Pages

TMA yatoa utabiri wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari leo makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam akitoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari leo makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam akitoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017. Kushoto ni Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Samwel Mbuya pamoja na Mkurugenzi wa Utafiti wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a (kulia).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (kushoto na meza kuu) wakizungumza na waandishi wa habari leo makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam kutoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017.

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi leo ametoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017, huku utabiri huo ukionesha uwezekano mkubwa wa mvua za wastani katika maeneo mengi ya nchi. Dk. Kijazi ameongeza ya kuwa kutakuwa na mtawanyiko hafifu wa mvua na vipindi virefu vya ukavu baadhi ya maeneo katika kipindi cha msimu wa mvua wa Machi hadi Mei, 2017 hususan Nyanda za Juu Kaskazini mashariki na Pwani ya Kaskazini.

Akizungumza na wanahabari leo ofisi za TMA Dar es Salaam, Dk. Kijazi alisema maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, Pwani ya Kaskazini na visiwa vya unguja na Pemba ukanda wa ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, kunatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi Juu ya Wastani.
Kwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini -Mashariki yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani, huku mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Pwani ya Kaskazini zinatarajiwa kuungana na mvua za msimu kabla ya kusambaa katika maeneo mengine wiki 1-2 ya mwezi Machi.

"..Vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki. Matukio ya vimbunga katika bahari ya Hindi yanatarajia kuchangia katika mwenendo wa msimu wa mvua nchini.
Baadhi ya wanahabari na maofisa wa TMA wakiwa katika mkutano na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi leo makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017.
Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Samwel Mbuya (katikati) akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari leo makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Kijazi pamoja na Mkurugenzi wa Utafiti wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a (kulia).

Kwa upande wa Kanda ya Ziwa Victoria kwenye mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu pamoja na Shinyanga mvua zinazoendelea baadhi ya maeneo ya Kagera na Mwanza zinatarajia kuungana na mvua za msimu na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya 1-2 ya mwezi Machi, 2017.

Mkurugenzi huyo mkuu wa TMA, alisema maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani ya Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinazoendelea kwa sasa (kwa Dar/Pwani) zinatarajia kuungana na mvua za msimu na kusambaa katika maeneo mengine ya Tanga, Visiwa vya Unguja na Pemba na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro wiki ya 1 na 2 ya mwezi Machi.
Alisema kwa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara mvua katika maeneo haya zinatarajia kuanza katika wiki 1-2 ya Mwezi Machi, 2017 huku zikiwa za wastani hadi chini ya wastani. Pia vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko hafifu wa mvua unatarajia katika baadhi ya maeneo.

Maeneo yanayopata mvua za msimu mmoja, Magharibi mwa nchi, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini -Magharibi kusini mwa nchini na pwani ya Kusini; kunatarajiwa kuwa na mvua za wastani katika maeneo mengi na juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Njombe, Songwe, Ruvuma, Mtwara na Lindi pamoja na maeneo ya Morogoro Kusini Mahenge.

Kanda ya Magharibi Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa kwa ujumla inataraji kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani na zitaishia Mwezi wa Aprili. Maeneo ya Kanda ya Kati mikoa ya Singida na Dodoma mvua za msimu zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi huku zikitegemewa kuishia wiki ya 2-3 ya mwezi Aprili, 2017.
Baadhi ya wanahabari na maofisa wa TMA wakiwa katika mkutano na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi leo makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2017.

Maeneo ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, mikoa ya Mbeya, Songwe, Irinda, Njombe na Morogoro Kusini mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, Huku maeneo ya Kusini na Pwani ya Kusini, mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi isipokuwa maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Lindi yatakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Aidha akitoa ushauri katika sekta ya afya, Dk. Kijazi alisema huenda kukawa na uhaba wa maji salama kwa shughuli za binadamu ikiwemo usafi, hivyo wananchi wanashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kuzuia milipuko ya magonjwa. Hata hivyo amewashauri wadau wa sekta ya afya pamoja na umma kuchukua hatua kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)