Pages

MFANYABIASHARA AJENGA ZAHANATI YENYE VIFAA VYA KISASA NA KUIKABIDHI SERIKALINI




Mfanyabiashara, Emmanuel Mallya (kushoto) akimkabidhi hati na mkataba wa zahanati EB Zahanati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila kwenye hafla hiyo ya makabidhiano. 

Mfanyabiashara, Emmanuel Mallya (katikati) akimkabidhi hati na mkataba wa zahanati EB, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila kwenye hafla hiyo ya makabidhiano. Kushoto ni mke wa Bw. Mallya, Bi. Marry Mallya akishuhudia makabidhiano hayo.

Makabidhiano ya hati na mkataba wa zahanati EB yakifanyika katika hafla hiyo.

Makabidhiano ya hati na mkataba wa zahanati EB yakifanyika katika hafla hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Moshi

MFANYABIASHARA na mzaliwa wa Kijiji cha Uchau Kaskazini wilaya ya Moshi Vijijini, Emmanuel Mallya, ameikabidhi serikali zahanati ikiwa na vifaa vya kisasa vikiwamo vitanda vya wagonjwa vinavyotumia nishati ya umeme.

Zahanati hiyo inayojukana kwa jina la EB zahanati, imejengwa na mfanyabiashara huyo kwa kutumia nguvu zake mwenyewe bila kuhusisha msaada kutoka Halmashauri ya wilaya ya Moshi wala serikali kuu.

Akizungumza katika hafla fupi ya kuikabidhi zahanati hiyo kwa serikali, mfanyabiashara huyo alisema wazo la kujenga zahanati hiyo lilitokana na kuwepo na changamoto za umbali wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Alisema changamoto hiyo ilipelekea kuwepo na vifo vya watu wengi vilivyochangiwa na umbali wa upatikanaji wa vituo vya afya na kwamba changamoto hizo ndizo zilizomsukama kuona haja ya kujenga zahanati hiyo.

Alitoa wito kwa mamlaka husika kuitunza zahanati hiyo pamoja na vifaa vitakavyotumika katika kuwahudumia wagonjwa huku akitoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitolea katika kuwahudumia wananchi wasio nacho.

“Utajiri unatokana na moyo wa mtu alionao, unaweza ukawa na utajiri na usiwe na moyo wa kuwasaidia wengine, kila mtu amepewa karama na mwenyezi Mungu, muhimu hapa ni namna ya kuzitambua hizo karama,” alisema.

Kabla ya ujenzi huo ulioanza julai mwaka 2013, familia iliyokuwa ikishi mahali ilipojengwa shule hiyo iliridhia ombo la mfanyabaishara huyo la kuachia eneo hilo na kupelekwa kwenye eneo jingine kwa ushirikiano wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Kimasio.

Aliwapongeza familia hiyo kwa kukubali ombi lake la kuliachia eneo hilo na kuongeza kuwa, bila familia hiyo kuridhia kuondoka katika eneo hilo ndoto zake za kujenga zahanati katika eneo hilo zingeishia ukingoni.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Anthony Komu alihimiza usimamizi wa karibu wa zahanati hiyo kwa wale watakakuwa wasimamizi baada ya aliyeijenga kuikabidhi kwa serikali.

"Mhehsimiwa Mkuu wa Wilaya, uzoefu unaonyesha kuwa, miradi mingi inayojengwa na wafadhili imekuwa ikiharibika kutokana na kutokuwepo na usimamizi wa karibu, ni rai yangu kuwa tuitunze zahanati hii isijekuwa mazalia ya popo kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia kwa baadhi ya zahanati na vituo vya afya,” alisema.

Alisema mfanyabiashara huyo ametenda wema wa hali ya juu kwa wananchi wa Wilaya ya Moshi Vijijini na Vunjo kwa ujumla  na kwamba wema huo kamwe hautafutika ndnai ya mioyo ya wananchi hao. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila, alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuchangishana kwa kile kidogo walichonacho ili wanunue gari la wagonjwa ambalo litahudumia zahanati hiyo kwa muda wa saa 24.

Alisema uwepo wa gari la wagonjwa katika zahanati hiyo utarahisisha kuwapeleka wagonjwa katika Hospitali kubwa ikiwamo ya Kibosho, Mawenzi na KCMC kwa wale ambao watahitaji kupewa rufaa.

Alisema maendeleo yanahitaji umoja na mshikamano na kuonya kuwa maendeleo hayana itikadi yoyote ya kisiasa kwani zahanati hiyo itahudumia wananchi wote bila kujali huyu ni wa chama gani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kippi Warioba alipongeza moyo ulioonyeshwa na mfanyabiashara huyo wa kusaidia watu wenye mahitaji. Pia alitoa wito kwa serikali ya kijiji hicho kuanza mazungumzo na wananchi wanaoishi karibu na zahanati hiyo kuachia maeneo yao ili zahanati hiyo ipanuliwe na kufika hadhi ya kituo cha Afya.

Alitoa wito kwa kila mtu kuchangia chochote alichonacho ndani ya jamii na si lazima iwe pesa na kuwapongeza walioachia eneo ilipojengwa zahanati hiyo wametoa mchango mkubwa sana kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)