Pages

MKUTANO WA 36 WA SADC UMEMALIZIKA NA TANZANIA YATEULIWA KUWA MWENYEKITI WA TROIKA

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka saini katika moja ya makubaliano yaliofanywa na nchi za SADC kwenye mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Lozitha, Mbabane nchini Swaziland.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto)akizungumza na  Makamu wa Rais wa Angola Mhe. Manuel Domingos Vicente wakati wa kuhitimisha mkutano wa 36 wa nchi za SADC mjini Mbabane Swaziland.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa kwenye mkutano wa 36 wa nchi 15 za SADC uliofanyika mjini Mbabane Swaziland, kulia ni Makamu wa Rais wa nchi ya Angola Mhe. Manuel Domingos Vicente na kushoto ni Waziri Mkuu wa Madagascar Mhe.Mahafaly Solonandrasana Olivier.
 Mwenyekiti wa SADC Mfalme Mswati wa III(kulia) akizungumza na Katibu Mkuu Mtendaji wa SADC Dr. Stergomena L. Tax wakati wa kuhitimisha mkutano wa 36 wa SADC mjini Mbabane,Swaziland.
 Mwenyekiti wa SADC Mfalme Mswati wa III akihutubia wakati wa kufunga mkutano 36 wa SADC mjini Mbabane ,Swaziland.


Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali umemalizika katika mjini Mbabane Swaziland ambapo Tanzania imeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi muhimu na nyeti ya Siasa, Ulinzi na USalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika- SADC- (SADC Organ On Politics, Defence and Security
Cooperation) ambapo nchi ya Angola imeteuliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa asasi hiyo.

Jukumu kubwa la asasi hiyo litakuwa ni kuangalia masuala yote yanahusiana na Siasa, ulinzi na usalama katika ukanda wa SADC huku changamoto kubwa ikiwa ni namna ya kutafuta suluhu ya kudumu hususani katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na Lesotho.

Akizungumzia mambo muhimu yaliyojiri kwenye Mkutano huo wa 36 wa SADC mjini Mbabane - Swaziland, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia  Suluhu Hassan ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli amesema mkutano huo umekuwa wa mafanikio makubwa na amehimiza ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa nchi wanachama wa SADC kwa sasa zinatakiwa kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi haraka kama hatua ya kujenga ustawi bora wa wananchi wa kanda hiyo.


Kuhusu Mpango wa Mfalme wa Swaziland wa III wa kujenga Chuo Kikuu cha SADC nchini mwake kabla ya mkutano ujao wa SADC hapo mwakani chuo ambacho kwa kuanzia kitatoa ufadhili wa masomo ya Sayansi,Ugunduzi na Utafiti kwa wanafunzi wanaotoka kwenye nchi wanachama wa SADC, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema mpango huo ni mzuri na utasaidia kutoa wataalamu wengi hasa wanasayansi katika ukanda wa SADC na serikali ya Tanzania inaunga mkono mkakati huo.

Kuhusu Tanzania kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa nchi za SADC, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa Dkt Augustine Mahiga amesema Tanzania itahudumu katika asasi hiyo kwa mwaka MMOJA na anaimani kuwa changamoto za kisiasa zilizopo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Lesotho zipatiwa ufumbuzi.

Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC pia umeiteua nchi ya Swaziland kuwa mwenyekiti wa SADC na Jamhuri ya Afrika Kusini imeteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC. Katika mkutano huo wakuu wa nchi na serikali wametia saini rasimu za maboresho ya mikataba mbalimbali ya jumuiya hiyo ikiwemo mkataba wa kuboresha itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya itifaki ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama ya SADC na maboresho ya itifaki ya biashara.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)