Pages

Wakazi wa Bukoba kunufaika na tawi la NMB Kaitaba

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu -Salum Mustafa Kijuu (kati kati) akizindua rasmi tawi jipya la NMB Kaitaba lililopo Manispaa ya Bukoba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja inayoadhimishwa na benki ya NMB Bank PLC. Kutoka Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa NMB Bank PLC-Bi Ineke Bussemaker pamoja na Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa NMB Bw. Abdulmajid Nsekela wakishuhudia uzinduzi huo.


WANANCHI wa Mkoa wa Kagera wameshauriwa kutumia fursa ya uwepo wa benki ya NMB Bank PLC kujiinua kiuchumi kwa kutumia huduma zao ikiwamo mikopo, kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali(Mstaafu)- Salum Kijuu, wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la NMB Kaitaba lililopo katika Manispaa ya Bukoba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, ambayo huadhimishwa mwezi Oktoba kila mwaka.

Kijuu alisema kuwa, serikali ya awamu ya tano imeweka mikakati mizuri ya kupunguza umaskini kwa wananchi wake kwa kutumia fursa zilizopo, na kuwa ndiyo maana imekuwa ikiunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali wa maendeleo, zikiwamo taasisi za fedha kama vile benki ya NMB.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza NMB Bank PLC kwa kuendelea kubuni huduma mpya na kufungua matawi mapya kwa lengo la kuhakikisha huduma zinakuwa karibu na wananchi, ili kuwaondolea adha ya kufuata huduma hizo mbali na makazi yao.

“Napenda kuwapa changamoto kwa ajili ya kusaidia kuendeleza na kukuza uchumi na ajira kwa wananchi, kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wakazi wa vitongoji vyote vya mkoa wa Kagera” alisema Kijuu.

Alisema kuwa, kuwapo kwa huduma za kibenki ni kichocheo madhubuti cha maendeleo ya uchumi, maana sekta ya fedha ndiyo inawezesha shughuli zote za uchumi kama kuwekeza, malipo ya kibiashara na ya binafsi, kuweka amana na mikopo binafsi na mikopo ile ya biashara.

Kwa upande wake Mkurugenziwa NMB Bank PLC Bi. Ineke Bussemaker alisema kuwa Bukoba ni mji unaoendelea kukua kiuchumi, hivyo unahitaji upanuzi wa huduma za kifedha, na kuwa ndiyo maana wamekubali maombi ya wananchi ya kuongezewa tawi jingine la benki.

“Kufunguliwa kwa tawi hili la NMB Kaitaba siyo kwamba tawi jingine lililoko hapa Bukoba tunalifunga, nalo litaendelea kufanya kazi maana tunapanua huduma ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hii pia itasaidia uokoa muda ambao wananchi wamekuwa wakiupoteza kwa kukaa benki wa muda mrefu kusubiria huduma,” alisema.

Aidha, alisema kuwa, mbali na kufungua matawi katika maeneo mbalimbali, pia NMB anazidi kuanzisha huduma mbadala ikiwamo kuweka mawakala, ilikuwezesha kuwa karibu zaidi na wateja, na kuwa kwa sasa wanamawakala zaidi ya 3,500 nchi nzima.

“Tulikuwa na matawi 209 tukiongeza na hili yametimia 210, mawakala wameongezeka sasa ni zaidi ya 3,800, lakini pia tuna mashine za kutolea fedha (ATM) zaidi ya 700 nchi nzima, na tutaendelea kuboresha huduma zaidi kwa ajili ya wateja wetu,”alisema.

Naye mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB BANK PLC- Protase Tehingisa, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Kagera ambao tayari wamenufaika na huduma za benki hiyo ikiwamo mikopo, kuwahamasisha watu wengine kujiunga na benki hiyo, ili nao waweze kunufaika na kujiinua kiuchumi kupitia NMB. Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu -Salum Mustafa Kijuu akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa NMB Bank PLC-Bi Ineke Bussemaker kwa uzinduzi wa tawi jipya la NMB Kaitaba lililopo Manispaa ya Bukoba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja inayoadhimishwa na benki ya NMB Bank PLC. Akishuhudia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Biashara Bw. Donatus Richard

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)