Pages

Benki ya Standard Chartered yadhamini Kongamano la Wanawake na Fedha kimataifa

Ofisa Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered, Sanjay Ruhani (Kushoto) akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam juu ya benki hiyo kudhamini Kongamano la kimataifa la Wanawake na Fedha linalotarajia kufanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, nchini Tanzania. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Women's World Banking, Tom Jones pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Biashara kati ya Mabenki, Bi. Heidi Toribio (katikati). Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Women's World Banking, Tom Jones akizungumza katika mkutano na wanahabari kuzungumzia udhamini Kongamano la kimataifa la Wanawake na Fedha uliotolewa na Benki ya Standard Chartered. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Biashara kati ya Mabenki, Bi. Heidi Toribio akishuhudia.

BENKI ya Standard Chartered imetangaza kudhamini Kongamano la kimataifa la Wanawake na Fedha linalotarajia kufanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, nchini Tanzania. Kongamano hilo la siku mbili linatarajia kukutanisha pamoja wanawake viongozi katika fani mbalimbali, zikiwemo mabenki, teknolojia, wafanyabiashara, mashirika ya umma na binafsi.

Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani alisema kongamano hilo linatarajiwa kuzinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Bi. Samia Suluhu Hassan. Akizungumzia udhamini huo Bw. Rughani alisema Benki ya Standard Chartered imekubali kudhamini mkutano huo ikiwa ni jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi.

"Alisema wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi zao, tumejidhatiti kikamilifu kuwawezesha wanawake kuwa na uhuru wa uchumi na fedha, kupata mitaji na kuwa na elimu ya mambo ya fedha na uchumi. Sisi kama benki tutaendelea kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kuchangia maendeleo ya nchi yetu," alisema Ofisa Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered, Bw. Rughani.

Aidha aliongeza kuwa, Benki ya Standard Chartered inaamini kongamano hilo litaleta mageuzi ya kiuchumi na kuwawezesha wanawake kuwa wadau wakuu katika kuleta maendeleo ya nchi ya Tanzania na nchi anuai zitakazo shiriki kwenye kongamano.

Aidha kongamano hilo linalotarajia kushirikisha wanawake zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali duniani na wakiwemo wanachama wa shirika la Women's World Banking kutoka mataifa 32. "Siku mbili zijazo zitasaidia kuleta mageuzi hasa katika kuwawezesha wanawake kuwa wadau wakuu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi Tanzania na katika nchi zingine....," alisisitiza Bw. Rughani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Women's World Banking, Tom Jones alisema uwepo wa washiriki wanawake kutoka katika sekta mbalimbali watakaoshiriki Kongamano hilo ni ushaidi tosha kuona namna wanawake walivyo na kiu ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika nchi zao.

Benki ya Standard Chartered Tanzania inaadhimisha miaka 100 tangu ifungue biashara zake nchini Tanzania na katika kuadhimisha sherehe hizo Mwezi Machi mwaka huu iliwaalika viongozi 40 kutoka mabara ya Afrika na Asia na kuzungumza nao kwa kina namna ya kukuza uchumi wa nchi zao kupitia fursa anuai zilizopo. Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Biashara kati ya Mabenki, Bi. Heidi Toribio (kulia) akizungumza katika mkutano na wanahabari kuzungumzia udhamini huo. Kushoto ni Ofisa Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani akifuatilia.
Sehemu ya wanahabari wakiwa katika mkutano kuzungumzia udhamini Kongamano la kimataifa la Wanawake na Fedha uliotolewa na Benki ya Standard Chartered.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)