Pages

Wanachama TEN/MET watoa hoja nzito kwa Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii

Mwanachama wa TEN/MET toka taasisi ya FAWETZ, Bi. Neema Katundu (kulia) akiwasilisha hoja mbalimbali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii jana mjini Dodoma juu ya maboresho katika sekta ya elimu. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba (kushoto) na katibu wake kulia wakizungumza na wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) jana mjini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na kuwasilisha hoja mbalimbali za kufanyiwa kazi na Serikali kupitia sekta ya elimu lengo likiwa ni kuhakikisha elimu bora inapatikana nchini Tanzania.

Akiwasilisha hoja hizo mahususi 14 mjini Dodoma, Mwanachama wa TEN/MET toka taasisi ya FAWETZ, Bi. Neema Katundu alisema hii ni mara ya pili kuwasilisha hoja na lengo la msingi ni kuitaka serikali kuingiza katika utekelezaji.

Bi. Katundu alisema wanaikumbusha Serikali kuhakikisha inatenga hadi asilimia 20 ya bajeti ya taifa kwenye sekta ya elimu na pia kuwekeza zaidi katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato na matumizi mabaya ya fedha toka mapato ya ndani ili iweze kutumika uboreshaji elimu ya msingi nchini.

Alisema hoja zingine walizowasilisha Serikalini ni pamoja na kutaka utoaji wa ruzuku shuleni hali halisi ya mahitaji ya sasa na kuhakikisha mchakato wa kuanzishwa kwa Bodi ya Taaluma ya uwalimu itakayoongeza tija na kulinda maslahi ya walimu katika sekta hiyo.

Aidha, hoja zingine walizowasilisha kwa kamati hiyo ni kutaka kuimarishwa kwa idara ya kudhibiti ubora (ukaguzi) na ipewe mamlaka na vitendea kazi kiuhalisia ili iweze kufanya kazi yake kiufasaha, uzingatiwaji wa haki za watoto na pia kuundwa kwa chombo maalumu cha usimamizi, utungaji na utekelezaji wa sera ya elimu.

Walishauri Serikali kutoa kipaumbele cha bajeti kwa sekta ya elimu kama ilivyofanywa kwa sekta ya miundombinu miaka miwili iliyopita, Serikali za mitaa kutunga na kusimamia sheria ndogondogo zitakazo wabana wazazi wanaowanyima watoto haki ya elimu, huku wakiomba fedha za mikopo ya elimu ya juu kutenganishwa na fedha za maendeleo ya wizara ya elimu.

Kilio kingine kilichofikishwa katika kamati hiyo ya Bunge ya Huduma za Jamii, ni pamoja na kutaka kuhimarishwa kwa kamati za shule, kuhamashishwa kwa wazazi kuchangia maendeleo ya watoto wao kielimu, kuingiza kipengele cha elimu ya mlipa kodi katika mitaala ya elimu na pia serikali kupunguza vigezo katika upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu na kuongeza bajeti eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba aliwashukuru wanachama wa TEN/MET kwa kuwa wazalendo kuipigania elimu nchini, hivyo kuwataka watoe muda kwa kamati hiyo ili iweze kuzifanyia kazi hoja hizo kwa maendeleo ya taifa. Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ikiwa katika kikao na Wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET). Afisa Programu toka HakiElimu, Makuba Mwemezi (kushoto) ambaye pia ni mwanachama wa TEN/MET akichangia hoja katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii. Kikao hicho kikiendelea jana mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)