Pages

Frankie Matson:Mbunifu wa mitindo ya mavazi ambaye ameibukia kwenye muziki

 Baadhi ya washabiki waliohudhuria onyesho la Frankie wakifuatilia muziki na kupata burudani
 Frankie  (wa tatu kutoka kushoto) akicheza na baadhi ya wanamuziki wenzake anaoshirikiana nao

Frankie akiimba kwa hisia kali katika moja ya onyesho alilolifanya hivi karibuni
Frankie (wa nne kutoka kushoto) akiwa na wanamuziki wenzake chipukizi

-Ndoto yake ni kuwa mwanamuziki  na mbunifu wa mavazi wa kimataifa
-Aipongeza TBL Group kwa kuwezesha wasanii chipukizi
Mbunifu wa mavazi na mitindo  kupitia chapa ya ‘Mkali’,Frankie Matson (24), ameibukia kwenye muziki ambapo hivi sasa ameungana na wasanii wenzake chipukizi wameanza kutumbuiza kwenye kumbi za starehe jijini Dar es Salaam na wamejipanga pia kutumbuiza kwenye matukio ya makampuni,mashirika na matamasha mbalimbali na kuingiza vibao vyao sokoni katika siku za karibuni.
Akiongelea kujitosa kwake kwenye muziki ,Frankie,alisema ana kipaji na ana malengo makubwa ya kukuza muziki wa Tanzania ili uweze kutamba  katika ngazi ya kimataifa.Alieleza kuwa kazi ya muziki ataifanya vizuri wakati huohuo akiendelea na  ubunifu wa mitindo ya mavazi ambayo ndiyo inamuwezesha kuendesha maisha yake.
Anasema Tanzania ina wanamuziki wengi wenye vipaji lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwafanya wasifike mbali zaidi ya muziki wao kusikika hapa nchini na wengi wao kutamba kwa muda mfupi na kupotea katika ulimwengu wa muziki huku wakiwa hawajanufaika na kitu chochote kimaisha.
“Bahati nzuri hivi sasa kuna wanamuziki wengi chipukizi ambao kazi zao zikiingia sokoni zinapokelewa vizuri na sio soko la hapa nchini bali hata nje ya nchi,kinachotakiwa ni ubunifu zaidi,kujiamini na kushirikiana katika kazi badala ya kupigana vita”.Alisema. Frankie.
Frankie ambaye mbali na kuimba anapiga ala mbalimbali za muziki alisema kuwa anaamini kuwa tasnia ya muziki ikisimamiwa ipasavyo na vyombo husika na wanamuziki kuiheshimu inazo nafasi nyingi za ajira kwa vijana na kuwa hapa nchini kuna vipaji vingi ambavyo vinapotea bila kutumika.
Alipoulizwa mikakati yake anayoingia nayo katika uwanja wa muziki alisema nyimbo zake zaidi zitalenga kuelimisha na vile vile kuiburudisha jamii na hataishia kutoa nyimbo kwa lugha ya kingereza bali atatoa nyimbo zilizoimbwa kwa lugha ya Kiswahili na ana imani kubwa zitafanya vizuri katika soko  la ndani na la kimataifa kwa kuwa anaamini kuwa muziki unaweza kuburudisha jamii yoyote hata kama wanaoburudishwa hawaelewi lugha iliyotumiwa katika muziki husika.
“Duniani kwa sasa hivi kuna ushindani  mkali katika nyanja zote. Sisi kama wanamuziki wa Tanzania tunapaswa kuhakikisha tunatoa muziki wa viwango vya juu na kuhakikisha tunalenga zaidi katika masoko ya nje kama wenzetu wanavyofanya kusambaza kazi zao. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kujiamini,kufanya vizuri ili tuweze kutangaza Tanzania,kutangaza lugha ya Kiswahili na kupata mapato ya kutosha kutokana na kazi ya muziki ambayo ikifanywa kitaalamu inalipa kwa kiasi kikubwa”.anasema.
Frankie ambaye anafanya kazi zake kwa kujiamini kutokana na kuwa na utaalamu wa biashara na masoko  amesema hadi kufikia katikati ya mwaka huu atatoa albamu yake ya kwanza  na anadai kuwa ndio itamfungulia njia ya kuingia rasmi katika uwanja wa muziki .
 Mwanamuziki anayemvutia zaidi kwa hapa nchini amemtaja kuwa ni Lady Jay Dee. Amekitaja kibao cha mwanamuziki huyo kinachokwenda kwa jina la “Machozi‘’kuwa kina ujumbe mkali kwa jamii.Pia aliwataja wanamuziki wengine maarufu nchini  kama vile Vanessa Mdee,Diamond ,Ali Kiba,Darasa na wengio wengi kuwa wanajitahidi kufanya vizuri na kazi zao zinazidi kuitangaza Tanzania katika ulimwengu wa muziki.
Frankie ambaye ni msomi mwenye shahada ya Biashara upande wa masoko kutoka Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam, ametoa wito kwa vijana wenzake kusisimua vipaji vyao na kujiamini kufanikisha ndoto zao na alishukuru makampuni ambayo yamekuwa na programu za kulea na kukuza vipaji kwa kuwa zinawatia moyo  na kuwawezesha kufanya vizuri zaidi.

 Aliishukuru kampuni ya TBL Group kwa kumuunga mkono wakati  anaanza onyesho lake la kwanza kwa kuwa pamoja na uchanga wake aliweza kuuza tiketi za kutosha kufanikisha onyesho  hilo na baadhi ya wafanyakazi  wa kampuni hiyo waliweza kuhudhuria na kumuunga mkono.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)