Pages

SHULE YA GENIUS KINGS YAJIPANGA KUWA SHULE BORA KITAALUMA TANZANIA

 Wanafunzi wa shule ya Genius Kings Nursery and Primary School iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, wakifundishwa somo la kompyuta.
Wanafunzi wa darasa la tano wakimsikiliza kwa makini mwalimu wa taaluma.
 Wanafunzi wa darasa la sita na la saba katika wa shule ya Genius Kings wakiwa katika chumba cha maabara wakijifunza somo la sayansi kwa vitendo.

Wanafunzi wa darasa la sita na la saba katika wa shule ya Genius Kings wakiwa katika chumba cha maabara wakijifunza somo la sayansi kwa vitendo wakitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Shule hiyo Bw. Machage Kisyeri.
Mkurugenzi wa Shule hiyo Bw. Machage Kisyeri akiwa ofisini kwake.

Shule ya awali na ya msingi ya Genius Kings iliyopo Tabata-Segerea jijini Dar es Salaam imejizatiti kuhakikisha inakuwa shule bora na ya mfano kitaaluma ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 10 tangia kuanzishwa kwake.

Akiongea jijini Dar es Salaam kuhusiana na maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambayo yameanza kusherehekewa mapema wiki na kutarajia kumalizika mapema mwezi Desemba mwaka huu,Mkuu wa shule hiyo,Bw.Aloyce Siame,alisema licha ya kwamba mwanzo huwa ni mgumu kwa mradi wowote ule, shule imeweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya elimu na kuweza kuchomoza kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri mkoani Dar es Salaam na kwa ngazi ya kitaifa.

Bw.Siame alisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 shule imeweza kushikilia rekodi ya kufanya vizuri kwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba na la nne kwa kiwango cha juu na kuingia katika shule tano bora wilayani Ilala na shule bora 20 mkoani Dar es Salaam mfululizo hali ambayo imewajengea hari ya kuzidi kufanya vizuri kwa mwaka huu na miaka ijayo.

“Moja ya mtazamo wa shule hii ni kuifanya kuwa shule bora ya mfano inayotoa elimu bora nchini kuanzia shule ya awali na shule ya msingi.Tumejipanga kuhakikisha lengo hili linatimia na tunatoa shukrani kwa serikali,wazazi na wadau wote ambao wameonyesha kutuunga mkono katika kipindi hiki cha awamu ya kwanza ya mwanzo ya miaka 10 na kuwezesha mafanikio haya kupatikana”.Alisema.

Aliongeza kuwa mbali na kufundisha masomo ya darasani kwa nadharia na vitendo na ujuzi wa kutumia kompyuta kupata maarifa ya kielimu shule inatoa mafunzo ya kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwa wabunifu,Sanaa,michezo mbalimbali,kuwajengea uwezo wa kujiamini kuongea mbele ya hadhara na kufanya mijadala ya kuchambua masuala yanayohusiana na elimu na nyanja nyinginezo hususani masuala yanayoendelea hapa nchini na nje ya nchi bila kusahau kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa shule hiyo,Bw.Machage Kisyeri,alisema anajivunia kwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka 10 na kuahidi kuwa uongozi umejipanga kuhakikisha kitaalamu shule inazidi kupanda zaidi na kuimarisha mafunzo ya shule ya awali kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi wadogo kupata elimu bora zaidi kwa kutumia nyenzo mbalimbali za kisasa,kuimarisha miundombinu na kuongeza walimu wenye ujuzi mkubwa wa kufundisha madarasa ya chini ya watoto wadogo kwa kuwa msingi mzuri kielimu ndio unawezesha watoto kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.

Kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo alisema kuwa zipo changamoto za kawaida kinachotakiwa ni ushirikiano baina ya wazazi,walimu,na wadau wanaosimamia elimu ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana na elimu ya Tanzania inazidi kupanda “Walimu wakiwezeshwa vizuri na kupewa ushirikiano wa kutosha naamini shule nyingi za Tanzania zitatoa elimu bora kwa kuwa tunao walimu wengi wazuri ambao wakitumiwa ipasavyo tutasonga mbele”.Alisema.

Akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake,Mwanafunzi John Magongo anayesoma darasa la saba shuleni hapa alisema kuwa wanawezeshwa kupatiwa elimu ya kuwajengea uwezo wa kufanya vizuri kitaaluma ,nidhamu, kujiamini na kujituma kiasi kwamba popote watakapokwenda wanaamini watazidi kung’ara kutokana na elimu inayotolewa shuleni hapo.

Shule ya Genius Kings ilianzishwa mnamo mwaka 2008 na vijana wa kitanzania wenye taaluma mbalimbali ambapo waliweza kupata walimu wazuri ambao kwa kipindi chote hiki wamewezesha kupatikana mafanikio ya shule kuwanoa wanafunzi vizuri kitaaluma na kuwa miongoni mwa shule bora mkoani Dar es Salaam ,pia uwekezaji wa shule hii umewezesha kupunguza tatizo la ajira kwa kuwa mbali na kuajiri walimu imeajiri wafanyakazi katika vitengo vyake mbalimbali vya uendeshaji.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)