Pages

Ujio wa ndege mpya: ATCL yajipanga kuleta mapinduzi ya usafiri wa anga.


Baadhiya mafundi wa kampuni ya kutengeneza ndege ya Bombardier ya nchini  Canada wakiendelea kuipaka rangi moja ya ndege mpya za Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) nchini humo hivi karibuni. Ndege hizo zinatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Septemba mwaka huu zikipishana kwa wiki moja.

Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) limesema ujio wa ndege zake mpya
mbili aina ya Bombardier Q400 zinazotarajiwa kuingia hapa nchini siku
chache zijazo, utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa
shirika hilo, huku shukrani zaidi zikielekezwa kwa Rais John Joseph
Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kufufua shirika hilo.

Akizungumza kupitia taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es  Salaam jana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la hilo Muhandisi  Patrick Itule alisema ujio wa ndege hizo utalirejesha shirika hilo
kwenye biashara ya ushindani dhidi ya makampuni mengine ya ndege hapa
nchini.

Ndege hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Bombardier ya  nchini Canada zinatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu na ya nne ya  mwezi Septemba mwaka huu zikipishana kwa wiki moja.

“Baada ya  ujio wa ndege hizi hatuoni tena sababu ya sisi kukwama na tutakuwa  tumeingia rasmi kwenye biashara ya ushindani kwa kuwa changamoto kubwa  ya uhaba wa ndege ambayo imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa itakuwa imeanza kutatuliwa,’’ alibainisha Muhandisi Itule huku akisisitiza kuwa  shirika hilo halitakuwa tayari kuwavumilia wafanyakazi watakaoshindwa  kuendana na kasi ya mabadiliko ya sasa.

Alisema shirika hilo  tayari limeunda kikosi kazi kinachosimamia masuala mbalimbali likiwemo  suala la mafunzo ya watendaji wake mbalimbali ili kuendana na matakwa ya biashara hiyo kwasasa.

“Tumejipanga kuboresha mfumo mzima wa  utendaji kazi na hiyo ni kuanzia mfumo wa ukataji tiketi na huduma zote muhimu kwa wateja ndio maana kwasasa tunawekeza zaidi kwenye ubora wa  rasilimali watu ili kuwavutia zaidi wateja…uvutiaji ambao utaambatana na utoaji huduma kwa gharama nafuu,’’ aliongeza.

Akizungumzia uwezo wa ndege hizo, Afisa Biashara wa shirika hilo Bw Josephat Kagirwa  alisema zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na kwamba ujio wake  utaongeza njia za kusafiri kwa shirika hilo kutoka njia mbili za sasa  hadi kufikia njia zaidi ya kumi.

“Tutakuwa na madaraja mawili  yaani daraja la uchumi (Economy Class) litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara (Business Class) litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege. Kwa ujio wa ndege hizi tutaweza kuongeza safari za ndani na  baadae mwakani itakapopatikana ndege ya tatu kama Mheshimiwa Rais  alivyoahidi ndipo tutaanza safari za nje ya nchi tukianza na nchi  jirani,’’ alibainisha.

Alitaja baadhi ya mikoa ambayo shirika  hilo litaboresha zaidi safari zake kuwa ni pamoja na Dodoma, Mwanza,  Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar,  Pemba, Bukoba pamoja na Visiwa vya Comoro. Hata hivyo alisisitiza  kwamba safari hizo katika maeneo tajwa na kwingineko zitaanzishwa baada  ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu.

“Lengo ni kuhakikisha  tunakuwa tayari kutoa huduma nje ya nchi ndani ya muda mfupi  iwezekanavyo ili tuweze kutimiza wajibu wetu kama shirika la ndege la  taifa kwa kutangaza nembo ya taifa letu nje ya nchi, kusafirisha
watanzania sambamba na kukuza utalii kwa kuwaingiza na kuwasambaza
watalii ndani na nje ya nchi kwa urahisi,’’ alisema.

Hata hivyo  Bw Josephat alisema mabadiliko hayo yanaambatana na changamoto kadhaa  huku akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uhaba wa wataalamu wa  kutosha kuendana na kasi waliyojiwekea, gharama kubwa katika uwekezaji  wa teknolojia ya kisasa na gharama za vipuri na mabadiliko ya mara kwa  mara yanayochangiwa na ushindani katika biashara ya anga.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)