Pages

Video: BONGO MOVIE SHINYANGA NA SWAHILI ARTS WAMEKULETEA TAMTHILIA YA VAISI VESA -TAZAMA HAPA SEHEMU YA KWANZA 'WIVU'

Tamthilia ya Vaisi Vesa- sehemu ya kwanza Wivu,itazame chini ya maelezo yote hapo chini
Amani Masuka(kushoto) na Ibrahim Songoro(kulia) wakiwa katika ofisi ya Bongo Movie Shinyanga Jumatano,Novemba 23,2016 wakiendelea na kazi 
Amani Masuka(kushoto) na Ibrahim Songoro(kulia) wakiwa katika ofisi ya Bongo Movie Shinyanga Jumatano,Novemba 23,2016
****
Kundi la sanaa ya uigizaji la Swahili Arts la jijini Arusha na Bongo Movie Shinyanga wameamua kuja upya kwa kuunganisha asasi zao na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha wanaiwakilisha vyema Shinyanga na kuitambulisha tasnia ya filamu mkoa wa Shinyanga. 

Wakizungumza na Malunde1 blog,wamesema sasa wameamua kuja kwa ujio mpya ambao utakuwa bandika bandua kwa kazi zenye ubora na mafunzo na wameanza kwa tamthiliya ya Vaisa Vesa. 

Hatua hiyo imekuja baada ya mwongozaji wa filamu nchini Amani Masuka anayeongoza kundi la sanaa ya uigizaji la Swahili Arts la jijini Arusha na mmliki wa Eden Media Creation,kumaliza tofauti zilizojitokeza mwanzoni mwa mwaka 2015 na Bongo Movie Shinyanga inayosimamiwa na Ibrahim Songoro ambaye pia anamiliki Songoro Media Production. 

Pamoja na mikakati kibao waliyonayo itakayoanza mwezi Desemba 05 mwaka huu,magwiji hao wa sanaa ya uigizaji na uongozaji wa filamu wameahidi kuja na mkakati utakaotengeneza wasanii wapya na kujenga misingi imara ya kiwanda cha filamu mkoa wa Shinyanga. 

Tayari wameanza na tamthilia fupi inayojulikana kwa jina la 'Vaisi Vesa' itakayokuwa inarushwa kwa njia ya mitandao ya kijamii kama vile youtube,instagram,whatsapp n.k. 

Wahusika wakuu katika tamthilia hiyo ni Ibrahim Songoro na Miss Grace,mwongozaji ni Masuka A.J na mpiga picha ni David Skerah. 

Mwandishi na mwongozaji wa tamthilia ya Vaisi Vesa,Amani Masuka amesema filamu hiyo imejaa visa mbalimbali vinavyotokea katika maisha ya binadamu vinavyotokana na watu wawili kupishana kauli. 

“Tamthilia ya Vaisi Vesa itakuwa inatoa visa vifupi ambavyo wahusika huwa wanatofautiana kauli ‘kauli tata’,itakuwa inahusisha watu wawili”,anaeleza Masuka. 

Amesema sehemu ya kwanza ya tamthiliya hii inaitwa “Wivu”,ambapo utata umeibuka kutokana na kauli ya “Ugonjwa usiokuwa na tiba”,ambapo mhusika mkuu Ibrahim Songoro anatafsiri ugonjwa usio na tiba kuwa ni Ukimwi ilhali binti aliyekuwa anamshawishi awe mpenzi wake akimaanisha ugonjwa usio na tiba kuwa ni wivu. 

“Hapo tunaona unafiki wa Songoro anayewakilisha wanaume walaghai akibadilika ghafla na kumshtumu binti huyo kuwa ni muuaji aliyekusudia kumwambukiza virusi vya Ukimwi”,anaeleza Masuka. 

“Binti anajitahidi kumwelewesha Songoro kuwa alimaanisha wivu,ndipo Songoro anarudi kinafiki na kuanza kujichekesha,hapa tunapata ujumbe kuwa siyo kila neno unaloambiwa unatakiwa kuliamini(wanawake),lakini pia kabla ya kuchukua maamuzi unapaswa kufikiria sana kabla ya kutoa uamuzi ulio sahihi (wanaume)”,ameongeza Masuka.

Akizungumzia tamthilia hiyo, mwenyekiti wa Bongo Movie Shinyanga Ibrahim Songoro “Songoro Gaddafi” amesema tamthiliya ya Vaisi Vesa imelenga kuielimisha,kuiburudisha na kuikosoa jamii katika masuala mbalimbali.

Kwa taarifa zaidi kuhusu tamthilia ya Vaisi Vesa na mambo mengine ya sanaa ya uigizaji wasiliana na Ibrahim Songoro kwa simu namba 0767831036 na Amani Masuka simu namba 0767856192.

Tumia dakika zako chache kutazama Tamthilia ya Vaisi Vesa hapa chini katika sehemu yake ya kwanza inayoitwa “Wivu”.




No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)