Pages

Bayport yatoa kompyuta nne kwa shule za Msingi Dodoma Mjini


Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mvunde (kulia) akipokea msaada wa Kompyuta Nne kwa Meneja Masoko na Mawasiliano wa Taasisi ya Kifedha Bayport Tanzania, Ngula Cheyo mjini Dodoma leo asubuhi. Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kati wa taasisi hiyo,


Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kati wa taasisi hiyo, Christopher Kihwele.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services, jana imemkabidhi kompyuta nne Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Mheshimiwa Anthon Mavunde kwa ajili ya shule za Msingi za Majengo, Chigonge, Mahomanyika na Uhuru zilizopo mjini Dodoma.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Majengo, wakinyoosha mikono juu katika tukio la kukabidhiwa kompyuta nne za Bayport Financial Services, zikipokewa na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.


Makabidhiano hayo yalifanyika katika shule ya Msingi Majengo, ambapo kompyuta hizo zina lengo la kuongeza kiwango cha elimu mkoani Dodoma. Akizungumza leo mjini Dodoma, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba msaada huo wa kompyuta umetokana na dhamira yao ya kusaidia jamii kwenye sekta ya elimu kama njia ya kuikomboa jamii. Alisema kwamba si mara ya kwanza kusaidia sekta ya elimu kutokana na kujitokeza mara  kadhaa kujenga madarasa, kununua thamani za shule pamoja na kudhamini mikopo ya  elimu ya juu na vitabu.

Baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Majengo, wakisoma shairi mahususi kwa ajili ya Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana, Anthony Mavunde wakati anakabidhiwa kompyuta nne kutoka kwenye taasisi ya Bayport  Financial Services.


“Bayport tuna lengo la kuikwamua jamii katika maendeleo kwa kuhakikisha kwamba tunakuza kiwango cha elimu, hivyo kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuhamia Dodoma, tumeamua kutoa kompyuta nne kwa kuboresha miundo mbinu ya elimu ili nchi yetu isonge mbele.

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo akizungumza jambo katika makabidhiano ya kompyuta nne kwa Naibu Waziri, wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.


Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mvunde (kulia) akizungumza kabla ya kukabidhiwa msaada wa kompyuta Nne kutoka Taasisi ya Kifedha ya Bayport Tanzania mjini Dodoma jana.

“Hatujaanza leo kusaidia jamii, ukizingatia kwamba kompyuta hizi nne zenye thamani ya Sh Milioni 10 kwa shule za msingi mjini Dodoma ni tofauti na zile 205 tunazotoa kwa serikali,” Alisema Cheyo.

Akipokea kompyuta hizo, Naibu Waziri aliwashukuru Bayport kwa msaada wao, akisema umekuja wakati muafaka na kuamini kuwa utasaidia kukuza kiwango cha elimu katika Mkoa wa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya Tanzania.

“Tunawashukuru Bayport kwa msaada wenu, wananchi wa Dodoma tumeupokea kwa furaha kwa sababu unatufanya tupige hatua kubwa kukuza elimu, ukizingatia kuwa mipango yangu kama mbunge ni kusambaza kompyuta kwa kila shule ili wanafunzi wetu wafanye mitihani kila mwisho wa wiki kama sehemu yao ya kujiandaa na mitihani ya Taifa,” Alisema Mavunde.

Naye Afisa Elimu wa Manispaa ya Dodoma, Scolastica Kapinga, alisema juhudi zao za kukuza kiwango cha elimu utafanikiwa kwa kupokea kompyuta hizo zilizotolewa na Bayport kwa juhudi kubwa za mbunge wao.

Bayport ni taasisi inayotoa mikopo ya fedha na bidhaa, ikiwamo ardhi yenye hati, ambapo pia imekuwa ikijitokeza mara kadhaa kusaidia mambo ya kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali kama sehemu ya kurudisha faida kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)