiutalii.

Alisema kuwa NMB kupitia fursa hizo imeona iwasaidia Wafanyabiashara wa Morogoro kwa kuanzishia kituo maalumu ambacho licha ya kupata elimu na kuunganishwa na masoko ya ndani na nje pia watapatiwa huduma anuai za mikopo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker alisema kituo cha Biashara cha Morogoro ni kituo cha kumi nchini na kimeanzishwa mahususi kwa ajili ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro waweze kukuza uchumi wao.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho kumetokana na kuwepo kwa fursa nyingi ikiwemo viwanda vya sukari vya kilombero na Mtibwa pamoja na fursa za uwepo wa migodi ya madini na shughuli za utalii ambapo kama wafanyabiashara watazitumia ipasavyo basi wataweza kukuza uchumi wa mkoa huo.

Mkurugenzi huyo alisema Benki ya NMB imekuwa ikiiunga mkono Serikali katika jitihada zake mbalimbali ikiwemo kusaidia kukusanya kodi zake na sasa, kuelekea uchumi wa viwanda imeamua kuwasaidia Wafanyabiashara kwa kuanzishia kituo chao maalumu ambapo watakutana na maofisa wa Benki hiyo kuweza kupata ushauri wa kibiashara na kuunganishwa na klabu 35 zenye jumla ya wanachama 2000 wenye uzoefu wa biashara na masoko ya ndani na nje ya nchini.

Naye Mkuu wa kitengo cha Biashara NMB Makao makuu, Donatus Richard, alisema Benki hiyo inajivunia kuwaona Wafanyabiashara waliochukua mikopo ya chini lakini leo wamekuwa matajiri wakubwa baada ya kupata ushauri katika vituo tisa vya kibishara vilivyopo katika mikoa mbalimbali na kutaka wafanyabiashara wa Morogoro kuchangamkia fulsa hiyo.

Uzinduzi wa kituo hicho cha kibiashara umekwenda sambamba na Benki hiyo kutoa msaada wa madawati yenye thamani ya sh milioni 10 kwa shule za sekondari za Lupanga na Kilakala zilizopo Manispaa ya Morogoro. 

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)