Pages

KIVULINI YAADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINA UKATILI WA KIJINSIA NA WATOTO KWA KUFANYA MDAHALO WILAYANI KISHAPU


Shirika la Kivulini linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto leo Ijumaa Disemba 8,2017 limeadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto kwa kukutanisha wadau wa haki za wanawake na watoto katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kwa ajili ya kujadili namna ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Mgeni rasmi katika mdahalo huo uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu alikuwa mkuu wa polisi wilaya ya Kishapu, SP Emmanuel Galiyamoshi.

Mdahalo huo uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya ukatili wa kijinsia na watoto umehudhuriwa na maafisa maendeleo,afya,ustawi wa jamii,elimu,watendaji wa kata na vijiji,mratibu wa mama na watoto, polisi,viongozi wa dini,polisi na jeshi la jadi sungusungu.

Akifungua mdahalo huo, mkuu wa polisi wilaya ya Kishapu SP Emmanuel Galiyamoshi alisema ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wadau wote hawana budi kuungana pamoja na kila mmoja akitimiza wajibu wake.

“Ukatili dhidi ya wanawake na watoto upo,ili kuumaliza lazima kila mdau atomize wajibu wake,elimu itolewe,kesi zipelekwe mahakamani na wahusika watoe ushahidi,kupitia dawati letu la jinsia na watoto tumejipanga vyema kusaidia watu wote wanaofanyiwa vitendo vya kikatili”,alisema.

Galiyamoshi alilipongeza shirika la Kivulini kwa kutetea haki za wanawake na watoto huku akiliomba kutanua huduma zao na kusaidia pia wanaume ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili katika familia zao.

Naye Afisa mwandamizi wa mradi wa usawa wa kijinsia kujenga uwezo kiuchumi kwa wanawake na vijana kutoka shirika la Kivulini Bi. Eunice Mayengela alisema shirika hilo limeamua kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto wilayani Kishapu ili kuangalia hali halisi ya masuala ya ukatili wilayani humo.

“Maadhimisho haya ya siku 16 za kupinga ukatili kufanyika kila mwaka ambapo wanaharakati kote duniani huungana kwa pamoja kupinga ukatili na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Ukatili dhidi ya wanawake haumuachi mtu salama,chukua hatua’ ",aliongeza.

Mayengela alisema takwimu zinaonesha kuwa kati ya wanawake 10 waliofanyiwa ukatili,watatu pekee wanatafuta kwa kutoa taarifa polisi.

“Asilimia 54 ya wanawake wanaofanyiwa ukatili wanatafuta msaada kwenye familia na asilimia 9 pekee wanatafuta msaada polisi”,aliongeza Mayengela.

Wakichangia hoja katika mdahalo huo,wadau walisema ili wahanga wa ukatili wa kijinsia waweze kusaidiwa ndani ya saa 72,ni vyema jamii ikapewa elimu kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa kwenye vituo vya polisi na ofisi za kata matukio yanapotokea.

Aidha waliomba mazingira ya kutolea taarifa kuwa rafiki kwani vitendo hivyo ni vya aibu na watu wengi wamekuwa wakihofu kuwa wakienda baadhi yao huombwa fedha ili wapewe huduma. 

Pia walishauri serikali za mitaa kuwa na ajenda ya kuduma kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia lakini pia kutunga sheria ndogo ndogo za masuala ya kijinsia. 

Walizitaja sababu zinazosababisha ukatili dhidi ya wanawake na watoto kuwa ni pamoja na umaskini,ukosefu wa elimu,kukosa hofu ya mungu lakini pia wazazi kutotimiza wajibu kwa watoto wao.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MDAHALO HUO
Mgeni rasmi Mkuu wa Polisi wilaya ya Kishapu SP Emmanuel Galiyamoshi akifungua mdahalo wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto katika wilaya ya Kishapu leo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa Polisi wilaya ya Kishapu SP Emmanuel Galiyamoshi akisisitiza umuhimu wa wadau wote kushirikiana katika kupinga ukatili wa kijinsia
Afisa mwandamizi wa mradi wa usawa wa kijinsia kujenga uwezo kiuchumi kwa wanawake na vijana kutoka shirika la Kivulini Bi. Eunice Mayengela akielezea historia ya shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1999 lakini pia malengo ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto duniani ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10.
Bi. Eunice Mayengela alisema maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili kufanyika kila mwaka kwa lengo la wanaharakati kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto ili familia na jamii ziishi salama.
Afisa Maendeleo ya jamii wilaya ya Kishapu,Joseph Swalala akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku 16 za ukatili wa kijinsia wilayani Kishapu yaliyoandaliwa na shirika la Kivulini.
Afisa miradi shirika la Kivulini,Glory Mlaki akitoa mwongozo wa mdahalo kujadili masuala mbalimbali ya ukatili wa kijinsia. 
Afisa mtendaji wa kijiji cha Wizunza Boniface Maganga akichangia mada kwanini wanawake wazee ndiyo wanaongoza kuuawa kwa imani za kishirikina. Alisema wanawake wengi hawana siri kuhusu mambo wanayoyafanya ndiyo maana wanaonekana kuwa ndiyo wachawi matokeo yake wanafanyiwa ukatili.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Shagihilu,Nicholaus Benard akichangia hoja wakati wa mdahalo huo ambapo alisema vikongwe wamekuwa wakiuawa kutokana na wananchi kuamini sana waganga wa kienyeji ambao miongoni mwao hawana hata leseni.
Sheikh Adamu Njiku akichangia hoja wakati wa mdahalo huo.Alisema vikongwe wamekuwa wakiuawa kutokana na watu katika jamii kutokuwa na dini hivyo kukosa hofu ya Mungu matokeo yake wanaamini katika uchawi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nhobola, Mohamed Shamte akichangia hoja kuhusu mauaji ya vikongwe. Alisema wachawi wengi ni wanaume lakini kutokana na kwamba udhaifu na ukosefu wa elimu kwa wanawake ndiyo maana wanaonekana kuwa wao ndiyo washirikina zaidi matokeo yake wanafanyiwa ukatili.
Kushoto ni afisa mwandamizi wa mradi wa usawa wa kijinsia kujenga uwezo kiuchumi kwa wanawake na vijana kutoka shirika la Kivulini Vaileth Elisa na afisa miradi wa shirika la Kivulini,Glory Mlaki wakiandika dondoo muhimu wakati wa mdahalo huo
Afisa vijana kutoka halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Alen Mjindo akichangia hoja ukumbini ambapo alisema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa elimu pamoja na mila na desturi.
Afisa ustawi wa jamii Mwajuma Abeid akichangia hoja wakati wa mdahalo huo
Kaimu afisa elimu msingi halmashauri ya Kishapu,Queen Sibonike akichangia hoja wakati wa mdahalo huo
Mchungaji John Kingu kutoka kanisa la EAGT Maendeleo Kishapu akisisitiza umuhimu wa kuhubiri elimu katika jamii ili kuondokana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto
Afisa mtendaji kata ya Ukenyenge Chief Ng'ombe akichangia hoja wakati wa mdahalo huo.Alisema matukio ya mimba na ndoa za utotoni yanasababishwa na wazazi kutokuwa karibu na watoto wao.
Askari polisi kutoka jeshi la polisi wilaya ya Kishapu Sarah Mwepe akichangia hoja wakati wa mdahalo huo
Afisa maendeleo ya jamii Neema Mwaifuge akichangia hoja wakati wa mdahalo huo ambapo alisema vitendo vya mimba za utotoni vinachangiwa na mahusiano mabaya baina ya watoto na wazazi lakini pia walimu na wanafunzi wao.
Askari polisi Grace Samson kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Kishapu akizungumza katika mdahalo huo ambapo alisema kesi nyingi za ukatili dhidi ya watoto zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya maafisa watendaji na mahakimu katika mahakama kwa kuchelewesha kesi hizo.
Muuguzi wa afya ya jamii Dinah Nkwabi akichangia hoja wakati wa madahalo huo.
Picha ya pamoja washiriki wa mdahalo huo.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)