Pages

UKOSEFU WA MAARIFA YA VIPINDI VYA MABADILIKO YA MWILI KUNAATHIRI MAKUZI BORA KWA VIJANA

Ukosefu wa maarifa na taarifa sahihi wa vipindi vya mabadiliko maisha ya vijana husababisha uwezekano wa kupotoka kimaadili kwa kufanya mafunzo kwa vitendo na kuathiri makuzi bora.

Akitoa mafunzo kwa wanafunzi wanaounda vikundi vya kutayarisha vipindi vya redio kwa ajili kupaza sauti zao kuieleza Jamii kuhusu hali zao mashuleni, mamlaka mbalimbali, majumbani na katika Jamii wilayani Sengerema na Pangani, Afisa Mtaalam masuala ya Afya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Herman Mathias alisema kwamba changamoto nyingi zinazoathiri makuzi ya kimaadili kwa vijana ni kutopewa maarifa na taarifa sahihi jinsi ya kutumia miili yao bila kuathiri ndoto zao.

“Vijana wengi wameshindwa kufikia ndoto zao kutokana na kutomaliza shule kwa sababu hawajui namna ya kufanya maamuzi sahihi kutumia fursa walizo nazo”, alisema Herman Mathias.
Mwezeshaji Herman Mathias kutoka UNESCO akitoa somo kwa washiriki wa Shule za Sekondari Sengerema.

Ili kufikia malengo ya ndoto zao Afisa huyo wa UNESCO alisema vijana wanahitaji kusoma kwa bidii na kuhitimisha mzunguko wa elimu, kuwa na tabia njema kwa kuepuka vishawishi vya mtaani hususan kuvuta bangi na matumizi ya vileo, utoro na matumizi ya lugha mbaya.

Alizitaja tabia njema nyingine pamoja na kuepuka tabia za kimapenzi yanayoweza kusababisha magonjwa ya zinaa, maambikizi ya virusi vya UKIMWI na ujauzito na upatikanaji wa malezi yanayojali nafasi na muda wa mtoto na kuweka mazingira rafiki ya kuishi na kusoma, afya bora kwa kutougua hovyo magonjwa mbalimbali na kuwa msafi wakati wote hali inayompa fursa kijana kushiri katika shughuli zote za kijamii na kielimu na kuwataka wazazi na walezi kufuatilia mwenendo wa kijana shuleni na katika Jamii.

Zaidi ya asilimia 52 ya vijana hawana elimu ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na afya ya uzazi.

Alisema kwamba mambo hayo yote yanawezekana kuepukika kwa sababu yako ndani ya uwezo wa vijana wenyewe na wazazi pia.
Washiriki wakichangia mawazo na uzoefu wao kuhusu changamoto zinazowakabili.

Wakichangia uzeofu wao unaowakwamisha kufikia ndoto zao, vijana hao walizitaja changamoto zinaowakumba katika kipindi cha makuzi ambazo ni mimba za utotoni zinazosababishwa na ukosefu wa elimu ya uzazi kuanzia shuleni na au katika familia, umaskini unaosababisha wasichana kutoka nje na kujiingiza katika matendo ya kimapenzi kwa kutafuta mahitaji mbalimbali muhimu na matamanio kukidhi matakwa yao kimaisha na makundi rika ambayo huchangia katika kushawishiana na kufundishana mabaya.

“Zaidi wa watoto 6,000 wanaacha masomo kutokana na ujauzito na mara nyingi waalimu wamekuwa hawaripoti taarifa za mimba badala yake huripoti utoro peke yake, lakini wanafunzi wanaelewa hali halisi na kuweza kueleza ukweli”, alisema Herman Mathias.
Kijarida kilichoandaliwa kama matokeo ya nadharia kwa vitendo.

Changamoto nyingine ni tamaa inayopita kiasi kwa kuona baadhi ya marafiki zao wanakuwa na vitu vizuri ambavyo wengine huvikosa hususan simu za mkononi, viatu na nguo nzuri, kubakwa na matumizi mabaya ya mawasiliano ya utandawazi na vifaa vya kielektroniki zinazopatikana kwa njia zisizo halali.

Matumizi mabaya ya utandawazi hushawishi vijana kuiga utamaduni wa kigeni hususan kuvaa nguo zisizo na maadili na vitendo vingine vinavyoenda kinyume na maadili ya Mtanzania na malezi yanayowapa vijana uhuru mkubwa wa kufanya mambo yao bila kurekebishwa au kuingiliwa na wazazi na walezi ni changamoto inayochangia kupotosha maadili katika makuzi ya kijana.
Wanafunzi washiriki wakifanya zoezi la viungo wakishirikiana na Mwezeshaji Herman Mathias.

Ndoa za utotoni zinazosababishwa na mila na desturi zinazoendelezwa katika Jamii kwa kiasi kikubwa zinachangia kufifisha vijana kufikia malengo ya ndoto zao na mimba za utotoni husababisha ulemavu wa mwili na akili na pia vifo kwa mama na mtoto.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 179 zilizokubaliana kutekeleza Mkakati wa Utekelezaji Mkutano wa Kimataifa wa Tatu na Maendeleo wa Cairo (UNFPA) mwaka 1994 wa harakati za maendelezo ya haki za uzazi, uzazi wa mpango, uzuiaji wa maambukizi ya VVU/UKIMWI, uwezeshwaji wa wanawake na maendeleo mengine yanayohusiana na hayo kulinda utimilifu wa kibailojia, kisaikolojia wa namna ambavyo mfumo wa uzazi unafanya kazi. Haki hizo zikipotea mtoto ana haki ya kupaza sauti kudai.

UNESCO kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Redio Jamii ya wilaya ya Sengerema na Pangani, iliendesha warsha za kuwajengea uwezo vijana wa shule za Sekondari wilayani Sengerema na Shule za Msingi wilayani Pangani kupitia vikundi rika maarifa na ujuzi wa elimu ya afya ya uzazi na makuzi yao kupitia redio Jamii ili waelimike kabla ya kuandaa vipindi.

Afya ya uzazi inahusisha mfumo wa uzazi wa mtu na via vya uzazi kwa watu ambao unajumuisha uzazi na ujinsia, kuingia utu uzima, mahusiano, mimba, maambukizi ya virusi vya UKIMWI/UKIMWI na dawa za kulevya.

Pamoja na elimu ya afya ya uzazi, vijana pia waliweza kupata mafunzo ya msingi ya uandishi wa habari na utangazaji ili kuandika na kutayarisha vipindi vya redio, vijarida na midahalo kwa ajili ya kuwasiliana kutoka rika moja hadi jingine kuelimishana, kukemea, kudai na kukumbushana haki zao.
Wanafunzi wa Shule za Msingi Pangani wakiwa katika ziara ya kutembelea kituo Redio Jamii Pangani FM wakati wa mazoezi.

Elimu rika kupitia vikundi vya vijana katika redio ni mpango wa majaribio katika wilaya ya Sengerema na Pangani ambao mafanikio yake yataendelezwa katika sehemu nyingine hususan Kahama, Isaka, Micheweni, Simanjiro na Loliondo.

Vikundi hivyo ni fursa ya kuwajengea misingi ya ajira ya uandishi wa habari iwapo wataitumia vizuri kwa kushirikiana na vituo vya redio Jamii vilivyoteuliwa kuandaa na kutayarisha vipindi, kushirikiana na wenzao kurekodi majadiliano na kuwa wabunifu wa kuandaa vijarida kwa ajili ya kutoa elimu rika kuhusu afya ya uzazi na malezi.
Picha ya pamoja wanafunzi wa Shule za Msingi Boza na Kikokwe Pangani, walezi, wajumbe wa kamati za shule na viongozi kutoka Wizara ya Elimu.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)