Pages

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUCHANGAMKIA NYUMBA ZA BEI NAFUU ZINAZOJENGWA NA SERIKALI

 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ujenzi  wa Nyumba za Watumishi wa Umma (WHC) Fredy Msemwa (katikati), akitoa taarifa kwa Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki (kushoto), kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa Umma zinazojengwa Gezaulole Kigamboni jijini Dar es Salaam. Waziri Kairuki alikuwa katika ziara ya siku moja kutembelea miradi ya ujenzi ya Taasisi hiyo iliyopo Dar es Salaam. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya WHC, Daud Msangi.
 Mjumbe wa Bodi ya WHC, Daud Msangi akitoa taarifa kwa 
Waziri Kairuki.
 Waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki (kushoto), akizungumza na watendaji wa mradi huo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ujenzi  wa Nyumba za Watumishi wa Umma (WHC) Fredy Msemwa (kushoto), akimuelekeza Waziri Kairuki jinsi ujenzi wa magorofa unavyoendelea katika mradi huo wa Gezaulole. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, Mjumbe wa Bodi ya WHC, Daud Msangi na Kaimu Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Robert Wambura.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki (katikati), akikagua nyumba zinazojengwa na Taasisi ya Ujenzi  wa Nyumba za Watumishi wa Umma (WHC) katika mradi ya Gezaulole Kigamboni Dar es Salaam leo asubuhi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa WHC, Fredy Msemwa na kulia kwake ni Mjumbe wa Bodi ya WHC, Agnes Meena.
 Waziri Kairuki (kushoto), akimuelekeza jambo Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Robert Wambura wakati wa ziara hiyo.
 Wafanyakazi wa WHC, wakijadiliana jambo kwenye ziara hiyo.
 Ukaguzi wa mradi huo ukiendelea.


Msanifu Majengo kutoka Onspace Consult. Co.Ltd, Edmund Kahabuka (kulia), akitoa taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa Magomeni kwa Waziri Kairuki.
 Mwonekano wa ujenzi wa magorofa yanayo jengwa katika mradi huo wa Gezaulole Kigamboni.
 Mwonekano wa nyumba za chini zinazojengwa katika mradi huo.
 Mwonekano wa jengo la ghorofa la mradi huo baada ya kukamilika ujenzi wake.

Na Dotto Mwaibale

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki amewataka watumishi wa Umma kuchangamkia nyumba za bei nafuu zinazojengwa na Serikali ili kuondokana na changamoto ya makazi.

Katika hatua nyingine Kairuki ameiagiza Taasisi ya Ujenzi  wa Nyumba za Watumishi wa Umma (WHC), kuzingatia ujenzi utakaokidhi mahitaji ya watumishi wenye mishahara ya kima cha chini wakiwemo walinzi, wahudumu, madereva na makatibu muhtasi.

Kairuki aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipofanya ziara kwenye mradi wa nyumba za WHC, zilizopo Kigamboni, Magomeni na Bunju jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuangalia ujenzi unavyoendelea.

Alisema asilimia 80 ya watumishi wa serikali wana mishahara midogo hivyo endapo nyumba hizo zitauzwa kwa gharama kubwa hawataweza kuzinunua, na azma ya serikali ni kuwa na nyumba bora zenye gharama nafuu kwa watumishi wake.

"Kwa asilimia 80 ya watumishi wa umma kiwango watakachoweza kumudu kununua nyumba hizo hakiwezi kuzidi sh. milioni 20 kwa miaka 18, Tujitahidi kupunguza gharama kwa kadiri inavyowezekana ili kutoa fursa kwa watumishi wa umma wa kipato cha chini kuweza kupata nyumba za bei nafuu za kuishi" alisema.

Waziri huyo alisema azma ya serikali ni kuhakikisha wanaboresha na kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma ambazo zinatakiwa ziwe sio chini ya nyumba 10,000.

Aliwataka WHC, kuwa na mpango mkakati wa kuweza kujenga nyumba zaidi ya 10,000 kwa mwaka ili kuwafikia watumishi wengi zaidi hasa waliopo vijijini.

Alisema katika manunuzi ya nyumba hizo serikali inaangalia jinsi ya kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ili kumpunguzia mtumishi gharama.

Nyumba hizo zinazojengwa kwa mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Pensheni zitauzwa kulingana na ukubwa wa nyumba husika kwani ile ya chumba kimoja itauzwa kwa sh.milioni 35, vyumba viwili milioni 75 na vyumba vitatu itauzwa sh.milioni 91.

Mkurugenzi Mtendaji wa WHC, Fredy Msemwa alisema katika eneo la Kigamboni lenye ekari 24 wanatarajia kujenga nyumba 790, mradi unaotekelezwa kwa awamu mbili.

Alisema katika nyumba za awamu ya kwanza wapo katika hatua ya umaliziaji ambapo nyumba hizo zinatarajia kukamilia Februari mwakani.

Nyumba hizo pia zinajengwa katika maeneo mbalimbali nchini, ambazo gharama zake ni kati ya sh. milioni 33 mpaka sh. milioni 190 pamoja na VAT.

Mwenyekiti wa Bodi ya WHC, Daud Msangi alielezea changamoto za mradi huo kuwa waliomba nyumba hizo zisiwe na vat, kupata viwanja bure na vya bei rahisi pamoja na serikali kuangalia huduma za maji, umeme na barabara.

Nyumba nyingine zimeanza kujengwa katika mikoa ya Morogoro, Mwanza, Dodoma, Mtwara, Lindi, Mbeya, Shinyanga, Singida na Arusha huku katika baadhi ya mikoa hiyo kukiwa na viwanja vya ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)