Pages

Shirika la Nyumba (NHC) lazindua sera mpya ya Mnunuzi Mpangaji maarufu kama “Tenant Purchase Scheme”

1
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Bw. Nehemia Mchechu akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya shirika hilo Upanga jijini Dar es salaam kuhusu uuzwaji mpya wa nyumba za shirika hilo kwa utaratibu wa sera mpya ya Mnunuzi Mpangaji maarufu kama “Tenant Purchase Scheme” ambayo ilitumika sana na Shirika lilipoanzishwa hadi mwishoni mwa miaka ya 1970.
2
Baadhi ya wakuu wa vitengo wa Shirika la Nyumba NHC kutoka kushoto ni Suzan Omary Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Itandula GambalagiMeneja Mauzo NHC na Meneja Biashara na Mipango Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Arden Kitomari wakiwa katika mkutano huo.
3
kulia ni Meneja wa Mauzo wa NHC Bw. Tuntufye Mwambusi akiakiwa pamoja na maofisa wengine wa shirika hilo wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari.
............................................................................
Shirika la Nyumba la Taifa linapenda kuutaarifu Umma wa Watanzania kuwa leo tarehe 07/11/2016 linazindua sera mpya ya Mnunuzi Mpangaji maarufu kama “Tenant Purchase Scheme” ambayo ilitumika sana Shirika lilipoanzishwa hadi mwishoni mwa miaka ya 1970.
Katika Sera hii ya Mnunuzi Mpangaji, mnunuzi atalipa kidogo kidogo kila mwezi (kiwango hutofautiana kulingana na bei ya nyumba na muda ambao mnunuzi mpangaji atatumia kulipa) kiwango kilichowekwa na kukubaliwa na Shirika na kiwango huhesabika kama gharama ya pango kwa mwezi na malipo ya kununulia nyumba na mnunuzi atahesabika kama mpangaji mpaka kiasi anacholipia kila mwezi kitakapofikia gharama ya nyumba, nyumba inakuwa yake rasmi na hukabidhiwa.
Sera hii itawasaidia Watanzania wengi ambao wana uwezo wa kulipia nyumba zao, lakini hawakidhi vigezo vya kibenki kuweza kupata Mkopo wa nyumba hizi zilizojengwa kwa ajili ya makazi katika mikoa ya Geita (Bombambili, Chato), Katavi (Ilembo, Inyonga), Dodoma (Kongwa), Ruvuma (Mkuzo), Kigoma (Mlole), Babati (Mrara), Singida (Unyankumi), Kagera (Muleba), Tabora (Uyui, Igunga) Arusha (Longido), Morogoro (Mvomero), Shinyanga (Bukondamoyo), Njombe (Makete), Mara (Buhare), Mtwara (Masasi), Mbeya (Mbarali) na Mkinga Tanga.
Chini ya utaratibu huu mpya unaoanza kutumika kuanzia Novemba 2016; Muombaji atapaswa kuainisha kwenye fomu ya maombi aina ya nyumba anayohitaji na Mkoa ilipo.
Sifa kuu ya Mnunuzi Mpangaji ni kwamba awe na Mshahara au kipato kinachozidi Shilingi 500,000 kwa mwezi. Mnunuzi Mpangaji atahitajika kulipa malipo ya awali ya asilimia Ishirini na tano (25%) ya thamani ya nyumba anayotarajia kununua (ikiwa na kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT).
Kiwango cha riba kitakuwa asilimia (15%) ya kiwango kilichosalia kuwekwa. Mnunuzi atahitajika kulipa malipo kwa mpango wa mwezi mmoja mmoja kulingana na thamani ya nyumba. Kiwango cha juu kabisa cha muda wa kulipa ni miezi 120 sawa na miaka kumi (10), Zaidi ya hayo malipo ya Bima ya Maisha ya asilimia moja (1%) na Bima ya Moto ya asilimia 0.077 yatalipwa mwanzoni mwa kila mwaka.
Kulingana na Mpango Mkakati wa Shirika la Nyumba la Taifa kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2024/2025, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), litajenga nyumba kwa ajili ya kuuza kwa wananchi wa aina zote za vipato; yaani wale wa vipato vya chini, vya kati na juu. Shirika litajenga nyumba 12,000 za gharama nafuu, nyumba 13,500 za kipato cha kati, nyumba 2,700 za kipato cha juu na nyumba 1,800 za bishara kufikia 2025.
Lengo kuu la Mpango Mkakati huu, ni kuliwezesha Shirika kujenga nyumba za makazi na biashara zipatazo 30,000 nchi nzima.
Bei za nyumba ni kati ya sh.29,000,000/= hadi sh.49,000,000/= (bila VAT). Bei hizi ni kulingana na ukubwa wa nyumba na mkoa nyumba ilipo. Ukubwa wa nyumba ni kuanzia vyumba viwili hadi vitatu.
Nyumba hizi za gharama nafuu zinajengwa nchi nzima zikiwa na lengo la msingi la kuwezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba za kuishi ambao hawawezi kujijengea nyumba kutokana na kuwa na kipato cha chini.
Wakati Shirika likijaribu kuweza kuongeza idadi ya nyumba za gharama nafuu huku Shirika likipata faida kidogo, Shirika pia lina lengo la kujenga nyumba katika maeneo yote ya nchi ili kufikia kila sehemu ya nchi, kikubwa zaidi ni kwamba litasaidia kujenga nyumba katika maeneo mapya na wilaya mpya zinazoanzishwa na Serikali.
Kwa kuongezea ni kwamba uendelezaji wa nyumba za gharama nafuu una athari nyingi chanya katika uchumi wa maeneo husika kwa mfano unachangia sana kukua kwa uchumi wa maeneo hayo kwa kutengeneza ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja, hivyo kupandisha kiwango cha maisha cha maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)