Pages

Hivi ndivyo Mkurugenzi wa Jamii forums alivyofikishwa Mahakamani leo

Na  Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Dar es Salaam.
Mwanzilishi-mwenza na Mkurugenzi wa Kampuni  ya Jamii Media, Maxence Melo Mubyazi (40), leo amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana katika kesi moja kati ya tatu zinazomkabili ikiwamo ya kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuendesha mtandao wa Jamii Forum bila usajili.

Mapema leo asubuhi mshtakiwa huyo ambaye pia ni
mfanyabiashara  na bosi wa mtandao huo, alifikishwa katika viunga vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  jijini Dar es Salaam.


Alipandishwa kizimbani saa 3:29 kusomewa mashtaka katika kesi yake
ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
 
Upande wa mashtaka  uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mohamed Salum akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Yohanes
Kalungula.
 

Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa
akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media Ltd, inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums, akiwa anajua polisi wanafanya uchunguzi kutokana na taarifa zilizochapishwa katika mtandao huo, alishindwa kutoa taarifa. Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alishindwa kutoa taarifa ambazo ziko chini yake huku akijua ni kosa.
 

Mshtakiwa alikana shtaka hilo, upande wa Jamhuri ulidaia kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na haukuwa na pingamizi la dhamana hivyo uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.  Hakimu Simba alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika au serikalini, watakaotia saini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 10 kila mmoja. 

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo dhidi ya kesi hiyo na imepangwa
kutajwa Desemba 29, mwaka huu. 
Katika kesi ya pili, mshtakiwa alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa. Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Mei 10 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media Ltd, inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums, huku akijua kwamba polisi wanafanya uchunguzi kuhusu taarifa zilizochapishwa katika mtandao wake, alishindwa kutoa taarifa hizo ambazo ziko chini yake. Mshakiwa alikana shtaka hilo. 

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
unaendelea na haukuwa na pingamizi la dhamana na uliomba tarehe ya kutajwa. Hata hivyo, mshtakiwa katika kesi hii alishindwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kutokuwa na wadhamini na alirudishwa mahabusu hadi Desemba 29, mwaka huu kesi yake itakapotajwa.

Katika kesi ya tatu, mkurugenzi huyo alipandishwa
kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
 
Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti, kati ya Desemba,
mwaka 2011 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, aliendesha mtandao wa kijamii ujulikanao kama Jamiiforums.com bila kuwa na usajili wa kuendesha mtandao huo.
  
Katika shtaka la pili, katika tarehe tofauti, kati ya Januari 26 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums huku akijua kwamba polisi wanafanya uchunguzi kuhusu taarifa zilizochapishwa katika mtandao wake alishindwa kutoa taarifa hizo ambazo ziko chini yake. 

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
  
Hakimu alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na mashahidi wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni Moja kila mmja pamoja na mshtakiwa. Mshtakiwa alitimiza masharti hayo na kesi yake itatajwa Januari 16, mwaka 2017. 
 Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo akiongozwa na Askari Polisi wakati alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam leo, kusomewa mashtaka yanayomkabili.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)