Pages

TGNP yatoa mafunzo kwa wanawake wafanyabiashara mipakani

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wanawake wafanya biashara wa mipakani na wadau wengine kuhakikisha masuala ya jinsia yanaingizwa katika michakato ya biashara za mipakani. Mafunzo hayo yameandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia (GTI) na AWDF Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi (kushoto) akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wanawake wafanya biashara wa mipakani na wadau wengine kuhakikisha masuala ya jinsia yanaingizwa katika michakato ya biashara za mipakani. Mafunzo hayo yameandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia (GTI) na AWDF. Kulia ni mtaalamu mshauri wa masuala ya kijinsia, Sultan Mhina akishiriki katika mkutano huo wa mafunzo. Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi (kushoto) akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wanawake wafanya biashara wa mipakani na wadau wengine kuhakikisha masuala ya jinsia yanaingizwa katika michakato ya biashara za mipakani.

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia (GTI) na AWDF leo imetoa mafunzo ya siku tatu kuhakikisha masuala ya jinsia yanaingizwa katika michakato ya biashara za mipakani kwa wanawake wafanya biashara wa mipakani.

Akizungumzia mafunzo hayo leo Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi alisema Mafunzo hayo
Yamekutanisha washiriki zaidi ya 35 wakiwemo maofisa wa Serikali kutoka mipaka tofauti tofauti, Asasi za Kiraia, pamoja na wafanyabiashara wanawake wanaojishughulisha na biashara za mipakani.

Alisema TGNP Mtandao imejikita zaidi katika kuhakikisha kuwa na Tanzania yenye kuheshimu, kuzingatia na kutekeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na makundi mengine yaliyopembezoni. Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ikiwa ni moja ya nguzo kuu katika kumwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika Maendeleo endelevu.

“TGNP, tumekuwa tukishirikiana na wanawake wafanya biashara za mipakani (Women cross border traders) na wadau wake katika kuwajengea uwezo ili kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao za biashara. Hivyo basi, siku hizi tatu za mafunzo nimwendelezo wa kuimarisha uwezo wa washiriki katika uingizaji wa masula ya jinsia katika sera, mipango, bajeti, miundo na michakato yote inayohusu biashara za mipakani,” alisema Bi. Lilian Liundi.

Aidha akifafanua zaidi aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wadau muhimu katika sekta hii ya biashara jinsi ya kuingiza masuala ya jinsia katika michakato ya biashara ili kumwenzesha kushiriki kikamilifu bila vikwazo na hatimaye kuwainia kiuchumi na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.

Vile vile mafunzo yatawawezesha wanawake na washiriki kwa ujumla kuwa na uelewa wa kanuni za Afrika Mashariki zinazohusu biashara za mipakani na kuboresha huduma za ufikiwaji masoko katika ngazi ya kanda na kimataifa.

“…Utafiti uliofanywa na kituo cha sera za biashara Afrika (ATPC) unaonyesha kuwa biashara inatoa ajira kwa asilimia 60 ya wanawake katika biashara zifanyikazo katika nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara, ambapo asilimia kati ya 70 na 80 ya wanawake hao wamejikita zaidi katika biashara isiyo rasmi. Vile vile, takwimu za UN women zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 74 ya wafanya biashara za mipakani katika nchi za maziwa makuu ni wanawake,” alisisitiza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TGNP.

Hata hivyo alisema kuwa biashara za mipakani zinakua na kukuza uchumi wa nchi za Afrika Mashariki, biashara hizo hizo ambazo zitakuwa zikifanyika kwa kiwango kidogo na kwa njia isiyorasmi zitashamiri. Ilhali serikali za Afrika Mashariki bado hazijachukua hatua madhubuti katika kuunda sera na mifumo maalumu yenye kuwalenga wafanya biashara wadogo ambayo itawasaidia kukuwa na kunufaika sawa na wafanya biashara wakubwa katika michakato ya kibiashara kikanda.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)