Pages

WAZIRI MKUU AONGOZA WANANCHI KUAGA MIILI YA WALIOKUFA KWA TETEMEKO

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba mjini kuaaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea jana (Jumamosi, 10 Septemba, 2016 mkoani Kagera.

Tetemeko hilo lilitokea jana Alasiri limesababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Kufuatia tukio hilo Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.

“Poleni sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu  Serikali ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo na hayafai kutumika.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi kulala uwanjani.

Pia Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuangalia kama kuna tetemeko linguine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu amesema kwa sasa wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba zao zimeanguka.Pia mkoa unaendelea kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Awali Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako majeruhi 170 wamelazwa na kutoa pole na kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hoispitali kubwa Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.
Waziri Mkuu Mh.Kassim Majaliwa akiwasili katika uwanja wa mpira wa Miguu wa Kaitaba mjini Bukoba mapema leo,kwa ajili ya kuwapa pole nyingi wakazi wa mji huo na kwingineko na pia kushiriki sala ya pamoja ya kuwaaga na kutoa heshima za mwisho kwa miili ya marehemu,waliokuwa wamekumbwa na tukio la tetemeko la Ardhi ambalo limetokea jana jioni na kupelekea idadi ya zaidi ya watu 15 akiwemo na mama mja mzito kupoteza maisha.

Tetemeko hilo kubwa la ardhi lenye mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 limetokea jana Septemba 10, 2016 katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa kadhalika nchi za Burundi na Uganda.Mikoa ya Kanda ya Ziwa iliyopata athari kwa mujibu wa taarifa ni Mwanza, Mara na Kagera nchini na kuripotiwa kuua zaidi ya watu 15 na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa sambamba na kubomoa majengo mbalimbali.
Pichani kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuelekeza jambo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu ,kabla ya kuanza sala ya pamoja ya kuwaaga na kutoa heshima za mwisho kwa miili ya marehemu,waliokumbwa na tukio la tetemeko la Ardhi ambalo limetokea jana jioni na kupelekea idadi ya zaidi ya watu 15 akiwemo na mama mja mzito kupoteza maisha.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuelekeza jambo Mbunge wa jimbo la BUkoba Mjini,Mh Wilfred Lwakatare,kabla ya kuanza sala ya pamoja ya kuwaaga na kutoa heshima za mwisho kwa miili ya marehemu,waliokumbwa na tukio la tetemeko la Ardhi ambalo limetokea jana jioni na kupelekea idadi ya zaidi ya watu 15 akiwemo na mama mja mzito kupoteza maisha. 

Baadhi ya ndugu na jamaa waliofika katika uwanja wa Kaitaba kushiriki sala ya pamoja ya kuwaaga wapendwa wao
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini akisoma majina ya masanduku yaliyobeba miili ya marehemu,tayari kwa kuagwa kwa pamoja katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini akiwa na baadhi ya viongozi wengine wa dini wakitazama majina ya masanduku yaliyobeba miili ya marehemu,tayari kwa kuagwa kwa pamoja katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini akiwa na baadhi ya viongozi wengine wa dini wakiwa katika uwanja wa Kaitaba kushiriki sala ya pamoja ya kuaga miili ya marehemu waliokumbwa na tetemeko la Ardhi hapo jana mjini Bukoba mkoani Kagera.
Baadhi ya Masanduku yenye miili ya marehemu walioathiriwa na tetemeko la Ardhi hapo jana mjini Bukoba mkoani Kagera.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)